-
Kwa nini ni muhimu kutafuta ushauri kutoka kwa watu unaowajua wamefanikiwa.
Kumbuka rafiki yangu kwamba, watu wanaokuambia huwezi, mara nyingi ni watu wa kawaida saana,na ni watu ambao hawana mafanikio.
Mawazo na mawaidha ya watu hawa yanaweza yakawa ni sumu kwako. Unapaswa ujiwekee ulinzi dhidi ya watu wanaokushawishi kwamba huwezi kufanikisha jambo fulani.
Kamwe husikubali watu wenye fikra hasi wakuvute chini kwenye sehemu yao walipo. Fanya hivi kuwa na sheria, tafuta ushauri kwa watu unaowajua wamefanikiwa.
Kuna madai au hata fikra ambazo sio sahihi eti kwamba, watu waliofanikiwa hawaingiliki! Hicho ni kitu ambacho hakina uhalisia.
Ukweli ni kwamba kadiri watu wanavyozidi kupata mafanikio makubwa ndivyo wanavyozidi kuwa wataratibu na wapo tayari kuwasaidia wengine.
Tengeneza mahusiano na kundi lingine la watu, kundi la watu wenye mafanikio makubwa kukuzidi. Pia unapaswa kutengeneza mtandao wa marafiki mapya.
Chagua marafiki ambao wana mawzo tofauti na ya kwako. Kama vile watu wa dini tofauti, vyama tofauti tofauti, lakini wawe na faida kwenye upande wako.
Hatua ya kuchukua, jihusishe na watu au marafiki ambao wanapenda vitu chanya, wanapenda kazi, kuweka bidii kwenye mambo yenye tija. Ambao wanapenda kukuona ukifanikiwa, au ukipiga hatua kwenye maisha yako.
Kutoka kwa anayekujali sana.
Maureen Kemei.
-
Dalili kuu za watu wasiosaidika.
” It’s hard to help people who don’t think they have a problem. It’s impossible to fix people who think someone else is the problem. ” Marshall Goldsmith.
Kuna watu unaweza kuwa unakazana kuwabadili sana kwenye maisha yako. Unawawekea vizuri mazingira yote yatakayowasaidia kwenye kubadilika lakini hawabadiliki.
Wakati mwingine ni wewe wenyewe, unasukumwa sana kubadilika lakini hubadiliki.
Unapaswa kujua dalili kuu ya watu wasiosaidika kwenye maisha, ili uache kupoteza nguvu zako kwa wengine.
Ukikutana na mtu ambaye anafikiri hana tatizo au anafikiri watu wengine ndiyo tatizo, basi jua hapo umekutana na mtu ambaye hawezi kusaidika. Huwezi kufanya chochote kikamsaidia mtu wa aina hii mpaka pale atakapokubali kwamba ana tatizo.
Na hili pia lianzie ndani yako mwenyewe, kama unafikiri huna tatizo, kama unafikiri watu wengine ndiyo tatizo kwenye maisha, nakuhakikishia wewe ni mzigo mkubwa kwa watu wengine. Huenda hawakuambii lakini unawapa mzigo sana.
Anza kujikagua na kujitathmini mwenyewe, anza na wale watu ambao unawalalamikia na kuwaona ni kikwazo kwenye maisha yako, na jiulize ni jinsi gani na wewe umechangia kwenye tatizo hilo.
Kama kwa mfano ni mahusiano yako kwenye kazi, biashara na hata maisha hayajakaa vizuri, tatizo siyo watu wengine, tatizo ni wewe. Na kama hutakiri kwamba tatizo ni wewe, utaendelea kusumbuka maisha yako yote.
Upo usemi kwamba kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua, na hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye matatizo binafsi, kujua kwamba wewe ni tatizo, ni hatua ya kwanza kwako kupiga hatua na kuwa bora zaidi.
Hatua ya kuchukua, usiwe mtu usiyesaidia, kubali pale ambapo wewe ni tatizo, kuwa tayari kubadilika na utaweza kupiga hatua zaidi.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
-
Aina 2 ya usumbufu.
