Home

  • Kwa nini tunapaswa kukataa kuzuiwa na hofu.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini matajiri huwa wanachukua hatua licha ya kuwa na hofu, wanajua njia ya kuishinda hofu ni kufanya kile wanachohofia.

    Ni kwa njia hiyo wamekuwa wanazalisha matokeo makubwa na ya tofauti kabisa. Masikini wamekuwa wanaruhusu hofu iwe kikwazo kwao, wanapanga kuchukua hatua na hofu inapowajia, wanaacha kufanya.

    Safari ya kufikia mafanikio makubwa siyo rahisi. Ni safari iliyojaa vikwazo na changamoto za kila aina. Vikwazo na changamoto hizo ndiyo vimekuwa vinawazuia wengi wasifikie utajiri kwa sababu hawapo tayari kukabiliana na magumu hayo.

    Wanaofika kwenye utajiri na mafanikio makubwa ni wale ambao hawakubali kitu chochote kile kiwe kikwazo kwao.

    Hawayakimbii magumu, bali wanayakabili kwa kuwa wameshajiambia watafikia utajiri au watakufa wakipambana.

    Maskini huwa wanaruhusu kila kikwazo kuwa sababu ya wao kutokufanya, wanapanga vizuri, ila wanapoanza na kukutana na vikwazo, huo ndiyo unakuwa mwisho wao.

    Hatua ya kuchukua; rafiki yangu orodhesha ni mambo gani yanayokupa hofu sana kwenye safari yako ya kuelekea kwenye utajiri na mafanikio makubwa kisha weka mkakati wa kuyakabili.

    Kila siku tunapaswa kufanya nje ya mazoea, kufanya kitu ambacho hatujazoea kufanya na tunakihofia, hata kama ni kidogo kiasi gani. Haya madogo tunayofanya kila siku yatajenga ujasiri mkubwa ndani yetu.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Umuhimu wa kuwaelewa wengine.

    Rafiki yangu mpendwa tabia inayowafanya watu kuwa na ufanisi mkubwa ni kuwa msikilizaji mzuri kutoka kwenye kitabu cha habits of highly effective people.

    Mwandishi anatueleza kuwa mawasiliano ni muhimu sana katika kila eneo la maisha, kuanzia kazi, biashara, ndoa, familia na hata urafiki.

    Mawasiliano yamekuwa changamoto kwa wengi kwa sababu tunafundishwa kuongea, ila kuna kimoja muhimu sana huwa hatufundishwi nacho ni KUSIKILIZA.

    Kusikiliza ni changamoto kubwa sana kwa wengi, kwanza wengi huwa hatusikilizi tunafikiria tutawajibuje wakishamaliza.

    Watu wenye ufanisi mkubwa ni wasikilizaji wazuri sana, na hawasikilizi tu kwa masikio, lakini pia wanatumia macho yao na uelewa wao.

    Wanajua sehemu kubwa ya mazungumzo haipo kwenye maneno yanayoongelewa, bali pia kwenye sauti na kwenye matendo ya mtu wakati anaongea lugha ya mwili.

    Watu wenye ufanisi mkubwa wanatumia muda wao mwingi kuwasikiliza wengine, na wanasikiliza kwa lengo la kuwaelewa. Kwa njia hii wanajua ni nini hasa watu wanataka na hivyo kuweza kuwapatia au kuiboresha mahusiano zaidi.

    Watu wenye ufanisi mkubwa, kabla hawajatoa maoni yao, kabla hawajatoa ushauri wao huwa wanasikiliza kwanza na kujua ni nini hasa kinawasilishwa pale. Wasiokuwa na ufanisi husikiliza juu juu na kukimbilia kuhukumu au kutoa ushauri, kitu ambacho kinaharibu kabisa mawasiliano yaliyopo.

