Home

  • 14/100.lazima kuchukua hatari.

    Habari
    Karibu sana tuendelee na kujifunza kwetu kuhusu safari ya kupata hazina ya maisha. Tukiongozwa na kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Ilionekana vita inachukua muda mrefu na hivyo msafara hauwezi Kuendelea. Alchemist alimwendea Santiago na kumwambia inabidi aendelee na safari yake licha ya kuwepo kwa hatari ya vita.
    Alimwambia auze ngamia aliyenaye na kununua farasi kwa sababu ndiyo wazuri kwenye safari.

    Santiago na the alchemist walianza safari ya kuelekea kwenye mapiramidi. Moyo wa Santiago haukuwa tayari Kuendelea na safari, alikuwa mzito na alikuwa ameanza kukata tamaa.

    Alchemist alimwambia hiyo ni kawaida pale mtu anapokuwa anakaribia ushindi, ndivyo mambo yanakuwa mazito na yanaonekana kama hayawezekani.

    Santiago aliamua kutokupingana na moyo wake na kuusikiliza, aliamua kuangalia kila anachohofia na hilo lilimfanya aanze kujiamini na kuamini ile ni safari ya ndoto yake.

    Kwenye maisha safari ya ndoto yako, mambo yatakuwa magumu lakini hayapaswi kukukwamisha, utaona kila kitu hakiwezekani lakini utapaswa kwenda zaidi. Usikilize moyo wako lakini usikubali kukata tamaa.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha.Anayejifunza kazi ya uandishi kupitia kwa waandishi wengine.

    Maureen Kemei
    Blog kufikirichanya.wordpress.com

  • 13/100. Vyeo visikufanye usahau ndoto yako.

    Karibu rafiki.
    Tunaendelea kujifunza namna ya kupata hazina ya maisha, kutoka kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Baada ya Santiago kuweza kutahadharisha kuhusu shambulio na hivyo kuwa ameokoa eneo zima, viongozi wa eneo lile walimpa nafasi kubwa ya uongozi,walimwambia kama atakubali kukaa pale watampa cheo kikubwa. Hili lilimfanya kuona hana tena haja ya kuhangaika, ameshapata mwanamke anayempenda na pia amepewa cheo kikubwa.

    Lakini yule mtu wa kubadili madini ya kawaida kuwa dhahabu’alchemist’alimsihi asiaje safari ya ndoto yake. Alimwambia cheo ni kitu cha muda tu na hakidumu milele, lakini kufikia hazina yake ni kitu kitakachodumu milele kwenye maisha yake. Hata mchumba wake Fatma hakukubaliana naye kuacha safari yake.

    Kuna zawadi nyingi sana utakazokutana nazo kwenye safari ya kuelekea kwenye ndoto yako, ambazo zitakushawishi usiendelee na safari hiyo. Hakikisha hufiki kwenye hali hii, usisahau safari ya ndoto yako, hata kama umepata cheo kikubwa kiasi gani.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha, Mwandishi anyejifunza kutoka kwa waandishi wengine katika eneo la mafanikio, ushauri nasaha, ujasiriamali na maendeleo binafsi ya elimu ya kifikra.

    Maureen Kemei
    kemeimaureen32@gmail.com

    is

  • 13/100. Dunia Ina lugha yake ya kukuambia vitu.

    Habari rafiki.

    Karibu tuendelee kujifunza namna ya kupata hazina ya maisha , kutoka Kwa kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Nishukuru Mungu kwa zawadi ya uhai ambayo ametujalia siku ya leo. Siku moja Santiago alikuwa peke yke jioni akitafakari safari yake, aliona mwewe wawili wakipigana na kuumizana.

    Hapa alikuwa amejifunza lugha ya dunia na alielewa kile ni kiashiria cha hatari. Aliona kwamba lile eneo walilopo linakwenda kushambuliwa na moja ya makundi yanayopigana kwenye vita.