Ubongo wetu ni rahisi sana kusumbuliwa, tunapokuwa tunafanya kazi, kitu chochote kipya kinachotokea, ni rahisi kututia kwenye kile tunachofanya na kujihusisha na kitu hicho kipya. Ndiyo maana ni vigumu sana kufanya kazi muhimu ukiwa kwenye eneo lenye kelele, akili yako haiwezi kutulia kwenye kile unachofanya.
Kuna usumbufu wa nje, ambao unatokana na vitu vipya vya nje ambavyo ubongo unashawishika kujihusisha navyo. Simu zetu za mkononi ndiyo chanzo kikuu cha usumbufu wa nje. Tafiti nyingi zinaonesha watu hawawezi kukaa kwa zaidi ya dakika kumi bila kuangalia simu zao, kitu ambacho kinawazuia kuweka umakini kwenye kazi zao.
Hivyo kama unataka kuwa na ufanisi mzuri, pale unapokuwa unafanya jukumu muhimu, zima kabisa simu yako. Au iweke kwenye ukimya na ikae mbali kabisa na wewe. Pia fanya kazi zako eneo ambalo halina usumbufu wa watu wengine au makelele.
Aina ya pili ya usumbufu ni usumbufu wa ndani, hapa akili yako mwenyewe inakuwa inahama hama kutoka kwenye kitu kimoja na kwenda kwenye kitu kingine. Kama hutaweza kuidhibiti akili yako na kuiweka kwenye kile unachofanyia kazi, utajikuta unachoka sana lakini haikamilishi unachofanya.
Njia bora ya kuondokana na usumbufu huu ni kujikamata pale mawazo yako yanapotaka kuhamia na kuyarudisha kwenye kile unachofanya. Ukichelewa kujikamata na ukajikuta mawazo yameshahamia sehemu nyingine, inakuwa kazi kubwa kuyarudisha kwenye kazi kuu.
Hatua ya kuchukua, kuwa mlinzi wa mawazo yako na yakamate pale yanapotoroka na uyarudishe kwenye jukumu kuu.
Akujaliaye sana
Maureen Kemei.
-
Kujijua ni nini hasa katika saikolojoa.
Mimi ni nani? Swali rahisi lakini la kina kabisa. Swali lingine la uchochezi ni “kwa nini ninatenda jinsi ninavyofanya?”
Ikiwa unajiuliza maswali kama hayo, hauko peke yako. Wakati hatujitambui au kutenda kwa njia ambazo hatuelewi au hatupendi, inaweza kuwa ishara kwamba mabadiliko yanafaa. Lakini swali ni je, tunabadilikaje? Na nini kinachohitajika hili kubadilishwa?
Einstein aliwahi kutafakari, ‘ni watu wangapi wamenaswa katika mazoea yao ya kila siku:sehemu wanakufa ganzi, sehemu wanaogopa au sehemu hawajali? Ili kuwa na maisha bora, lazima tuendelee kuchagua jinsi tunavyoishi.
Ujinga, woga na Kutojali hakutoi msukumo wa kujitambua au kuleta mabadiliko chanya. Kinyume chake, uchanganuzi wa kibinafsi husababisha kujijua, ambayo ni hatua ya kwanza ya lazima katika kuanzisha mabadiliko chanya.
Kujijua katika saikolojoa ni “habari halisi ambayo mtu anayo kujihusu.” (Morin and Racy, 2021,p,373). Hii inajumuisha maelezo kuhusu hali yetu ya kuhisia, hulka za utu, mahusiano, mifumo ya kitabia, maoni, imani, maadili, mahitaji, malengo, mapendeleo na utambulisho wa kijamii.
Maarifa ya kibinafsi yanatokana na michakato ya kujitafakari na kijamii. Walakini, ujuzi wa kibinafsi hautolewi tu kutoka kwa ukaguzi wa ndani. Kwa mujibu wa brown, kuna vyanzo vitano vinavyochangia hifadhi ya kujijua.