    Watu wasio na ufanisi mkubwa, husikiliza kwa kutumia uelewa wao wenyewe na huwa wanatumia njia hizi nne kuwajibu wale wanaowasiliana nao;

    1. Moja ni wanatathmini kile ambacho mtu anaongea, hivyo wanaamua kukubali au kukataa.
    2. Pili wanachimba zaidi kwa kuuliza maswali ya kuhoji, kutokana na uelewa wao wenyewe.
    3. Tatu wanashauri kulingana na uelewa wao na uzoefu wao wenyewe.
    4. Nne wanatafsiri, kujaribu kufikiria watu wana ni nini kingine wanataka au kinawasukuma.

    Hatua ya kuchukua; Rafiki yangu boresha mawasiliano yako na wengine kwa kujifunza kuwa msikilizaji. Awe mtu yeyote yule, mteja,bosi wako, mfanyakazi wako, mwenza wako, mtoto wako.

    Usikimbilie kutoa hukumu au kushauri, usimsikilize ukiwa tayari una upande wako, badala yake sikiliza kuelewa badala kuhitimu na hukumu.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Jinsi ya kuwa makini na mwenye maono.

    Rafiki yangu mpendwa watu wote wenye ufanisi mkubwa na ambao wanafikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao ni watu makini.

    Ni watu ambao wana maono kwenye maisha yao na wanayaishi maono hayo. Watu hawa wanajua ni nini wanachotaka kwenye maisha, na wanakifanya kazi kila siku.

    Watu wenye ufanisi mkubwa wanajua ya kwamba maisha yao ni jukumu lako na hivyo wanachukua hatua katika kuyafanya yawe bora. Hawalalamiki wala kulaumu wengine, badala yake kama kuna kitu hakipo sawa wanachukua hatua.

    Lakini wale wanaokosa ufanisi mara zote huangalia ni nini wamekosa na kuanza kutafuta watu wa kulaumu au kulalamika.

    Mtu mwenyewe ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya maisha yao, haijalishi ni kitu gani kimetokea, maamuzi ya mtu ndiyo yanayopelekea kufaidika au kutofaidika.

    Hata kama mtu amekutukana, siyo tusi ambalo litakuumiza wewe, bali iwe maana ya tusi unavyoichukulia. Watu wenye ufanisi hawaruhusu hali za nje kuwavuruga, wasiokuwa na ufanisi huvurugwa na kila kinachotokea kwenye mazingira yao.

    Watu wenye ufanisi mkubwa wanajua matatizo yote tunayokutana nayo kwenye maisha yetu kwenye makundi matatu;

    1. Matatizo ambayo yanatuhusu sisi moja kwa moja, ambayo yanatokana na tabia zetu au matendo yetu, haya wanayafanyia kazi mara moja.
    2. Kundi la pili ni matatizo ambayo hayatuhusu moja kwa moja, ambayo yanatokana na matendo ya wengine; haya huyashughulikia kwa kubadili mtazamo wao.
    3. Kundi la tatu ni matatizo ambayo yako nje ya uwezo wetu, ambayo hatuwezi kufanya chochote, haya wanaachana nayo. Wasio na ufanisi wanachanganywa na kila tatizo.

    Kuchukua hatua; rafiki yangu amua kuchukua hatamu ya maisha yako, amua kupanga ni jinsi gani maisha yako unataka yaende.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Ni nini adui wa mafanikio yako?

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kila kitu kizuri chenye manufaa huwa kinakuwa na maadui wake.

    Kadhalika ufanisi wa hali ya juu huwa unakuwa na maadui ambao unapaswa kuwajua na kuwashinda ili uweze kujijengea hali hizo mara kwa mara na kufanya makubwa.

    Adui wa kwanza ni kufanya mambo mengi kwa pamoja. Huwezi kuzama kwenye ufanisi wa juu kama akili yako inahangaika na mambo mengi kwa wakati mmoja. Chagua kufanya jambo moja tu kwa wakati na achana na mengine yote katika wakati huo.

    Adui wa pili ni msongo. Msongo wa mawazo huwa unaondoa umakini wa mtu kwenye kile anachofanya na kuupeleka kwenye mambo mengine yanayomsumbua.

    Kabiliana na yale maeneo ya maisha yako yanayokupa sana msongo, iwe ni kazi, mahusiano au afya, tatua vyanzo vyote vya msongo.

