Home

  • Unachohofia mara nyingi huwa hakipo.

    Mara nyingi kile tunachohofia hata huwa hakitokei. Ni sisi tu binadamu huwa tunatengeneza mazingira ya hofu ambazo hata kiuhalisia hazipo.

    Hofu huwa tunatengeneza akilini. Baada ya kuijaza hofu akilini mwili unapokea matokeo yake na hapo tunashindwa kuthubutu na kufanya kile tulichochagua kufanya.

    Dawa ya hofu ni kukabiliana nalo mzima mzima, bila kujali nini kitatokea hata unachohofia saa zingine huwa hakitokei katika hali ya kawaida.

    Twapaswa kutokuwa na hofu wowote, bali tuiachie asili ifanye kazi yake. Kama asili imepanga kutokea itatokea tu, na kama haijapanga kutokea haitatokea.

    Hivyo usijali sana ni nini kitatokea baada ya kufanya kitu unachohofia sana, wewe fanya tu na matokeo yatakuja yenyewe.

    Hatua ya kuchukua leo, usiwe na hofu, mara nyingi kile unachohofia huwa hakipo. Timiza wajibu wako acha kufikiria juu ya hofu.

    Ukiwa mtu wa kujali hofu, hutaishi kwa amani, utakuwa na wasiwasi siku zote unapoamua kuchukua hatua fulani ya mafanikio.

    Kuishi mara nyingi inahitaji ujasiri ili kuweza kukabiliana na hofu, ukiwa jasiri dunia itakuheshimu na kukupa unachohitaji, ukiwa mnyonge dunia itakuonea.

    Mimi wako akujaliaye.

    Maureen Kemei

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com

  • Kupata tumaini la maisha.

    Zawadi tuliyopewa sisi wanadamu siyo kuona bali kuwa na maono makubwa juu ya maisha tunayotamani kuyaishi. Lakini, ni muhimu pia kufurahia kile ulicho nacho wakati unapambana kupata kilicho kubwa zaidi.

    Hapo ndipo chanzo cha tumaini kinaanza, kufurahia ulichonacho huku ukiwa makini usiridhike sana na hapo ulipo. Unapambana kufikia ndoto na maono yako makubwa.

    Hiyo ni njia ya kwanza kabisa ya kuondokana na matatizo au msongo yanayoweza kukukwamisha. Kuwa na ndoto kubwa au maono makubwa yanayokuwajibisha kwelikweli. Litakufanya uwe ‘bize’ wakati wote kukimbiza ndoto yako na usumbufu wowote ule hakutakuwa na nafasi kwako.

    Hatua ya kuchukua leo, kwa vile sisi binadamu tumetumwa hapa duniani kukamilisha kitu maalumu, tunahitaji kujiwekea malengo makubwa na yanayotimika.

    Hii ni njia mojawapo ya kufahamu ni nini hasa tunapaswa kutimiza kabla masiku yetu hayajaisha hapa duniani. Na hapo tunapata tumaini ya kesho bora au mwisho wetu kuwa bora.

    Mimi akujaliye.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com

  • Unatumiaje muda wako?

    Karibu, nikushirikishe ninayojifunza kutoka kitabu cha Pata masaa mawili ya ziada kila siku. Kilichoandikwa na kocha Makirita Amani.

    Japokuwa wote tuna masaa 24 kwa siku, matumizi yetu hayafanani. Wapo wanaotumia vizuri muda wao na wanaofanikiwa na wale wanaoshindwa wanatumia vibaya.

    Chochote unachofanya kwenye maisha yako ili kuongeza kipato, Kuna muda ambao unatumia kwenye shughuli hiyo na kuna muda ambao unabaki baada ya kuondoa muda huo wa kazi.

    Muda huu ndio unaotofautisha wale wanaobaki chini wakiwa na maisha magumu na wale wanaonzia chini lakini baada ya muda wanakuwa juu.

    Mwandishi Brian Tracy alinukuliwa akisema kuwa kwenye jamii zetu unafanya kazi kwa masaa nane kwa siku kwa ajili ya kuishi (survive). Muda wowote unaoongeza zaidi ya masaa haya ni kwa ajili ya mafanikio (success).

    Huu ni ukweli maanake kama utatumia masaa nane kufanya kazi, huku masaa zinazobaki unatumia hovyo, utashangaa wengine wanaotumia vizuri wakipika hatua huku wewe ukibaki palepale.

    Hatua ya kuchukua leo tumefahamu na kujua umuhimu wa kuwa na muda tofauti na wa kazi. Ambao tunaweza kuutumia vizuri kutengeneza maisha tunayotaka.