Vyanzo hivyo ni kama :ulimwengu wa kimwili, ulinganisho wa kijamii, tathmini iliyoakisiwa, kuchunguza na kujiona.
Hatua ya kuchukua, kujijua ni kitu muhimu katika maisha yetu kama wanadamu, ni wajibu wetu kujua kwa nini tunafanya kile tunachofanya.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
-
Usiangalie upande mbaya pekee.
“Things go wrong occasionally, but when you focus on that, you miss the enormity of what goes right.” Loretta Graziano Breuning.
Ni kawaida yetu sisi binadamu kuangalia upande mbaya wa jambo lolote lile. Kama huamini basi fungua TV, radio au gazeti linaloripoti habari. Kama habari mpasuko sana sana wanahabari wanaweka vipaumbele habari hasi.
Kama kwa siku kuna mammilioni ya magari yanayofanya safari zake, lakini katika mammilioni ya magari yanayofanya safari zake, kuna magari kumi labda huenda yatapata ajali.
Tutakazana kuangalia magari hayo kumi yaliyopata ajali na kusahau mamilioni ya magari ambayo yamekamilisha safari zake salama bila ya ajali. Kuangalia upande baya wa kitu ilikuwa na manufaa kwetu sisi binadamu kipindi ambacho maisha yetu wanadamu yalikuwa magumu na usalama ilikuwa ndogo.
Kipindi ambacho hatari ya kuliwa na wanyama wakali ilikuwa kubwa, mara zote ilibidi uangalie dalili za mambo kuwa mabaya. Lakini zama tunazoishi sasa, hatari kama hizo ni ndogo sana, lakini akili zetu bado zinafanya kazi kama zilivyorithi kwa watangulizi wetu walioishi kwenye hatari hizo.
Hivyo tunapaswa kutengeneza upya akili zetu, badala ya kuangalia upande mbaya pekee, tuangalie hali nzima na tutaona mengi mazuri.
Mambo mabaya lazima yatokee, lakini kama utapeleka fikra zako zote kwenye upande mbaya wa mambo, utakosa mengi mazuri ambayo yanaendelea kwenye maisha yako.
Ni katika kila baya linalotokea, ndipo kuna zuri ambalo linaambatana na baya hilo. Ukiangalia utapata kuona.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
-
Njia 10 za kutengeneza tabia za furaha.
Kila ambaye amekuwa anaanza kufanya kitu chochote kwenye maisha yake kwa lengo la kupata furaha amekuwa anaishia kujisikia vibaya baada ya kupata alichofikiri akipata kitampa furaha.
Wengi wetu tunapokutana na hali hii huwa tunafikiri kuna shida kwenye kile tunachopata. Lakini ukweli ni kwamba shida haipo kwenye chochote tunachotaka, bali shida ipo ndani yetu.
Furaha ya kweli kwenye maisha huanza ndani, ni kitu kinachoanzia kwenye fikra zetu na siyo matokeo ya kile tunachopata. Hata kama tumepata kitu kikubwa na muhimu kiasi gani, furaha yake huwa ni ya muda mfupi tu, baada ya hapo tunarudi kwenye hali yetu ya kawaida.
Kutoka kwenye kitabu cha “habits of a happy brain,”Loretta Graziano Breuning anatushirikisha njia kumi za kutusaidia kutengeneza tabia za furaha kwenye bongo zetu.
Wote tunajua kwamba mabadiliko huwa yanakuwa magumu kwa sababu ya tabia. Tabia mpya huwa ni ngumu kujijengea, na tabia za zamani huwa ni ngumu kuzivunja. Bila ya kuwa na njia sahihi, zoezi la kutumia ubongo wetu kuzalisha furaha litakwama.