    Na pia unapopanga kufanya kitu ambacho unataka kuzama kwenye ufanisi wa juu, sahau yote yanayokupa msongo katika wakati huo. Jiambie unajipa muda mfupi wa kusahau yote yanayokusumbua na kuweka umakini wako wote kwenye kile unachofanya.

    Adui wa tatu ni hofu ya kushindwa. Kutaka ukamilishaji ni kikwazo kikubwa kufika kwenye ufanisi wa juu. Kama unataka kufanya kwa ukamilifu mkubwa, kama unaona kukosea au kushindwa ni fedheha kubwa, umakini wako utaenda zaidi kwenye hofu ya kushindwa kuliko kufanya kitu husika.

    Sahahu kuhusu ukamilishaji, acha kufikiria kushindwa. Wewe fikiria kile tu unachofanya na hapo utaweza kuzama kwenye ufanisi wa juu.

    Adui wa nne ni kutokuamini kile unachokifanya. Kama huamini kweli kwenye kile unachofanya, kama hujiamini kwamba unaweza kukifanya, hutaweza kuzama kwenye ufanisi wa juu.

    Amini kwenye kile unachofanya kwamba ni muhimu, na kinawezekana. Jiamini kwamba una uwezo wa kukifanya, ujuzi na maarifa yote muhimu. Kwa kuwa na Imani hivyo, utaweza kuzama kwenye ufanisi wa juu na kufafanua makubwa.

    Kuchukua hatua Ili uweze kufanya makubwa na kuondoa kila aina ya ukomo kwenye maisha yako, jijengee hali hizo za ufanisi wa juu kwenye yale makubwa unayofanya.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Misingi minne ya kufanya Kwa kusudi.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kuna njia mbili za kufanya chochote unachofanya. Njia ya kwanza ni kufanya kwa mazoea, hapa unafanya kama unavyozoea na hujisukumi kujaribu kitu chochote kipya.

    Kwa njia hii hujifunzi chochote kipya wala hujaribu chochote cha tofauti. Kufanya kwa mazoea ndipo wengi wanakwama na kushindwa kupiga hatua kwenye kile wanachofanya.

    Njia ya pili ni kufanya kwa kusudi. Hapa unaondoa mazoea na kufanya kwa utofauti. Unajifunza njia mpya za kufanya na kujaribu vitu vya tofauti.

    Kwa njia hii unajisukuma kutoka kwenye mazoea, kitu ambacho siyo rahisi, lakini kina matokeo mazuri.

    Wote wanaobobea na kufanikiwa kwenye kile wanachofanya, wanatumia njia hii ya kufanya kwa kusudi.

    Ili kufanya kwa kusudi, unahitaji kujijengea misingi mikuu minne.

    1. Msingi wa kwanza ni kujifunza kusiko na ukomo. Lazima kila wakati uwe tayari kujifunza vitu vipya kwenye kile unachofanya. Hata siku moja usijione kwamba unajua kila kitu.
    2. Msingi wa pili ni kuweka juhudi na umakini kwenye kile unachofanya. Hapa unaweka juhudi na umakini mkubwa kwenye kufanya. Hapa ndipo unapoondoa mazoea kabisa.
    3. Msingi wa tatu ni kupata mrejesho wa kweli kutoka kwa watu sahihi. Unahitaji watu ambao wamebobea kwenye kile unachofanya na ambao wapo tayari kukupa mrejesho wa kweli hata kama utakuumiza. Wawe tayari kujiambia ni wapi unapokosea au wapi una udhaifu. Watu hawa wanaweza kuwa walimu,makocha, washauri au mamenta.
    4. Msingi wa nne ni kuendelea kujisukuma kutoka nje ya mazoea yako. Kama unafanya kitu na hukutani na magumu au changamoto, basi jua unafanya kwa mazoea na hutaweza kubobea. Unapaswa kuyatafuta magumu na changamoto kwa kutoka nje ya mazoea yako.

    Hata kama tayari unapata matokeo mazuri, usibaki kwenye ulichozoea, jaribu vitu vipya, jaribu ambavyo hujazoea.

