Home

  • 51/100. Mabadiliko ni kitu ambacho hakitabadilika.

    Karibu, tujifunze zaidi kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century ambacho kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Kitu pekee ambacho hakitabadilika ni mabadiliko, kila kitu kinabadilika na kitaendelea kubadilika. Na eneo ambalo linaathiriwa sana na mabadiliko ni elimu. Namna ambavyo tumekuwa tukifundishwa na kufundisha imepitwa na wakati.

    Kufundishwa kwa kukariri kulifanya vizuri enzi ambazo maarifa yalikuwa adimu. Lakini katika zama hizi maarifa ni mengi, kukariri ni njia iliyopitwa na wakati

    Kukariri pia kinachosha kwenye zama hizi ambazo hutaweza kuwa na kazi moja na ukadumu nayo. Kila wakati utapaswa kubadilika kwa namna mambo yanavyobadilika, utapaswa kupata maarifa mapya na ujuzi mpya wa kufanya vitu vipya.

    Mfumo wa elimu na hata kufunza unapaswa kubadilika, badala ya kuwapa wanafunzi maarifa zaidi ya kukariri, elimu inapaswa kujengwa kwenye misingi minne;Kufikiri kwa kina, mawasiliano, ushirikiano na ubunifu.

    Mtu akibobea kwenye maeneo hayo manne, ataweza kujifunza vitu vingine mwenyewe na pia kushirikisha na wengine vizuri, kitu ambacho ni muhimu kwenye karne hii ya 21.

    Pia watu wanapaswa kufundishwa zaidi stadi za maisha na namna ya kukabiliana na mabadiliko yanayoendelea kutokea.

    Hatua ya kuchukua tunapswa kukataa elimu ya kukariri na kutafuta elimu inayotufikirisha hili ya tusaidie katika utatuzi wa changamoto za maisha.

    Ahsante kwa kusoma nakala hii, imeandikwa na mwanafuzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei

    Blog :kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 50/100. Wakati ujao siyo kama tunavyoona kwenye sinema.

    Karibu

    Katika kujifunza zaidi kuhusu changamoto zinazotukabili karne hii ya 21, kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century, ambacho kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Kumekuwepo na sinema nyingi ambazo zinaonesha hali itakavyokuwa baadaye. Baadhi ya sinema hizi kama the matrix zimekuwa zinaonyesha nguvu kubwa ya teknolojia kuja kudhibiti na kutawala wanadamu.

    Lakini sehemu kubwa ya yale yanayoonyeshwa kwenye sinema hizi siyo yanayotokea.

    Tuna wajibu wa kutengeneza sinema zinazoendana na uhalisia,zinzojengwa kwenye misingi ya tafiti za kisayansi ili kuwaelewesha mambo magumu kwa njia rahisi.

    Sinema ni njia rahisi kutoa ujumbe mgumu na kueleweka kirahisi . Sisi binadamu tunaelewa zaidi kwa hadithi kuliko kupewa ukweli kama ulivyo.

    Zikitengenezwa hadithi nzuri za namna siku za mbeleni zitakavyokuwa, watu watajifunza na kuchukua hatua.

    Nikushukuru sana kwa Kuendelea kusoma nkala hii, tukutane kesho. Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei.

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 49/100. Habari ya uongo unadumu muda mrefu.

    Karibu, katika kujifunza zaidi kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century. Leo tukiwa changamoto ya 16 kati ya 21 ambayo mwandishi Mwana historia Yuval Noah Harari ametushirikisha.

    Changamoto nyingine kubwa kwenye karne ya 21 imekuwa ni habari za uongo au kama ambavyo imekuwa ikichulikana kama fake news.

    Imechochewa zaidi na urahisi wa kuzambaa kwa taarifa kupitia kwa mtandao wa kijamii. Pia kwa mitandao ya kijamii kujua tabia za watu, habari za uongo zinasambaa kitabaka na kuweza kutengeneza matabaka baina ya watu.