Moja, jifunze kwa wengine, angalia watu ambao wana tabia unazotaka kujijengea kisha jifunze wanafanya nini na wewe ufanye. Ukifanya kile ambacho wenye furaha wanafanya, na wewe utakuwa na furaha pia.
Mbili, tumia kemikali za furaha ambazo hutumii kwa sasa. Kila mtu kuna kemikali anazotumia sana na ambazo hatumii kabisa. Ili kutengeneza tabia za furaha, angalia ni kemikali zipi hutumii na anza kuzitumia. Kama umekuwa mtu wa kuweka malengo na kuyafikia, kazana pia kuboresha mahusiano yako na wengine na hilo litakupa furaha.
Tatu, tengeneza tabia mpya kwenye tabia za zamani ulizonazo sasa. Angalia kile kitu ambacho unapenda kukifanya sasa, kisha ona jinsi gani unaweza kukifanya na ile tabia unayotaka kujenga. Unapohisianisha vitu hivi viwili unaweza kujenga tabia bora kwako.
Nne, nguvu. Kujenga tabia yoyote kunahitaji nguvu, hivyo panga kufanya kile unachofanya ili kujenga tabia mpya unapokuwa na nguvu. Asubuhi na mapema ni muda mzuri wa kufanya yale yanayojenga tabia mpya.
Tano, sifa. Unapofanya kitu kwa ajili ya sifa yako ya baadaye inakuwa rahisi kwa kitu hicho kuwa tabia. Pale unapofikiria kuacha alama fulani hata baada ya kuondoka, unasukumwa kufanya zaidi.
Sita, burudani. Fanya zoezi la kujenga tabia mpya kuwa burudani kwako. Usifanye kama ni jukumu zito na linalochosha, badala yake fanya kuwa burudani na itakuwa rahisi kwako kuendelea nalo.
Saba, vunja jukumu kubwa kwenye majukumu madogo madogo, na unavyokamilisha sehemu ndogo ya jukumu unapata hamasa ya kuendelea na jukumu sehemu nyingine. Kwa kugawa majukumu madogo madogo haikuchoshi wala kukukatisha tamaa.
Nane, fanya inayoridhisha badala ya kutaka kufanya iliyo kamili. Badala ya kusubiri mpaka uweze kuchukua hatua iliyo kamili na sahihi zaidi, chukua hatua inayoridhisha. Unapoona nafasi ya kuchukua hatua, hata kama haijakamilika, ni bora kuliko kusubiri mpaka upate ukamilifu ambao haupo.
Tisa, anza maandalizi mapema. Unapojua kuna tabia unataka kujijengea, anza maandalizi yake mapema kabla ya kufika wakati unaohitaji.
Kumi, tengeneza taswira ya kuwa na ile tabia unayotaka kutengeneza. Kwa kutengeneza taswira ya aina hiyo, njia zako kwenye ubongo zinazotengeneza tabia zinaimarika hata bila ya kufanya tabia husika. Hii limedhibitishwa na tafiti kwenye michezo, wachezaji ambao wanatengeneza taswira wakiwa wanacheza vizuri wanaimarisha uchezaji wao hata kama hawajacheza.
Hatua ya kuchukua, rafiki, tutumie njia hizi kumi katika kujijengea tabia za furaha ambazo zitadumu kwenye maisha yetu. Tuiaje kukimbilia njia za kupata furaha kwa haraka na pia furaha hizo huishia kuwa huzuni baadae.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
-
Kile kinachodhihirisha thamani yetu.
Binadamu tunaweza kusema tutakavyo, lakini watu huamini zaidi kile tunachofanya. Maneno ni rahisi, kila mtu anaweza kusema atakavyo. Lakini matendo ni magumu na hayo ndiyo yanadhihirisha kweli mtu anasimama wapi.
Kama kwa kweli kitu ni muhimu kwako utakifanya, hutaishi tu kusema. Kama unakitaka kitu kweli utafanya kila namna mpaka ukipate, hautakubali kuzuiwa na chochote. Hivyo una angalia yale unayofanya, hayo ndiyo yanaonyesha nini unajali zaidi.