    Alifikisha taarifa hizi kwenye uongozi wa eneo lile ambao walifanya na walipokuja kushambuliwa waliweza kuwashinda na hivyo kuokoa eneo lile.

    Wakati unaendelea na safari ya kuelekea kwenye ndoto yako, dunia itakuwa inakupa viashiria mbalimbali. Unapaswa kuijua kuisoma na kuielewa lugha ya dunia ili kuweza kuelewa viashiria hivyo na kuvifanyia kazi kwa manufaa yako na ya wengine.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha.Pia ni mwandishi ambaye anajifunza kupitia kwa waandishi wengine katika eneo la mafanikio,ushauri nasaha, ujasiriamali na maendeleo binafsi ya elimu ya kifikra.

    Maureen Kemei

    Kemeimaureen32@gmail.com

    0713698650

  • 12/100.Tumia changamoto kwa manufaa.

    Habari.

    Namshukuru Mungu ametuwezesha kuona siku nyingine tena, hivyo utukufu ni wake siku zote.

    Karibu sana tusonge mbele katika kujifunza namna ya kupata hazina ya maisha. Tukiongozwa na kitabu kizuri cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Safari ya kuelekea kwenye mapiramidi ilikwama kutokana na vita, hivyo walikaa kwenye eneo lile kwa muda. Badala ya kuona ni mwisho wa safari, Santiago aliamua kutumia changamoto hiyo kwa manufaa. Kwa kushirikiana na yule mwingereza waliyekutana naye kwenye msafara, waliamua kumtafuta mtu mwenye utalaamu wa kegeuza madini ya kawaida kuwa dhahabu.

    Waliulizia kwa watu mbalimbali na hatimaye wakampata, mtu yule alimpa yule mwingereza zoezi la kufanya kwanza akishalikamilisha ndiyo arudi kwake. Lakini kwa Santiago, aliona kitu cha tofauti na alimwambia kwamba ana kitu cha tofauti ndani yake. Santiago alimweleza lengo la safari lake na mtu yule alimwambia ni safari sahihi kwake kufikia ndoto yake.

    Lakini pia wakiwa wamekwama kwenye eneo hilo, Santiago alikutana na binti mzuri ambaye alimpenda sana binti huyo aliitwa Fatma. Binti naye alimpenda pia na walikuwa wakionana mara moja kila siku. Santiago aliahidi kwamba angemuoa binti huyo baada ya kukamilisha safari yake, na binti alikubali, akimsisitiza lazima akamilishe safari ya kufikia ndoto yake.

    Kwenye safari ya kuelekea kwenye ndoto yako, Kuna wakati utakutana na changamoto ambazo zitakutaka usubiri. Katika wakati ambao unasubiri, usiupoteze, badala yake utumie kwa manufaa. Jua na Pata vitu muhimu vitakavyokusaidia kwenye safari yako.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha.

    Maureen Kemei.

  • 12/100.Changamoto hazitakoma.

    Habari.

    Karibu sana rafiki katika kujifunza namna ya kupata hazina ya maisha kupitia kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Wakiwa wanaendelea na safari jangwani, taarifa zilikuwa zinawafikia kwamba Kuna vita vinaendelea jangwani. Hivyo msafara ulipaswa kwenda kwa umakini zaidi. Hivyo walipofika eneo la jangwa lenye maji na makazi (oasis) msafara ulisimama kwa muda mpaka pale vita vitakapoisha. Haikujulikana ni muda gani itachukua kumalizika kwa vita hivyo.

    Santiago alizidi kuona jinsi safari ya kufikia ndoto yake inakuwa ngumu, akiwa ameshafika jangwani na kukaribia mapiramidi, anakutana na kikwazo cha vita, alipatwa na hali ya kukata tamaa.

    Lakini alijiambia anapaswa kuwa na subira, uchungaji wa kondoo umemfundisha subira ambayo anaihitaji sana kwa sasa. Wakati akiwa anafikiria kuhusu kikwazo hicho, alikutana na mwendesha ngamia ambaye walikuwa naye kwenye msafara.