    Utatengeneza magumu na changamoto ambazo zitakusukuma zaidi, zitakufanya ujifunze zaidi, ufanye kwa ubora zaidi, upate mrejesho wa kukujenga zaidi na uweze kubobea na kufanikiwa zaidi.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@kemeimaureen.

    Jiunge na mtandao huu.

    Jaza fomu hii kujiunga na mtandao huu Ili upokee mafunzo zaidi kwenye email yako. Asante.

  • Umuhimu wa kuwa na udhibiti.

    Rafiki wangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini tafiti mbalimbali zimekuwa zinaonesha watu wanakuwa na ufanisi mkubwa kwenye kazi wanazofanya, pale wanapokuwa na udhibiti kwenye kazi.

    Watu wanapokuwa na udhibiti wa kuamua nini wafanya na wakifanye kwa namna gani, wanapoamua watumieje muda wao, wanakuwa na ufanisi mzuri.

    Hivyo hatua muhimu unayopaswa kuchukua Ili kujenga kazi ya ndoto yako, kazi utakayoifurahia na kuipenda ni kuhakikisha unakuwa na udhibiti mkubwa kwenye kazi unayofanya.

    Unapaswa kuchagua nini unachotaka kufanya, unakifanya kwa namna gani, na watu gani na kwa wakati gani.

    Ukiwa vizuri kwenye kile unachofanya na ukawa na udhibiti mkubwa kwenye kukifanya unapata ridhiko kubwa na kupenda kile unachofanya.

    Tumia ujuzi mtaji ulionao kuhakikisha unakuwa na udhibiti mkubwa kwenye kile unachofanya. Kwani hata ukiwa bora kiasi gani kwenye unachofanya, kama wengine ndiyo wanakudhibiti, hutakuwa huru kwenye kufanya.

    Udhibiti ni mzuri na muhimu, lakini kuna vikwazo vinavyowazuia wengi kupata udhibiti.

    Akupendaye sana.

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Faida za kufikiri chanya.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kufikiri chanya kuna manufaa makubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.

    Kwanza kabisa kunafanya afya ya mtu kuwa imara. Tafiti zinaonesha wanaofikiri chanya wana hatari ndogo ya kupata magonjwa ya moyo ukilinganisha na wanaofikiri hasi.

    Pili wanaofikiri chanya wanaona fursa nyingi za uwezekano kuliko wanaofikiri hasi. Unapofikiri chanya ni kama unakuwa umeifungua akili yako iweze kuona mengi yalivyo kwenye uhalisia.

    Mara zote fikiria chanya na amini unaweza na inawezekana, hilo litafungua fursa nyingi zaidi kwako.

    Kuchukua hatua rafiki yangu unao ushahidi wa kutosha, kwako mwenyewe na kwa wengine pia ambao wanaweza kufanya makubwa. Tumia ushahidi huo kujenga imani isiyo na ukomo.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Umuhimu wa kubadili mtazamo wako.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kuna hadithi maarufu kutoka katika kitabu cha Acres of diamonds cha Russell H. Conwell, kinachomhusu mkulima aliyeuza shamba lake baada ya mtu mwenye hekima kumwambia kuwa akiwa na kipande kidogo cha almasi kama kidole gumba chake anaweza kuwa tajiri mkubwa na mwenye nguvu, pia akiwa na kipande cha almasi kama tofali anaweza akamiliki nchi yote.

    Mkulima yule ajulikanaye kwa jina la Faitz, usiku ule hakulala kabisa na alikuwa hana furaha kabisa usiku kucha. Kesho lake alifanya mambo ya kuuza shamba lake, aliamua kuuza shamba lake lote na kwenda kutafuta almasi.

    Alizunguka Africa yote lakini hakuweza kuiona, akazunguka Ulaya nzima lakini hakuiona, hatimaye alipofika Uhispania akiwa amechoka na hela zimemwishia, aliamua kujiua kwa kujitosa kwenye Mto Barcelona.