    Tumeweza kuona ni namna gani ni muhimu kwetu kuwa na muda wa ziada kwa ajili ya kufanya mambo muhimu ya maisha yetu.

    Ni mimi akujaliye.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com.

  • Zawadi ambayo tumepewa kwa usawa.

    Rafiki, karibu nikushirikishe yale ninayojifunza kutoka kitabu pendwa kiitwacho Pata masaa mawili ya ziada kila siku. Kilichoandikwa na Kocha Makirita Amani.

    Mwandishi anaanza kwa kusema tumepewa zawadi ya muda kwa usawa kabisa, ni sisi wenyewe tunachagua tuitumieje zawadi hii ya kipekee.

    Mwandishi anaendelea kusema hakuna anayeweza kukunyima muda au kununua ya ziada hata kama ana hela kiasi gani.

    Anasema kama huna hela unaweza kumkopa mtu hela ukapata, lakini huwezi kopa muda, kama umepoteza umepoteza au kama umetumia vizuri imekufaidi.

    Anasema kuwa huwezi kamwe kukopa muda wa kesho utumie leo wala kutumia akiba wa Jana leo. Kwani hali hii inafanya muda kuwa wa thamani na wa kipekee sana.

    Hatua ya kuchukua leo kwa sababu tumejifunza kuwa muda ni wa thamani na wa kipekee, inabidi tuwe makini nao, tusiruhusu usumbufu wowote itufanye tukapoteza muda wetu.

    Mimi wako akujaliye.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com.

  • Kutafuta thamani yako.

    Unapaswa ujue kuwa uwezo wako upo wapi alafu utapeleka nguvu zako pale ambapo uwezo wako upo.

    Itambue thamani yako baada ya kujua usiache thamani yako ipotee bila kutumika au kwa lugha rahisi usitumie thamani chini ya viwango.

    Binadamu ana bahati sana maana ana uwezo mkubwa ulioko ndani yake. Hakuna kitu ambacho binadamu hawezi ni ile tu hajaamua.

    Licha ya kwamba binadamu tumebarikiwa kuwa na uwezo mkubwa ndani yetu, lakini cha ajabu ni wachache mno ambao wanaweza kugundua na kutumia uwezo huo vizuri.

    Hatua ya kuchukua leo, twende tukatumie uwezo wetu vizuri, tuepuka kujidhalilisha kwa kujiweka viwango vya chini, wakati wewe ni mtu wa viwango vya juu.

    Jiamini, kuwa na mtazamo chanya, amini mambo mazuri yanakwenda kutokea leo katika maisha yako.

    Mimi wako akujaliye.

    Maureen Kemei

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com

  • Kupenda unachofanya.

    Watu wote tunaowaona wana mafanikio makubwa walianza kwa kupenda kile wanachofanya. Hakuna kikubwa ambacho kimewahi kufanywa na mtu ambaye hana mapenzi ya kweli kwenye kile anachofanya.

    Inasemekana kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, kama unataka kufanya makubwa na kuacha alama hapa duniani, lazima kwanza upende kile ambacho unakifanya.

    Hao ambao wamefanikiwa walipokuwa wanaanza walikatishwa tamaa na wengine, walikutana na mambo magumu, changamoto na hata kushindwa. Lakini hawakukata tamaa, kwa sababu ni kitu ambacho walikipenda kweli, kitu ambacho kilitoka ndani yao.

    Hatua ya kuchukua leo kama unataka kuwa zaidi ya ulivyo sasa, basi lazima upende sana kile unachokifanya.

    Upendo una nguvu kubwa Sana, nguvu ya kuvunja kila aina ya kikwazo na changamoto, nguvu ya kukuwezesha Kuendelea hata pale unapokuwa umechoka na kukaribia kukata tamaa.

    Mimi wako anayekujali.

    Maureen Kemei.

    Mshauri na Mwandishi.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com.

  • Umuhimu wa kuwa king’ang’anizi.

    Sifa pekee inayowatofautisha washindi na wale ambao wanashindwa ni uvumilivu na ung’ang’anizi.

    Kama kweli mtu umekadiria au umeamua kutoka ndani yako kwamba lazima nifikie mafanikio makubwa. Utajitoa kweli kwenye kile unachokifanya na utapambania hadi ufanikishe jambo hilo.

    Unapokutana na changamoto au kikwazo njiani, kwa vile uliamua kweli kupambana changamoto hizo haziwezi kukutoa. Lakini kama uliamua kwa kuangalia wengine wanafanya nini ukikutana na magumu yoyote lazima tu yatakutoa.

    Unapoamua kuwa king’ang’anizi utapata upinzani mkubwa kutoka kwa familia yako, marafiki, na ata mwenzi wako, kwa maana wanaona unafanya kilicho tofauti na wao. Hivyo wanajaribu kukurudisha kwenye ukawaida katika hali kama hii uvumilivu na king’ang’anizi ni muhimu kuliko vingine vyote.