    Alionekana kutokuwa na wasiwasi na Santiago alipenda kujifunza kutoka kwake. Mtu yule alimwambia kwamba huwa anafanya kitu wakati kukifanya, kama anakula basi mawazo yake yote yanakuwa kwenye kula na siyo sehemu nyingine yoyote.

    Alimwambia haishi kwenye Jana wala kesho, bali anaishi kwenye wakati uliopo, hivyo hahofii changamoto yoyote inayokuja, bali anakabiliana nayo anapokutana nayo.

    Kwenye safari ya ndoto yako, changamoto na vikwazo havitakoma, wajibu wako ni kukabiliana nazo. Usisumbuke na mambo yaliyopita wala yale yajayo, badala yake ishi kwenye wakati uliopo, mawazo yako yote yawe kwenye kile unachokifanya na hakuna kitachokushinda.

    Asante Sana mwanamafanikio mwenzangu, tukutane wakati mwingine.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha.

    Maureen Kemei.

    Kemeimaureen32@gmail.com.

  • 12/100.Jifunze kutoka kwa wasafiri wengine.

    Habari.

    Karibu katika safari yetu ya kutafuta hazina ya maisha, tukiendeleza kabisa uchambuzi wa kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Santiago libeba akiba yake yote na kujiunga na msafara unaoelekea jangwani. Msafara ulikuwa na watu wengi na huko alikutana na mwingereza ambaye alikuwa anaenda jangwani kumtafuta mtu mwenye uwezo wa kubadili madini ya kawaida kuwa dhahabu ‘alchemist’.

    Alikuwa amebeba mabegi yaliyojaa na muda mwingi alitumia kusoma vitabu kuhusu ujuzi huo wa kubadili madini kuwa dhahabu. Wakitengeneza ukaribu na Santiago ambapo alimweleza vitu vingi kuhusu utalaamu huo,na kumweleza habari za mtu aliyeishi jangwani, ambaye ana vitu viwili, jiwe ambalo lina nguvu ya kubadili madini ya kawaida kuwa dhahabu (philosopher’s stone) na kimiminika ambacho kinaweza kuponya ugonjwa wowote (elixir of life).

    Kupitia mtu huyu Santiago alijifunza vitu vingi sana kuhusu utalaamu huo wa kubadili madini ya kawaida kuwa dhahabu (alchemy) na kuvutiwa kujua zaidi.

    Mtu huyo alimfundsha kuhusu lugha ya dunia na umuhimu wa kufahamu kwa sababu inamwongoza mtu kufanya yaliyo sahihi.

    Kwenye safari ya kuelekea kwenye ndoto zako, utakutana na wasafiri wengine, hakikisha unajifunza kupitia wasafiri hao,kwa sababu watakuwa na ujuzi na uzoefu tofauti na ulionao wewe.

    Una kitu cha kujifunza kutoka kwa yeyote unayekutana naye, kuwa tayari kujifunza. Tukutane baadae rafiki yangu uwe na wakati mwema.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio na maisha Maureen Kemei

    Kemeimaureen32@gmail.com.

    0713698650

  • 11/100.Usisahu ndoto, hata mambo yakiwa mazuri kiasi gani.

    Habari

    Karibu katika Kuendelea kujifunza kutoka kitabu cha ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho. Kinachotufunza na kutuelekeza namna ya kupata hazina yetu.

    Santiago alifanya kazi kwa mwaka mzima kwenye duka lile, wakati anaanza lengo lake lilikuwa ni apate fedha za kununua kondoo wake wa kurudi kwenye uchungaji.

    Lakini baada ya mwaka, alikuwa amepata fedha nyingi za kumwezesha kununua kondoo wengi aliokuwa nao mwanzo. Pamoja na kupata fedha hizo nyingi,hakurudi kwenye uchungaji, wala Kuendelea kubaki kwenye duka lile.