Na hata kwa wengine, usisikilize sana wanasema nini, bali wewe angalia wanafanya nini. Kama meneno na matendo ya mtu vinatofautiana, amini zaidi matendo kuliko maneno.
Hatua ya kuchukua, ikiwa una mipango mazuri unapanga kila mwaka kuyafanya na hufanyi, jua hutaki kufanya, maana kama ungetaka ungekuwa umeanza kufanyia kazi.
Kuchukua hatua ya kufanyia kazi ndoto na malengo yetu kama binadamu, ndio inadhihirisha thamani yetu na viumbe wengine kama wanyama.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
-
Njia 10 za kufanya watu wakukubali na kuwa karibu na wewe.
Hitaji Kubwa la asili ya binadamu ni kukubalika na watu. Kwenye kitabu cha the power of positive thinking Dr Vicent Norman Peale, ametushirikisha njia kumi za kufanya watu watukubali na wawe karibu na sisi.
Hatua ya kwanza ni kujifunza kukumbuka majina ya watu uliowahi kukutana nao. Kumwita mtu kwa jina lake linamfanya ajiskie anajaaliwa sana na kufurahia kuongea na wewe.
Hatua ya pili kuwa mtu mzuri na mtulivu, binadamu tunapenda utulivu na amani, kwa sababu ni ufunguo wa maisha ukiwa mtulivu utawavuta wengi wapende kuwa karibu na wewe.
Hatua ya tatu kuwa mtu wa kufurahia kukutana na watu, kuwa uso wa tabasamu na kutokuchukia mtu yeyote yule, watu watapenda kukimbilia kwako.
Hatua ya nne usiwe mbinafsi, jilinde kwa kutoa hisia kwa vitu vyote unavyovifahamu. Kuwa halisi na mnyenyekevu siku zote.
Hatua ya tano jifunze kuwa mtu wa kuvutiwa ili watu wapendezwe kuwa karibu na wewe na kupata msisimko wa kufanya muunganiko kwako.
Hatua ya sita jifunze uwe mtu wa kwanza kuona kitu cha kipekee kwa watu. Hata kwa vile ambavyo huvifahamu.
Hatua ya sapa jaribu kujiponya wewe mwenyewe, migogoro yote unayopitia kwenye maisha usiweke wazi kila mtu aujue. Jaribu kuondoa manung’uniko kwenye maongezi yako na jiponye kupitia maombi.
Hatua ya nane jifunze kuwakubali watu mpaka pale utakapokuwa unafanya kwa uhalisia. Kutana na watu unaowakubali siku zote.
Hatua ya tisa usisite kusema neno la pongezi kwa mtu yeyote aliyepiga hatua fulani na kutoa pole kwa mtu mwenye huzuni au matatizo, vile vile kushukuru unapotendewa wema.
Hatua ya kumi kuwa na imani thabiti ya kiroho ;utakuwa na kitu cha kuwapatia watu, ambacho kitawafanya watu hao wawe imara na kuyafanya maisha yao kuwa na ufanisi.
Hatua ya kuchukua, kwa vile tumezifahamu njia hizi muhimu zaidi ni kuweka kwenye matendo sisi wenyewe kabla ya kukubaliwa na watu. Kuwatia watu nguvu ni kitu bora zaidi kwenye maisha.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.
-
Njia 10 ya kupumzika kwa ajili ya kupata nguvu zaidi.
Utafiti ulifanywa kwamba idadi kubwa ya kesi ya watu wenye vidonda vya tumbo, nusu ya wao waliugua siyo kwa sababu za kiumbo bali ni kwa sababu wagonjwa walikuwa na hofu kupitiliza, chuki na wasiwasi uliopitiliza.
Kwa kukaa kwenye mwanga wa jua na kufikiri maajabu ya Mungu na uwezo wake utakufanya upate nguvu ya ajabu katika akili yako na utakufanya uishi maisha toshelevu yasiyo na wasiwasi na hofu kupitiliza.