    Huku nyuma aliyenunua shamba la mkulima, siku moja alikuwa ananywesha maji ngamia katika kijito cha maji kilichokatiza katika shamba lile. Miale ya jua iliangazia jiwe lililokuwa karibu na kijito kile, na lilitoa rangi ya kumetameta kama rangi ya upinde wa mvua. Yule jamaa mwenye shamba alilichukua lile jiwe na kuliweka ndani yake.

    Yule mwenye hekima alipokuja na kuliona lile jiwe aliuliza swali Faitz amekuja? Faitz ndilo lilikuwa jina la yule mtu aliyeuza shamba. “Hapana,” yule aliyekuwa amelinunua shamba alijibu na akamuuliza ” Kwa nini anauliza hivyo?” “Kwa sababu ile ni almasi.”

    Yule mmiliki mpya wa shamba alisema ” Hapana, ni jiwe tu ambalo nimeliokota kwenye kijito na yapo mengi tu.” Walienda kuokota na kwenda kuyafanyia uchunguzi na kweli walikuta yale mawe ni almasi. Katika shamba lile kulikuwa na heka za almasi.

    Mambo muhimu ya kujifunza kutokana na hadithi hii, kutoka katika kitabu cha Acres of diamonds cha Russell H. Conwell.

    Kwanza kama mtazamo yetu iko sahihi au ni chanya tunapaswa kugundua kuwa wote tunatembea kwenye heka za almasi. Hakuna aliye masikini bali ni kutojua siri hii. Kwani kila mtu anao uwezo ndani yake wa kumwezesha kutimiza kusudi lake la kuwa hapa dunia.

    Kuchukua hatua, rafiki yangu uwezo wa kutimiza ndoto yako upo mikononi mwako. Unaweza kufikia malengo na kutimiza ndoto yako kama ukitambua kuwa unao uwezo katika ncha za vidole vyako.

    Hii inahitaji uwe na mtazamo chanya. Fursa mara nyingi huwa ziko chini ya miguu yetu. Wala haihitaji kwenda mbali, kinachohitajika ni kutambua tu hizo fursa.

    Dkt. Eli VD Waminiani aliwahi kusema, ” Watu wengi ni masikini kwa sababu wanahangaika kutafuta utajiri mbali na mahali walipo, lakini kumbe utajiri wanaona mikononi mwako” Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu wanahangaika kutafuta vitu ambavyo tayari wanavyo.

    Ukitafuta kitu ambacho unacho hutakipata, bali unatakiwa kukitambua na kukitumia ili kukinufaishe.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Umuhimi wa kubadili mtazamo wako.

    Rafiki yangu mpendwa, mara nyingi mtazamo wako ndiyo unaokutofautisha na wengine. Nini mtazamo wako juu ya maisha, mafanikio na uwezo.

    Kuna aliyefanya utafiti kidogo tu juu ya mtazamo ya watu. Aliweka maji kwenye glasi. Kuna aliyeona glasi imejaa nusu, kuna aliyeona nusu haijajaa au haikujaa nusu. Watu hao wawili wana mtazamo tofauti.

    Mtazamo wako juu ya uwezo wako utakutofautisha na wengine. Kitu cha kushangaza ni kuwa mtazamo wako unatafsiri utendaji wako. Hivyo, unaweza kuathiri vitendo vyako chanya au hasi kulingana na mtazamo wako.

    Kama mtazamo wako ni kuangalia udhaifu wako juu ya uwezo wako, ni lazima utakupeleka kushindwa kwa kila kitu unachokifanya.

    Kuna mtazamo chanya na hasi. Unahitaji mtazamo chanya Ili uweze kusonga mbele. Kwa mfano ukimsikia mtu akisema ‘ hawezi’ kuna mawili;

    1. Yaweza kuwa anamaanisha hajui. Hivyo, anahitaji kufundishwa Ili ajue kuwa anaweza na inawezekana kufanya na kuwa chochote anachotaka.
    2. Anahitaji kufundishwa lakini uwezo wa kufanya jambo lolote uko ndani mwake na wala hauko mbali.