    Alikumbuka ndoto yake ya kufika kwenye mapiramidi n kuipata hazina yake. Hivyo alimuaga mwenye duka, ambaye alisikitika sana kumpoteza Santiago ambaye aliweza kuifufua sana biashara yake.

    Santiago alipata taarifa za kutosha kuhusu kwenda kwenye mapiramidi, aliambiwa kuna msafara wa watu unaoelekea jangwani na huo utamwezesha kufika kwenye mapiramidi.

    Watu wengi huwa wanazisahau ndoto zao pale wanapopitia kwenye hali nzuri, unakuta, mtu alikuwa na ndoto ya kuwa na biashara fulani,lakini hana mtaji wa kuanza biashara hiyo.

    Hivyo, anatafuta kwanza ajira, pale ajira inapomlipa vizuri, anasahau ndoto yake na Kuendelea na ajira hiyo. Haijalishi mambo ni mazuri kiasi gani, kama utaisahau ndoto yako, baadaye itakusumbua.

    Rafiki yangu usisahau ndoto yako unapopata ajira inayokulipa vizuri, nikutakie siku njema tukutane kesho.

    Makala hii imeandikwa na mwanafunzi :

    Maureen Kemei.

    Kemeimaureen@gmail.com.

    0713698650

  • 11/100.Toa thamani kwa chochote unachokifanya zaidi.

    Habari

    Karibu tuendeleze uchambuzi wetu wa ‘the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho. Kinachotufunza na kutuelekeza namna ya kupata hazina yetu.

    Baada ya Santiago kupata kazi kwenye duka, alijituma sana katika kazi yake aliwahudimia wateja vizuri na mauzo yalianza kuongezeka.

    Mwenye duka alifurahia sana hili, alimwambia Santiago kwamba amekaa kwenye biashara hiyo kwa miaka 30 na alishakata tamaa kwamba biashara hakuna tena, lakini tangu yeye amefika, biashara imekuwa zaidi.

    Santiago aliona fursa nyingine, mahali palipokuwa na duka, hapakuwa na mgahawa au eneo la kupumzika. Na aliwasikia wateja wakilalamika kwamba hakuna sehemu wanayoweza kupumzika na kupata kinywaji chochote.

    Santiago aliona fursa ya kuuza chai ndani ya duka hilo la vyombo, hivyo akaweka mpango na kushirikisha mwenye duka. Aliposikia mpango huo aliukataa, alimwambia Santiago kwamba yeye yupo kwenye biashara ya vyombo na siyo ya kuuza chai.

    Alimweleza hawezi kukabiliana na wingi wa wateja watakaokuja kwa ajili ya chai.Santiago alimweleza kwamba hiyo ni fursa ambayo kama hawtaitumia basi itawapita. Mwenye duka alikubali shingo upande na kumwambia Santiago ajaribu mpango wake.

    Ulikuwa ni mpango bora sana, wateja waliongezeka na wengi walisifu na kushukuru kwa huduma hiyo. Mauzo yaliongezeka sana, mwenye duka hakuamini kwamba biashara ingeweza kuwa vizuri kiasi hicho.

    Popote unapopata nafasi ya kufanya kazi au kuwahudumia wengine, kazana kutoa thamani kubwa zaidi, usifanye kitu tu unachopaswa kufanya, nenda hatua ya ziada.

    Utakapoomba kwenda hatua ya ziada ambao hawajazoea kwenda watakupinga, lakini utakapo toa thamani kila mtu atakuwa tayari kukulipa zaidi.

    Popote ulipo na kwa chochote unachofanya, jiulize unawezaje kuongeza thamani zaidi na fanya hivyo.

    Naamini mwanamafanikio mwenzangu umetoka na kitu ya kufanyia kazi, kutoa thamani kwa vyovyote vile unavyovifanya.

    Limeandikwa na mwanafunzi

    Maureen Kemei

    Kemeimaureen32@gmail.com.

    0713698650

  • 10/100. Angalia wapi panahitaji msaada wako na toa msaada huo.

