Home

  • Jinsi Ya Kuvunja Imani Zenye Ukomo.

    Rafiki yangu mpendwa ili uweze kuwa huru kufikiri na kufanya makubwa, lazima kwanza uvunje imani zote zenye ukomo ulizonazo.

    Hapa kuna hatua tatu za kuvunja imani hizo;

    Hatua ya kwanza ni kutambua imani za ukomo ulizonazo. Jisikilize sauti zinazotoka ndani yako, kwenye kila unachojiambia huwezi au haiwezekani, jua hapo una ukomo wa imani. Hata kama ni jambo ndogo kiasi gani, kama unajiambia huwezi au haiwezekani, jua hapo una ukomo wa imani.

    Hatua ya pili ni kuangalia ukweli . Mengi unayojiambia huwezi au haiwezekani siyo kweli, ni mazoea tu umekuwa nayo.

    Chukua hatua ya kuangalia ukweli kwenye kila eneo uliyojiwekea ukomo. Utagundua kuna wakati uliweza kufanya yale unayojiambia huwezi.

    Hata kama ulifanya na ukashindwa matokeo hayakuwa mabaya kama ulivyotegemea yawe kwa kuona ukweli huo, utazidi kuona jinsi imani uliyokuwa nayo siyo sahihi.

    Hatua ya tatu ni kutengeneza Imani mpya isiyo na ukomo kwenye maeneo yote ambayo umejiwekea ukomo. Kila unachojiambia huwezi au haiwezekani, jiambie unaweza na inawezekana.

    Kwa kubadili imani yako kwenye maeneo uliyokuwa na ukomo, unaacha kuona ukomo na kuanza kuziona fursa mbalimbali za uwezekano.

    Chukua hatua sasa rafiki anza kubadili imani uliyonayo za ukomo na kuanza kuziona fursa mbalimbali za uwezekano kwenye maeneo haya.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Sababu 5 Za Kujua Kwa Nini Kubwa Za Mbona Wewe Uteseke??

    Rafiki yangu mpendwa unajiuliza sasa hivi kuteseka huku kunamaanisha nini haswa?

    Kuteseka huku ni kuvumilia changamoto unazopitia wakati unapambana, wakati unajituma ili kufikia ndoto zako kubwa kwenye maisha.

    Kwa hivyo basi, unapaswa kujua kwa nini uteseke, unateseka ili uweze kupata njia ya kutokea na kuboresha mwanzo wako.

    Kama hauna kwa nini kubwa inayokusukuma kila siku ili ufikie ndoto zako kubwa utakatishwa tamaa sana na utapotea.

    Yafuatayo ni mambo 5 ya kukusaidia kujua kwa nini kubwa tuteseke kwenye maisha ya mafanikio.

    1. Kujua kusudi la maisha yako. Nateseka kwa sababu kazi au biashara ninayofanya ni sababu kubwa ya kwa nini nipo humu duniani.
    2. Kupata furaha na uhuru kamili wa kifedha. Nateseka nikitafuta fedha ili niwe na maisha ya furaha na uhuru wa kutembea popote ninapotaka kwenda humu duniani na pia kuweza kununua kile ninachotaka kwenye maisha bila kuzuiwa na ukosefu wa fedha.
    3. Kuweza kuwasaidia wengine. Nikipata fedha naweza saidia wenye uhitaji mbalimbali bila kuona ugumu wowote. Kama kumiliki biashara inayoweza kuajiri wengine, kumiliki kiwanda ili kuajiri wafanyakazi na hivyo waweze kupata hela za kuendesha maisha yao.
    4. Kuacha jina nzuri au legacy. Ninapojituma kufikia ndoto zangu kubwa kama kumiliki kiwanda au kumiliki biashara inayojiendesha enyewe bila ulazima wa uwepo wangu. Hapo nitakuwa nimeacha jina nzuri kwa vizazi vilivyo hai na vijavyo.
    5. Kuwaonyesha wengine kuwa inawezekana na waweze pia kufanya. Ninateseka kwenye kutafuta hela, kufanya biashara na kuvumilia changamoto mbalimbali bila kukata tamaa. Ninapofanya hivyo wadogo wangu wanaona na wanajifunza pia kwamba ili kupata mambo mazuri kwenye maisha tunapaswa kujituma bila kukata tamaa.