    Changamoto ya habari za uongo haijaanza leo, tunaweza kusema maisha ya mwanadamu yamekuwa yanaongozwa kwa habari na hadithi za uongo.

    Kwenye kila jamii utakutana na hadithi nyingi za kishujaa ambazo ni za uongo kabisa, hazina ukweli wowte. Lakini watu wameishi nazo milele kuziamini.

    Kadhalika kwenye dini, zipo habari na hadithi nyingi ambazo ni za uongo kabisa, ambazo haziendani hata na uhalisia wa kawaida, lakini watu wanazichukulia kama ukweli.

    Hivyo tunapaswa kujua ukweli siyo kitu ambacho watu wanakitafuta sana, na kama unataka ukweli, ni jukumu lako kuutafuta na siyo kutegemea wengine wakupe ukweli.

    Kama unataka kupata habari na taarifa za kweli, kwanza lazima uwe tayari kulipia, kama unapata taarifa na maarifa yako bure, jua kuna aliyelipia wewe uyapate bure na huyo atakuwa na ajenda yake binafsi.

    Pili mwandishi anasema soma vitabu na tafiti zilizofanyika kisayansi, usitumie habari unazopata kwenye vyombo vya habari na mitandao kama ndiyo ukweli, kila unachosikia kwa wengine chukulia kama maoni, na ukitaka ukweli nenda kauchimbe sehemu sahihi.

    Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei

    Blog :kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 48/100. Maana tuliyonayo kwenye haki imepitia na wakati.

    Karibu

    Katika kujifunza kwetu kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century, ambapo leo tupo kujifunza changamoto ya 15 kati ya 21. Tumeshirikishwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Dhana ya haki ni changamoto kubwa kwenye karne ya 21,hasa wakati ambapo nguvu ya dini inapungua na teknolojia inakua kwa kasi.

    Dhana ya haki tuliyokuwa nayo ni kufuata misingi na maadili fulani. Lakini kwa Sasa dhana hii haiwezi kufanya kazi, kwa sababu unaweza kufuata misingi na maadili, na bado unachofanya kikawa siyo haki kwa wengine.

    Mfano unafuata misingi na maadili yako katika fedha na hivyo kuamua kuwekeza fedha zako ili baadaye usiwe na shida ya kipato.

    Lakini kampuni uliyowekeza fedha, ikawa inachafua mazingira, au inawanyonya wafanyakazi au wakulima au inazalisha bidhaa ambayo inaleta uharibifu kwenye afya za wengine, je hapo wewe umetenda haki?

    Katika karne ya 21, dhana sahihi ya haki ni kuangalia kisababishi na matokeo. Tunapaswa kuangalia kila hatua tunayochukua inaleta madhara gani kwa wengine.

    Japokuwa siyo mara zote unaweza kuona madhara kwa usahihi, lakini kujua kwamba dhana uliyonayo kwenye haki imepitwa na wakati, kunakusaidia kufikiri na kukazana zaidi ili kuweza kutenda haki kwa wengine.

    Shukran kwa Kuendelea kusoma nakala hii, tukutane kesho. Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei

    Blog:kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 47/100. Unajua kidogo mno kuliko unavyofikiri.

    Karibu, katika kujifunza zaidi kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Kwa kuwa tunaishi zama za taarifa ambapo maarifa yanapatikana kwa urahisi, watu wengi wamekuwa waifikiri wanajua sana. Watu wamekuwa wakiamini wanafikiri kwa kina na kufanya maamuzi sahihi.

    Lakini tafiti zinaonesha huo siyo ukweli. Maamuzi mengi tunayofanya tunatumia kundi, kwa kuiga kile ambacho wengine wamefanya na kuamini ni sahihi na pia tunatumia hisia, tunatumia fikra zetu kwa kiasi kidogo.

    Kuna vitu vingi sana vya kujua kiasi kwamba hakuna anayeweza kujua vyote, na kila siku vitu vipya vinagunduliwa. Hivyo badala ya kujidanganya kwamba tunajua sana na kufikiri tunafanya maamuzi kwa fikra zetu, ni vyema tukakubali udhaifu wetu ili tunapofanya maamuzi tujue hasa ni wapi tunaegemea.