    Kuchukua hatua rafiki yangu ni wakati sahihi wa kubadili mtazamo wetu, kama tunataka tuwe wa tofauti au kuondokana na kundi kubwa la wengi wanaoishi maisha ya kawaida, wakifanya mambo ya kawaida tu. Hatuna budi kuibadili mtazamo wetu yaani tuwe watu wenye mtazamo wa uwezekano,uchanya na ufaulu.

    Mtazamo ni muono wa ndani yaani ni tofauti na kuona kwa macho. Macho yako yanaweza yakakusaidia kutengeneza mtazamo wako wa ndani, mtazamo chanya au mtazamo hasi.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Njia 10 za kumfanya mtu ajiskie wa muhimu.

    Rafiki yangu mpendwa kila binadamu anahitaji kujiskia ni wa muhimu na kuheshimiwa na wengine, kila mtu anatakiwa kupendwa na anataka ajiskie ni wa muhimu.

    Hatua ya kwanza ya kumfanya mtu ajiskie ni wa muhimu ni kuwa kama una tatizo ambalo mtu mwingine anaweza kukusaidia kulitatua, basi mwambie hivi, ” Wewe ni mtu muhimu katika swala hivi nitashukuru kama utanisaidia .” Mguse mgongoni. Mwambie akusaidie. Mfanye ajiskie ni wa muhimu.

    Njia ya pili kila mara wasalimu watu kwa tabasamu bayana. Watu huwa wanaguswa na mtazamo uliopo nyuma ya salamu. Wasalimu kwa shauku kubwa kuwa umefurahi kuwaona.

    Njia ya tatu ni kwenye kukumbuka majina ya watu. Tambua majina kiusahihi kabisa, na usisahau cheo cha mtu kukitaja kama ni Bw,Bi,Dkt,Mh,Prof, na kadhalika. Cheo kinamfanya mtu ajiskie ni wa muhimu. Hivyo vitumie.

    Njia ya nne ukiwa kwenye mazungumzo na wengine, usiwakatishe, kumbuka mzungumzaji mzuri ni maarufu zaidi. Zungumza kama unacho cha kuzungumza, lakini sikiliza na onesha kuvutiwa na wengine wanachokizungumza.

    Tano, kila mara kuwa tayari kumsaidia mwingine, iwe ni ushauri au kwa neno sahihi, katika uelekeo sahihi na kwa wakati sahihi. Ukimsaidia yeyote katika ngazi ya mafanikio yake, yeye pia atakuwa katika nafasi ya kukusaidia siku za nyuma.

    Sita, onesha kutambua mchango na juhudi za mtu mwingine kwako kwa kumshukuru moja kwa moja, au kumtumia ujumbe wa shukrani. Ukarimu kidogo tu huleta faida kubwa.

    Sapa, katika kutambua vipaji vya wengine, kuwa mvumilivu kwa vile visivyofikia kiwango chako. Hakuna mtu aliyekamilika.

    Nane, ukiwa katika kusanyiko epuka kuwaseng’enya wengine, au kufanya uwezo wa mtu mwingine kuwa hasi. Kama huwezi kusema kitu kizuri kuhusu mtu yeyote yule usiseme chochote.

    Tisa, jizoeshe kila siku kutambua mchango wa mtu . Waoneshe watu wengine kwamba unawapenda. Usisubiri mtu afe ndipo utambue mchango wake katika maisha yako.

    Kumi, kamwe usipinge bila kusifia, au kutambua mchango wa mtu. Hakuna mtu anayependa kuambiwa hafai katika kazi yake. Pinga kwa kujenga, na si kwa kubomoa, halafu sifia angalau hata mchango mmoja wa huyo mtu.

    Kuchukua hatua rafiki yangu, hayo ndiyo mambo kumi ya kuyafanya watu wawe tayari kukusaidia na kusaidiana nao.

    Jijengee tabia hii muhimu ya kuwashukuru watu, na kusema asante kwa kila jambo au mtu unayekutana naye. Naye atakuwa tayari kukusaidia au kushirikiana na wewe.

    Kumbuka, kila mtu anamtegemea mwenzake Ili aweze kutimiza ndoto zake na kuwa anayemtaka bila kuwa na kikwazo chochote.

    Akupendaye sana,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com