    Chukua hatua; Rafiki tunapaswa tujue kwa nini kubwa kwenye maisha yetu, ili tunapoteseka kutafuta hela, tunajua nini haswa tunataka kwa kufanya hivyo tutakuwa waangalifu sana na kutumia hela vizuri bila kufuata mkumbo na kwa kufanya hivyo tutaweza kuishi maisha yenye furaha na uhuru mkubwa.

    Rafikj yako,

    Maureen Kemei.

  • Mambo 5 Muhimu Ya Kuzingatia Kwenye Maisha Yako.

    Rafiki yangu mpendwa kwenye kitabu cha 12 rules of life mwandishi Jordan Peterson anatushirikisha mambo muhimu ya kuzingatia katika maisha yetu.

    Na baadhi ya mambo ambayo mwandishi anatushirikisha ni kama ifuatavyo;

    1. Sema ukweli. Nafikiri hili hakuna haja ya maelezo marefu, sema ukweli mara zote, usidanganye hata kama ni kitu kidogo kiasi gani, sema kweli na kweli itakuweka huru. Kweli ni rahisi kukumbuka na ukweli itakuweka sehemu salama mara zote.
    2. Usifanye kitu unachokichukia. Fanya unachokipenda, penda unachofanya, huu ndiyo msingi wa maisha bora na ya mafanikio. Kama kuna kitu hutaki au hupendi kufanya usifanye, muda wako ni mchache na wa thamani, usiupoteze kwa yasiyo muhimu.
    3. Fanya kwa namna ambavyo utaweza kueleza ukweli wa ulichofanya. Fanya kitu ambacho unaweza kukielezea kwa wengine kama huwezi kukielezea kwa wengine usifanye.
    4. Fanya kile ambacho ni muhimu kwako, na siyo ambacho ni rahisi. Kila mtu anataka kukata kona, kila mtu anatafuta njia ya mkato ya mafanikio, kila mtu anatafuta njia ya kupata fedha bila ya kufanya kazi. Fanya kilicho muhimu kwako na siyo kutafuta kilicho rahisi. Kwa sababu mwisho wa siku maisha siyo fedha tu, unaweza kuzipata na bado ukaona maisha hayafai.
    5. Kama unahitaji kuchagua, kuwa mtu anayefanya mambo, na siyo mtu anayeonekana kufanya mambo. Kila mtu anapenda kuonekana ni mfanyaji, lakini wengi ni wasemaji na walalamikaji, kuwa mfanyaji, acha wengine wawe watu wa maigizo, wewe fanya.

    Hatua ya kuchukua leo; nenda kuyaishi mambo haya kwa vitendo na utakuja kunishukuru baadaye.

    Sema ukweli, usifanye kitu unachokichukia. Fanya kwa namna ambavyo utaweza kueleza ukweli ambacho ni muhimu kwako kufanya. Kuwa mtu anayefanya mambo.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Mambo Ya Kuzingatia Wakati Wa Kuandaa Bajeti.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kuweka bajeti inakusaidia kufanikisha mambo mengi ya kifedha kama; kuweka malengo, kujenga nidhamu yako ya kifedha, inakusaidia kuepuka madeni ya kiholela holela, unakuwa na picha kamili ya kile ambacho kitatumika na na kuona halisi ya kifedha.

    Hapa kuna mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kuandaa bajeti.

    1. Lazima uangalie kipato chako halisi.
    2. Utajua kipato chako ni kiasi gani.
    3. Kutambua matumizi ya dharura ni vigumu mwezi uishe bila dharura.
    4. Andika bajeti yako sasa. Andika kwenye simu yako, note book yako, group private kwenye simu yako.
    5. Kuanza kufuatilia mwenendo wa bajeti yako, kila siku kila wiki.
    6. Kukitokea mabadiliko yanatokeza uzingatie pia. Mfano mapato yakiongezeka matumizi yasiongezeke.
    7. Kuwekeza . Mpango wa uwekezaji uwepo
    8. Kuepuka matumizi ya hadharani. Kushindana na watu wengine kwa mfano kununua magari, kufanya biashara, n.k.
    9. Jifunze kutoka kwa wengine. Soma mambo mbalimbali ili uweze ujifunza kutoka kwa wengine.
    10. Kagua bajeti yako mara kwa mara.