    Na zama tunazoishi sana ni hatari zaidi kwa sababu ujuzi wetu unazidi kupungua. Hii ni kwa sababu tunategemea zaidi wengine katika kufanya maamuzi. Watu wamekuwa wavivu wa kusoma vitabu na wanapenda kusikiliza wengine wanasema nini au wanafanya nini na wao ndiyo wafanye.

    Ili kuondokana na hatari hii, lazima tuwe tayari kuweka muda na nguvu katika kuboresha ujuzi wetu na kuongeza maarifa tuliyonayo, hasa kwa yale maeneo muhimu kwetu.

    Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 46/100.Kutambua kivuli cha mfumo wa kidunia.

    Karibu, katika kujifunza changamoto ya karne ya 21, leo ikiwa tupo changamoto ya 14. Kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century ambacho kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Baada ya dini kushindwa, kutokana na machafuko mengi kuhusishwa na dini, njia bora ya kuendesha nchi na hata jamii imekuwa ya kidunia, kwa kutokuegemea upande wowote wa dini.

    Hapa taifa linakuw halina dini, ila mwananchi mmoja mmoja ana uhuru wa kuchagua dini yake na haruhusiwi kuingilia dini ya mwenzake.

    Huu ni mfumo bora ambao umeleta utulivu kwa nchi nyingi duniani, pia umetoa uhuru kwa wengi. Kwa sababu katika mataifa yanayoendeshwa kwa sheria za dini, kila mtu inabidi akubaliane na wengine wote, hata kama hana imani iyo.

    Mfano kama wewe ni mkristo na unaishi kwenye nchi inayoendeshwa kwa sheria za kiislamu, hutaruhusiwa kula hadharani wakati wa mfungo wa Ramadhani.

    Moja ya misingi muhimu sana kwenye kuishi kidunia ni kutafuta ukweli kuutumia ukweli kama kigezo cha kufanya maamuzi, kitu ambacho kwenye dini hakipo.

    Dini nyingi zinaendeshwa kwa imani na siyo ukweli. Ukitaka kuhoji ukweli kwenye dini utaambiwa unakosa imani.

    Kwa kutambua uvuli cha udunia na kutumia ukweli kama misingi wa maamuzi kunaufanya mfumo wa kidunia kuwa bora katika na ushirikiano kuliko mfumo wa kidini.

    Nakushukuru kwa Kutenga muda wako kusoma nakala hii, tukutane kesho. Kimeandikwa na mwanafuzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei

    Blog, kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 45/100. Kutotaja bure jina la Mungu.

    Pongezi Mwana mafanikio kwa kuzidi kujifunza kila siku. Hilo ndilo muhimu zaidi katika kulisha akili zetu, kama tufanyavyo kwa mwili. Leo tupo changamoto ya 13 kati ya 21 ambazo tunajifunza kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Changamoto nyingine kubwa karne hii no uwepo wa Mungu. Mjadala kama Mungu yupo au la umekuwepo miaka na miaka. Lakini katika zama zilizopita haukuwa unapata nguvu kwa kuwa majibu ya matatizo ya wengi yalikuwa yanatolewa na viongozi wa kidini.

    Kama mtu aliumwa alienda kuombewa au kufanyiwa uganga na akapona. Kama mvua haikunyesha basi watu waliomba na wengine kutoa kafara n mvua zikanyesha.

    Pale ambapo watu waliioombewa hawakupona, au mvua haikunyesha baada ya maombi au kafara, Ilionekana Mungu alikuwa na hasira sana na kuamua kuwaadhibu watu wake.

    Lakini siku hizi watu wana uelewa wa matatizo mbalimbali na namna ya kuyatatuta. Ukiumwa unajua unaenda hospitali kupata tiba, na hata kama utaombewa, lakini bado utategemea tiba ya kisayansi. Kama mvua hainyeshi tunajua Kuna uchafuzi wa mazingira unaobadili hali ya hewa.