    Unapaswa kufahamu kwamba vikwazo hivi ni vipimo tu, kama kweli umejitoa au upo tayari kutoa chochote kile ulichonacho ili kupata mafanikio unaotaka.

    Tunajifunza leo kwamba kile tumeamua kufanya kwenye maisha ni vizuri tujitoe kweli, tung’ang’anie yale tunayofanya na hatimaye tutafikia kwenye uhuru wa maisha ambao ni mafanikio.

    Imeandikwa na mwandishi na mshauri.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com.

  • Badili mtazamo.

    Mzizi wa mambo yote ni kubadili mtazamo au fikra zetu,kama tunataka kweli kufanikiwa.

    Matatizo mengi yanayowakumba watu yanaazia kwenye fikra. Wanasema kuwa, unakuwa vile unavyofikiria, kumbe basi eneo la kufikiri ni eneo moja muhimu sana. Kwa hivyo ni busara mno kujiwazia au kujitamkia mazuri.

    Ili tuweze kubadili asili ya vitu, iwe ni ndani yetu au kwa wengine, tunatakiwa kubadili mawazo au fikra zetu na siyo matukio.

    Tunapaswa kubadilisha fikra zetu ambazo ndizo zinaumba matukio tunazokutana nazo.

    Hatua tunayochukua leo, kubadilisha fikra na mawazo. Tuwe makini na kile tunachowaza kwani asili inatupa kile tunachowaza mara nyingi.

    Kwa hiyo, tusipambane na hali zinazotutokea bali tupambane na fikra zinazotuletea matokeo ambazo ni mazuri kwetu.

    Imeandikwa na mwandishi na mshauri.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com.

  • Kutambua mchango wako kwenye yote unayopitia.

    Kwenye maisha ni rahisi sana kulalamika na kuwalaumu wengine pale tunapokutana na matatizo au changamoto fulani kwenye maisha.

    Labda watu wamekudanganya, wamekuibia, wamekusaliti au kukutelekeza. Ni rahisi kulaumu wengine na kufarijika na lawama hizo. Ila haitakuwa na msaada wowote kwako.

    Njia bora ya kukabiliana na hali ya kulalamika na kulaumu ni kuchukulia kila kitu ni makosa yako. Hata kama mtu kakudanganya, ni wewe umempa nafasi mpaka akakudanganya, ni wewe mwenyewe umemwamini.

    Kuchukulia kila kitu ni makosa yako ni bora kuliko hata kusamehe. Maana unaposamehe bado unakuwa unaamini Uliyemsamehe ndiye mwenye makosa. Lakini unapokubali kila kitu ni makosa yako, unajiondoa kwenye hali ya mambo fulani kujirudia rudia kwako.

    Hili linakupa nguvu kubwa ya kuona kila kitu ni wajibu wako hivyo utachukua hatua sahihi na kuweza kujiboresha mwenyewe.

    Imeandikwa na mwandishi na mshauri.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com.

  • Kujiandaa kukabiliana na mabaya.

    Katika maisha lazima tujiandae kukabiliana na mabaya, katika falsafa ya Ustoa tunafundishwa kila mmoja ajiandae kukabiliana na mabaya.

    Tunapojiandaa na mabaya hata yakija kutokea hayatakuja kuumiza sana yatatukuta tumejiandaa vizuri.

    Chochote kinaweza kutokea, hivyo iandae akili yako kupokea ata yale mambo hasi ambayo hukutekemea kuyapata.

    Mfano, kama umeajiriwa ikitokea umefukuzwa kazi maisha yako yatakuwaje? Falsafa inatufundisha hapa kujiandaa kuzoea hali ambayo hatujawahi kutegemea kuipata na hata ukiipata hutopata shida maana tayari utakua umeshaizoea.

    Dunia ina mazuri na mabaya. Siku yoyote mambo yanaweza kubadilika hivyo ni muhimu kujiandaa kwa lolote litakalotokea na namna ya kulikabili hilo jambo.

    Hatua ya kuchukua leo ;jiandae kukabiliana na mabaya. Kama umetegemea kupata jiandae hata ukiikosa kiakili na ukija kukosa utasema nilishalijua hili na halitakuumiza kama yule mtu aliyeweka matumaini yote.

    Unapojiandaa kwa hali zote unakuwa imara na huwezi kuangushwa na kitu chochote kile.

    Imeandikwa na mwandishi na mshauri.

    Maureen Kemei.

    Blog;kufikirichanya.wordpress.com.

    Email, kemeimaureen7@gmail.com.