    Chukua hatua; rafiki ukiwa una bajeti inakukubusha kuwa ili halikuwa kwenye bajeti yangu. Lakini bila bajeti pia fedha hazionekani, hivyo ni muhimu kuwa na bajeti.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Utatokaje Kwenye Tabia Hii Ya Kutokusamehe.

    Rafiki yangu mpendwa maandiko yanasema hivi kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe nyinyi.

    Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe nyinyi makosa yenu.

    Utatoka kwenye tabia hii ya kutokusamehe kwa kufanya yafuatayo;

    1. Kujifunza kusamehe na kuachilia siku zote za maisha yako hapa duniani.
    2. Kama mtu amekukosea jambo kubwa muite kaa naye chini ongea naye kwa upendo bila kupayuka payuka kama mtu asiye na akili, mwambie mahali ambayo amekukosea, mtangazie msamaha hapo hapo na endelea kumpenda na kumtakia mema siku zote.
    3. Baada ya kusamehe mtu usiizungumzie tena hilo jambo, endelea na maisha yako na malengo juu ya ndoto yako.
    4. Tafuta kuwa na Amani ndani ya moyo wako, jifunze mambo mazuri juu ya ndoto yako.
    5. Jiepushe na marafiki wagomvi na wenye kupenda mapambano ya maneno.
    6. Siku zote kuwa mtu wa kulingana na imani yako.

    Chukua hatua; rafiki katika kusamehe utaishi maisha yenye amani na furaha na itakusaidia kufika kwenye ndoto yako.

    Kitu kimoja zaidi kusamehe ni mlango wa kufika kwenye ndoto yako.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Utajuaje Una Tabia Ya Kutokusamehe.

    Rafiki yangu mpendwa Kutokusamehe ni mlango ambao unafunga mafanikio, baraka na ndoto yako hapa duniani.

    Aliyewahi kuwa Raisi wa Afrika Kusini Nelson Mandela aliwahi kupitia kipindi kigumu sana kabla ya kuwa Rais ya Nchi hiyo. Moja ya vipindi vigumu alivyopitia ni kufungwa jela kwa miaka 27.

    Na kipindi yupo gerezani wale askari walikuwa wakimfanya dhihaka sana kwa kutumbukiza kwenye shimo na kumkojolea na kumwambia meneno mabaya ya kwamba hataweza kuja kuongoza Nchi ya Afrika Kusini.

    Lakini wakati anakojolewa Nelson Mandela alimwambia yule askari ya kwamba siku moja nitaiongoza Nchi yangu. Na baada ya kutoka gerezani aliwasamehe wote waliomfanyia mabaya yale, na mwishowe alikuja kuiongoza Nchi kwa ushindi mkubwa.

    Watu wanaweza kukukosea mambo makubwa sana na ukajisemea moyoni kwamba hutawasamehe, ukweli ni kwamba wewe ndiye utakayejiumiza na kujirudisha nyuma sana, utabeba uchungu, visasi na mwishowe ikakupelekea kutokuwaza wala kufikiria juu ya hatima ya maisha yako

    Yule aliyekukosea anaweza asigundue amekukosea sana, na anaweza asikuombe hata msamaha na akaamua kukaa kimya, kwa wakati huo unatakiwa uchukue hatua ya kumsamehe na kuendelea na mambo mengine na siyo kushikilia kama ni kanuni ya mafanikio.

    Utajuaje Una Tabia Ya Kutokusamehe.

    1. Muda wote unazunguka ubaya wa nyuma ambayo ulishawahi kufanyiwa na marafiki, mchumba, wazazi, ndugu, wafanyakazi wenzio na bosi wako hiyo ni dalili ya kwamba hukusamehe bado unatembea na mabaya hayo.
    2. Huamini kama kuna watu wema na wenye kutenda wema.
    3. Kutoshirikiana au kumsaidia yule aliyekukosea hata kama ameshaomba msamaha.
    4. Kukumbushia yale mabaya ya mwenzio kila wakati hata kama alishakuomba msamaha, na hii huwa inatokea sana kwa wapenzi, wachumba na Wana ndoa.
    5. Kupanga mabaya na visasi juu ya aliyekukosea.

    Chukua hatua; tujifunze kusamehe na kuachilia siku zote za maisha yetu hapa duniani.

    Rafiki Yako,

    Maureen Kemei.

  • Misingi 11 Ya Charles T Munger.