    Maendeleo haya yamepunguza sana nguvu ya dini katika kutoa suluhisho la matatizo mbalimbali.

    Lakini pamoja na hayo, bado jina la Mungu limekuwa linatumika katika maeneo ambayo halipaswi kutumika. Amri ya tatu katika amri kumi za Mungu inasema usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako.

    Wengi wamekuwa wanachukulia amri hii kama kutokutamka jina la Mungu kila wakati, lakini kama amri hii ukiitafakari kwa kina inamaanisha usimtumie Mungu kwa sababu ya wewe kufanya unachotaka kufanya.

    Tumekuwa tukiona nchi zinaingia kwenye vita kwa kizingizio cha kutetea jina la Mungu, au watu kugombana na wengine kwa kumtetea Mungu.

    Mwandishi anatamatisha mada hii kwa kusema, kama unataka kufanya mambo yako fanya, lakini usiyahusishe na jina la Mungu. Kama Mungu yupo ana majukumu makubwa ya kuiendesha hii dunia kuliko kukutegemea wewe uue wengine au kutesa wengine ili kumfurahisha yeye.

    Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei.

    Blog :kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 44/100. Hakuna aliye kitovu cha dunia.

    Siku nyingine ya ushindi, tunaenda kujifunza zaidi kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century, ambacho kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Mwandishi anasema kuwa, changamoto kubwa ya karne hii ni unyenyekevu. Wengi wamekuwa wakiamini wao ni bora zaidi kuliko wengine,kuanzia kwenye ngazi ya jamii, dini na hata taifa.

    Hali hii ya kujiona wa muhimu kuliko wengine ndiyo imezalisha matatizo makubwa sana hapa duniani. Kuanzia mapigano ya kikabila, machafuko ya kidini na hata vita ya dunia.

    Ukweli ni kwamba mataifa na hata dini ni vitu vilivyotengenezwa na wanadamu, na havina miaka mingi ukilinganisha na muda ambao wanadamu wamekuwa hapa duniani.

    Tafiti zinaonesha binadamu ameishi hapa duniani kwa zaidi ya miaka milioni moja, lakini dini yenye umri mkubwa sana ni miaka elfu tatu, na mataifa mengi hayana hata miaka elfu moja ya kuwa kama taifa.

    Hivo ukilinganisha uwepo wa binadamu na uwepo wa hizi taasisi, binadamu wamekuwepo muda mrefu. Hivyo kufikiri dini au taifa fulani ni bora kuliko upande mwingine ni kujidanganya.

    Tunapswa kuwa na unyenyekevu na kuelewa kwamba taasisi zote zinazotuleta pamoja hazina nguvu kutushinda sisi wanadamu. Taifa, dini na hata taasisi nyingine, ni vitu ambavyo vilitengenezwa na watu, hivyo vina uimara wake na madhaifu yake.

    Kusema upande mmoja ni bora kuliko mwingine na kutaka kuonesha hilo, ndilo upumbavu wa mwanadamu ambayo huleta madhara makubwa kwa dunia zima.

    Imeandikwa na mwanafunzi wa ushauri nasaha, mafanikio ya maisha na uandishi.

    Maureen Kemei.

    Blog kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 43/100. Changamoto ya vita.

    Karibu, katika kujifunza kwetu kutoka kitabu cha 21 lessons for the 21st century kimeandikwa na Mwana historia Yuval Noah Harari.

    Leo tupo changamoto ya kumi ambapo mwandishi anatushauri kuwa, tusichukulie poa upumbavi wa mwanadamu.

    Vita ni changamoto nyingine kubwa katika karne hii, japo hakuna vita kubwa ambayo imewahi kuwepo hapa duniani tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia, bado vita ni changamoto kubwa.

    Ni changamoto kubwa kwa sababu uwezo mkubwa wa kijeshi na uwepo wa silaha za maangamizi ni hatari sana kwa dunia nzima.

    Hivyo tunaweza Sema kwamba uwezo huu wa maangamizi inaweza kuwa kitu cha kutupa hofu tusijihusishe na vita, lakini tusichukue poa upumbavi wa mwanadamu.

    Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa wazuri katika kutengeneza zana bora, lakini hatuwezi kuzitumia vizuri. Hivyo tunapaswa kuwa na njia bora ya kuhakikisha maendeleo makubwa tuliyofikia hayawi chanzo cha kuondoa maisha duniani.

    Njia bora kabisa ya kuzuia upumbavu wa mwanadamu usiwe angamizo kwa dunia ni kwa watu kujifunza unyenyekevu na kuwajali wengine. Ile dhana kwamba taifa letu ni bora kuliko mataifa mengine au dini yetu ni bora kuliko dini dini nyingine ndiyo imekuwa chanzo cha vita nyingi.

    Kama watu watajifunza kwamba kila mtu ni muhimu na kila mtu ni bora, ushirikiano utakuwa nzuri na hapatakuwa na vita.

    Nikushukuru sana kwa Kuendelea kusoma nakala hii, imeandikwa mwanafunzi wa ushauri nasaha, mafanikio ya kuimarisha na uandishi.

    Maureen Kemei

    Blog :kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.

  • 42/100.Tusiwe na hofu ya magaidi.

    Hongera kwa Kuendelea kujifunza, leo tupo katika changamoto ya kumi kati ya 21. Ambapo Mwana historia Yuval Noah Harari, ametushirikisha katika kitabu chake cha 21 lessons for the 21st century.

    Hofu kubwa inayowatawala watu kwa sasa, kuanzia uongozi wa jumuia za kimataifa, uongozi wa nchi na hata mwananchi mmoja mmoja ni ugaidi. Magaidi wameweza kutumia hofu zetu wenyewe kututawala.

    Tukio kubwa la kigaidi ambalo limetokea kwenye karne ya 21 ni la septemba 11 2001, lakini baada ya hapo matukio yanayofuatia ya kigaidi ni madogo mno.

    Kwa mfano kwa mwaka watu 25,000 wanauawa kwenye matukio ya kigaidi, na hili linatupa taharuki kubwa Sana ugaidi ni hatari kubwa ya dunia.

    Lakini tukiangalia hizi namba nyingine za kifo ;kwa mwaka watu 1,250,000 wanakufa kwa ajali duniani, watu zaidi ya milioni tatu wanakufa kwa kisugari na uchafuzi wa hali ya hewa unaua watu zaidi ya milioni 7.

    Tukilinganisha vifo vya ugaidi na vifo tutaona namna ambavyo vingine ugaidi unasababisha vifo vichache, lakini wote tunahofia sana ugaidi kuliko ajali au kisugari.

    Ugaidi unatumia hofu zilizopo ndani ya watu kuwaumiza wao wenyewe. Kwa kutokuwa na uhakika na kutokujua ni wakati gani tukio la kigaidi linaweza kutokea, watu wanakuwa na hofu mara zote.

    Magaidi hutumia hofu kuwasukuma mataifa kusaidia kazi zao. Mfano, kama kikundi la kigaidi linatoka kushambulia Iraq lakini hakina uwezo wa kijeshi, kinachofanya ni kuendesha vitendo vya kigaidi kwenye nchi kama marekani kwa mgongo wa Iraq, kisha taifa hilo kinataharuki na kuvamia nchi ya Iraq. Hivyo kazi ya kikundi cha kigaidi inakuwa imekamilika bila ya wao kuingia kwenye vita, ni kama wanasaidiwa.

    Hivyo kitu sahihi kufanya kwenye ugaidi ni kutokuwa na hofu na kwa taifa kutotaharuki. Hii haimaanishi mataifa yasipambane na ugaidi,bali mataifa yawe na utulivu badala ya kutaharuki na  kuzalisha matatizo zaidi, kama ilivyotokea mashariki ya kati.

    Imeandikwa na mwanafunzi wa mafanikio, ushauri nasaha na uandishi.

    Maureen Kemei.

    Blog:kufikirichanya.wordpress.com

    Maisha yangu, uchaguzi wangu.