Kutoka kwenye kitabu cha the power of positive thinking na Dr Vicent Norman Peale. Norman anatushirikisha njia ambazo zitakufanya upumzike na kupata nguvu kubwa.
Njia ya kwanza ni kutojibebesha mzigo wa vitu vingi na kuwa bize kupita kiasi.
Njia ya pili ni ipende kazi yako, usibadili kazi yako badala yake jibadili wewe mwenyewe na kazi yako itakuwa ya tofauti.
Njia ya tatu ni itengeneze mpango wa kazi yako. Ukiwa hauna mfumo, kazi yako haitakuwa na mwelekeo.
Njia ya nne usijaribu kufanya kila kitu kwa mara moja. Kuwa na utaratibu unaokuongoza.
Njia ya tano jijengee mtazamo sahihi kwamba ugumu au wepesi wa kazi yako inategemea na wewe jinsi unavyoifikiria. Ukifikiri kwamba ni ngumu, utafanya iwe ngumu. Ukifikiri kwamba ni rahisi, utaifanya iwe rahisi.
Njia ya sita kuwa mwenye ufanisi kwenye kazi yako, maarifa ni nguvu. Ni rahisi kufanya kitu kwa usahihi ukitumia maarifa.
Njia ya sapa jipe muda wa kupumzika, unapopumzika unaupa mwili wako muda wa kujenga nguvu mpya na kubwa ambayo itakusaidia ufanye kazi kwa ufanisi kubwa.
Njia ya nane jifunze kutoghairisha, kitu kinachoweza kufanyika leo, kifanye leo. Mlundikano wa kazi nyingi zilizoachwa hufanya kazi kuwa ngumu. Weka kazi zako katika ratiba.
Njia ya tisa iombee kazi yako, itakufanya uwe mwepesi na kuifanya kwa ufanisi.
Njia ya kumi iweke Mungu kama rafiki yako asiyeonekana lakini ni mwaminifu kwa maana hiyo anapatikana kila mahali katika kazi zako.
Hatua ya kuchukua tuiweke njia hizi kumi katika matendo na tutafanya kazi zetu kwa ufanisi zaidi.
Akujaliaye zaidi.
Maureen Kemei.
-
Jinsi maisha yalivyo mzunguko.
Kwenye maisha ya kila siku, unaweza kuhangaika kutafuta kitu, halafu mwisho wa siku unarudi pale pale ulipoanzia, tena ukiwa vibaya zaidi kuliko ulivyoanza.
Hasa kwenye zama hizi ambapo maendeleo makubwa yanaendelea kutokea kwenye teknolojia na pia yameleta usumbufu mkubwa sana.
Hivyo basi, limesababisha watu wengi kukimbizana na mambo mengi yasiyokuwa na mchango yoyote kwenye maisha yao. Mwisho wa siku watu hujikuta wanachoka bila kukamilisha chochote cha maana na hivyo kurudi pale pale walipoanzia, huku wakiwa wamepoteza zaidi.
Wengi wamejipata wanajisahau, wanasahau malengo yao na kuanza kuiga wengine kwenye mtandao na pia kushindana kwenye mambo yasiyokuwa na tija kwenye maisha yao.
Kwa hivyo, Kuna umuhimu wa kuwa makini na chochote unachokimbizana nacho, mara nyingi unaishia kurudi pale ulipoanzia, huku ukiwa umepotea zaidi.
Hatua ya kuchukua, hakikisha kwenye safari yako ya kutafuta chochote, hujisahau na kupotea. Badala yake unajifahamu zaidi, kuweka malengo na juhudi ili kuyafikia.
Kamwe tusiache kusikiliza sauti yetu ya ndani, maana hiyo ikinyamaza tunakuwa tumekufa kibinafsi ila kimwili tunaendelea kuwepo na hapo mwili utaumizwa zaidi na kila aina ya anasa.
Akujaliaye sana.
Maureen Kemei.