    Rafiki yangu mpendwa karibu sana tujifunze misingi haya ambayo Charles T Munger aliyaishi kwenye maisha yake, ili tuweze kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa

    Mafunzo haya yanatokana na mfumo wa maisha ya Charles ambao unaendeshwa na misingi ifuatayo;

    1. Kujifunza maisha yote
    2. Udadisi
    3. Uzani
    4. Kuepuka wivu na chuki
    5. Kuwa mtu unayeweza kutegemewa.
    6. Kujifunza kutokana na maisha ya wengine .
    7. Uvumilivu na ung’ang’anizi.
    8. Kufikiri kwa akili yako.
    9. Kuwa tayari kujaribu imani yako mwenyewe.
    10. Kugeuza kitu ili kukielewa vizuri.
    11. Kutumia mfumo wa akili wa kufanya maamuzi unaohusisha taaluma mbalimbali.

    Charlie alikuwa anatumia hadithi na vichekesho ili kufikisha ujumbe wake, kitu ambacho kinawafanya watu wamwelewe vizuri.

    Lengo kuu la Charles kwenye yake ni uhuru, hivyo alitumia utajiri kama kitu cha kumpa uhuru na siyo kinyume chake.Amewahi kunukuliwa akisema; ” niliamua kuwa tajiri ili niweze kuwa huru kama Lord Maynard Keynes.

    Chukua hatua; rafiki yangu tunapaswa kuwa na misingi yetu binafsi ambayo yatatutuongoza kwenye maisha yetu ya kila siku na kuuishi misingi haya kama vile Charles aliyaishi na aliweza kufikia utajiri mkubwa.

    Rafiki Yako,

    Maureen Kemei.

  • Jinsi Ya Kujua Una Tabia Ya Hasira.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini tabia ya hasira imepelekea watu wengi kutokufikia kwenye ndoto zao, na wengine wanaichukulia kama sehemu yao ya kujihami endapo changamoto zitatokea kama ugomvi.

    Watu wengi wenye hasira mara zote siyo watu wanaotumia akili zao kufikiria juu ya changamoto iliyojitokeza mara nyingi wanatumia hisia zao ambazo ni hasira kutatua changamoto zao kwa maana nyingine ni wagomvi sana.

    Moja ya misemo maarufu sana duniani inasema hivi; watu dhaifu hulipiza kisasi, watu imara husamehe, watu wenye akili hupuuzia.

    Hasira zimesababisha watu wengi sana biashara zao kufikisika, mahusiano na watu muhimu kuvunjika, ndoa kuvunjika, watu kufukuzwa kazi na hayo yote yanatokana na kitu kinachoitwa hasira.

    Utajuaje umetawaliwa na tabia hii ya hasira?

    1. Unapaniki na kukasirika sana kwenye jambo dogo. Jambo dogo tu umeshakasirika na hali ya hewa imeshabadilika ndani ya muda mfupi.
    2. Hulipi jambo muda baada ya kutokea.
    3. Kufanya maamuzi papo kwa papo bila kutaka ushauri wa mtu.

    Tabia ya hasira ina uwezo wa kukutoa kabisa kwenye malengo yako na ikakupeleka ukashindwa kabisa kufika kwenye ndoto yako na mwisho wa siku utawaona watu ni wabaya, utabaki na uchungu na visasi ndani ya moyo wako.

    Kuondokana na tabia hii, jenga tabia ya kutokutawaliwa na hisia ya hasira, ugomvi unapotokea jizuie usionyeshe hasira zako mbele ya watu ili uonekane una kifua sana , jifunze kujishusha, kuwa na muda wa kupata majibu ya tatizo lililojitokeza.

    Hatua ya kuchua; fanya mambo yanayokufurahisha zaidi, zungukwa na watu wenye mtazamo chanya, soma sana maandiko matakatifu, pamoja na vitabu vingine, kuwa na muda mzuri na Mungu ( quality time with God).

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Umuhimu Wa Kuishi Wito Wako.

    Rafiki yangu mpendwa kila mtu ana wito fulani ndani yake, asili inayomvuta kufanya zaidi vitu vya aina fulani.

    Mtu anapofanya kitu cha wito wake, anafurahia, anajituma na anakuwa na hamasa na hachoki katika kufanya.

    Wale wanaofanikiwa sana ni wale wanaojua wito wa maisha yao na kuuishi kwa viwango vya juu sana.

    Kujua wito wako, anza kwa kuangalia vitu ambayo ulikuwa unapenda kufanya na kufuatilia tangu ukiwa mdogo.