    Habari

    Karibu tuendelee kujifunza kutoka kitabu cha ‘the alchemist’ ambacho kinamaanisha namna ya kupata hazina ya maisha yako.

    Santiago alitafuta mahali pa Kulala na kesho yake alipoamka aliamua kutembea kujionea maeneo mbalimbali. Ilipofika mchana alikuwa na njaa lakini hakuwa na fedha ya kununua chakula.

    Hivyo katika matembezi aliona duka mbali lilikuwa likiuza vyombo. Aiingia kwenye duka lile na kumwomba mwenye duka amsaidie kazi ili ampe chakula, lakini mwenye duka akamwambia hana kazi ya kumpa, kwa sababu hakuna wateja wengi kama zamani.

    Santiago alichukua kitambaa na kuanza kufuta vyombo vile ambavyo vingi vilikuwa na vumb. Alifuta kwa umakini mkubwa na ilianza kuonekana vizuri. Akiwa anaendelea na zoezi hilo wateja wawili walikuja na kununua.

    Baadaye mwenye duka alimpeleka kupata chakula na kumwambia “nitakupa kazi kwenye duka langu,ulipokuwa unafuta vyombo, Kuna wateja wamekuja na kununua, hiyo ni dalili nzuri”. Na hapo alipata kazi.

    Haijalishi upo chini kiasi gani Kuna msaada unaweza kutoa kwa wengine na usisubiri mpaka mtu akuambie umsaidie. Badala yake angalia uhitaji ambao mtu anao kisha jitoe kumsaidia, utakapozalisha thamani lazima mtu atakulipa.

    Angalia ujuzi na uzoefu ulionao, angalia muda ulionao na kisha jiulize ni watu gani wanaweza kunufaika na hivyo ulivyonavyo, kisha vitoe kuwasaidia na utakapowapa thamani watakuwa tayari kukulipa.

    Shukrani mwanamafanikio mwenzangu kwa kusoma makala hii imeandikwa na

    Maureen Kemei ambaye ni mwanafunzi wa mafanikio na anajifunza sana kupitia Kazi za Kocha na daktari Makirita Amani. Uwe na wakati mwema.

    Mawasiliano :

    Email.

    Kemeimaureen32@gmail.com.

    0713698650

  • 9/100.makosa yasikurudishe nyuma.

    Habari

    Karibu tuendelee na kujifunza kutoka kitabu cha’ the alchemist’ kilichoandikwa na Paulo Coelho.

    Baada ya kuwa ametapeliwa fedha zake zote, Santiago alijikuta amesimama mwenyewe gulioni na hakuna mtu mwingine yeyote.

    Alifungua pochi lake na kuangalia kitu gani kilichobaki, kulikuwa na kitabu, koti na mawe mawili aliyopewa na yule mzee aliyekutana naye.

    Baada ya kuyaangalia mawe yale, alipata nafuu fulani, na kuona pamoja na kwamba amepoteza kila kitu, lakini ana kitu cha kumwongoza.Alifikiria jinsi alivyouza kondoo wake wote akijua anaenda kupata hazina yake, lakini ameishia kupoteza kila kitu.

    Hakuruhusu hilo limkatishe tamaa wala kurudi nyuma, badala yake aliangalia kile alichonacho na kuchagua kusonga mbele. Alijua hawezi kupoteza tena kama atafuata mwongozo ambao dunia inampatia.

    Makosa yoyote utakayofanya kwenye safari yako ya kuelekea kwenye hazina, haijalishi ni makubwa kiasi gani na yamekupa hasara kiasi gani, usikubali yakurudishe nyumba.

    Kila unapoanguka, amka na angalia wapi unaweza kuanzia ili Kuendelea na safari yako.

    Asante rafiki yangu kwa kusoma makala hii imeandikwa na mpishi Kemei Maureen.

    Ambaye ni mwanafunzi wa mafanikio na maisha, na pia anajifunza mengi kutoka kwa kocha na daktari Makirita Amani.

    Mawasiliano

    Email :Kemeimaureen32@@gmail.com.

    0713698650