    Kisha ingia kuvifanya kama kazi au biashara inayokulipa, huku ukiendelea kujifunza kuhusu unachofanya na kuhusu wewe mwenyewe na kuendelea kujiboresha zaidi.

    Kwa kwenda hivyo, utajikuta umetengeneza kazi au biashara ya kipekee kwako, inayowanufaisha watu na inayokulipa sana.

    Uzuri wa kuishi wito wako ni hakuna anayeweza kushindana na wewe akakushinda, maana hapo unakuwa unaishi maisha na siyo kuigiza.

    Chukua hatua; rafiki tunapaswa kuishi na wito wetu ili tufanye makubwa.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Jinsi Ya Kutofautisha Yaliyo Ndani Na Nje ya Uwezo Wetu Na Mstoa Epictetus.

    Rafiki yangu mpendwa mwanafalsafa Epictetus aliweza kujifunza falsafa akiwa mtumwa, kwenye utumwa huo haukumwacha salama bali alipata kilema.

    Akiwa kilema aliweza kuishi maisha yake kama mstoa, aliweza kuandikia wanafunzi wake falsafa ya kuweza kuishi maisha kwa utulivu mkubwa bila kuyumbishwa na mambo mengine.

    Baadhi ya mambo yapo ndani ya uwezo wetu na mengine yapo nje ya uwezo wetu. Chochote ambacho tunakifanya sisi kipo ndani ya uwezo wetu, miili yetu iko nje ya uwezo wetu. Sifa, watu na chochote ambacho hatukifanyi vipo nje ya uwezo wetu.

    Changamoto kwenye maisha ni pale unapohangaika na mambo yaliyo nje ya uwezo wetu yanakufanya uwalaumu watu wengine.

    Kama utafikiria yale tu yaliyo ndani ya uwezo wako hakuna mtu atakayekusumbua, atakayekulaumu, atakayekushtumu, au hata kudhurika kwa namna yoyote ile. Kwa sababu umeamua kuhangaika na yale yanayohusika na wewe.

    Usihangaike na yaliyo nje ya uwezo wako kabisa, tunapojihusisha na mambo yaliyo nje ya uwezo wetu ni kama hatuna au hatumiliki chochote kabisa.

    Usiruhusu kilicho nje ya uwezo wako kivuruge maisha yako, labda ni tabia ya mtu mwingine, usihangaike kutaka kubadilisha tabia za watu.

    Yaliyo ndani ya uwezo wetu ni maoni tuliyonayo, hatupaswi kuwa na maoni juu ya kila kitu. Hisia zetu pia tunapaswa kudhibiti hisia zetu, chochote ambacho tunaweza kukifanya kipo ndani ya uwezo wetu na tunaweza kudhibiti.

    Watu wengi wanaopata msongo wa mawazo ni wale wanashindwa kuelewa kuwa vitu vingi wanazozimiliki tumepewa kwa muda na tukizipoteza hatupaswi kuwa na msongo juu ya hayo mambo.

    Tunapaswa kuishi kwa msingi wa falsafa, kuishi maisha yetu wenyewe, kuwa na furaha wakati wote bila kukuhusu mambo ya nje yatusumbue.

    Mduara wa uwezo , mara nyingi sana watu wanasumbuka kwenye mambo yaliyo nje ya uwezo wetu, kufikiri kuwa wanaweza kuadhiri mambo yaliyo nje ya uwezo wetu. Kama tabia za watu, maono yao, mtazamo yao, yote yapo nje ya uwezo wetu.

    Njia nzuri ya kuadhiri yaliyo nje ya uwezo wako ni kufanya vizuri kabisa yale yaliyo ndani ya uwezo wetu, kama kuishi maisha yako kwa namna bora zaidi, kwenye kutunza muda, kuwa na kiasi kwenye mambo mengine kwenye maisha.

    Kwa kufanya hivyo utaweza kuadhiri maisha ya wengine na wao kutaka kufanya mambo na wewe au wakimbie, wasitake wao wenyewe wanaona hawataendana na jinsi unavyofanya mambo.

    Chukua hatua; rafiki hatupaswi kuumizwa sana au kuyumbishwa na maoni ya watu wengine juu jinsi tunavyoishi maisha yetu. Tunapaswa kuishi maisha yetu kwa uhalisia na kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wetu.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.