Home

  • Njia za watu wenye nguvu ya akili huzuia kujihurumia kuharibu mafanikio yao.

    Rafiki yangu, kuwa mtu wa kujihurumia mara zote kunaweza kuwa unajiharibu kabisa. Hufanya kushinda changamoto na magumu ya maisha kuwa ngumu zaidi. Inakufanya uone haiwezekani na pia kukufanya uendelee kukwama.

    Watu wenye nguvu za kiakili wanakataa kuruhusu kujihurumia kuharibu mafanikio yao. Badala yake, wanatumia ugumu wa maisha usioepukika kama njia ya kuimarika na kuwa bora zaidi.

    Yafuatavyo ndivyo watu wenye nguvu kiakili huepuka mtego wa kujihurumia.

    Njia ya kwanza: wanakabiliana na hisia zao. Watu wenye nguvu kiakili hujiruhusu kupata hisia kama huzuni, kukatishwa tamaa au upweke. Hawajisumbui wenyewe kutoka kwenye hisia hizi kwani wanajihoji kama matatizo hayo ni ya haki au kwa kujihakikishia kuwa wameteseka zaidi kuliko wale wa karibu nao. Wanajua njia bora ya kukabiliana na usumbufu ni kupitia tu.

    Njia ya pili :wanahoji maoni yao. Hali yetu ya kuhisia huathiri jinsi tunavyoona ukweli. Unapojihurumia, Kuna uwekezekano wa kuzingatia mambo mabaya yanayoendelea katika maisha yako, huku ukipuuza mazuri. Watu wenye nguvu ya akili huhoji kama mawazo yao yanawakilisha ukweli.

    Njia ya tatu: wanahifadhi rasilimali zao kwa shughuli za uzalishaji. Kila dakika unayotumia kuandaa karamu yako mwenyewe ya huruma ni sekunde 60 unachelewesha kushughulikia suluhisho.

    Watu wenye nguvu kiakili hukataa kupoteza wakati wao wa thamani na nishati kwa kukaa juu ya taabu zao. Badala yake, wanatoa rasilimali zao za kikomo kwa shughuli za uzalishaji ambazo zinaweza kuboresha hali zao.

    Njia ya nne : wanajizoeza kushukuru. Haiwezekani kujisikia huruma na shukrani kwa wakati mmoja. Wakati kujihurumia ni juu ya kufikiria, “Ninastahili bora,” inajumuisha kutafuta shukrani juu ya kufikiria, ” Nina zaidi ya ninayohitaji.” watu wenye nguvuĀ  kiakili wanatambua yote wanayopaswa kushukuru maishani, hadi kwenye hewa Safi ya kupumua na maji Safi ya kunywa.

    Njia ya tano :wanasaidia wengine. Ni vigumu kujihurumia unaposaidia wale ambao hawana bahati. Matatizo kama vile kudai wateja au kupungua kwa mauzo hayaonekani kuwa mabaya sana unapokumbushwa kuwa kuna watu ambao wanaikosa chakula na makazi. Badala ya kuchungulia kero zao wenyewe, watu wenye wenye nguvu kiakili hujitahidi kuboresha maisha ya wengine.

    Njia ya sita : wanadumisha mtazamo wa matumaini. Baadhi ya matatizo ya maisha hayawezi kutatuliwa wala kuzuiwa. Misiba ya asili, matatizo ya magonjwa na ya kiafya na matatizo mengine ambayo watu wanakabiliana nayo kwenye maisha. Watu wenye nguvu kiakili huweka mtazamo mzuri juu ya uwezo wao wa kushughulikia chochote.

    Njia ya sapa : wanakataa kulalamika. Kuzungumza na watu wengine kuhusu ukubwa wa matatizo yako huchochea hisia za kujihurumia. Watu wenye nguvu kiakili hawajaribu kupata huruma kutoka kwa wengine kwa kulalamika juu ya hali zao ngumu. Badala yake, wanachukua hatua hili kufanya mambo kuwa bora, au wanakubali hali ambazo hawawezi kubadilisha.

    Hatua ya kuchukua : kila mtu ana nguvu ya akili. Kwa kukuza uwezo ulioongezeka wa kudhibiti mawazo yako, kudhibiti hisia zako na kuishi kwa matokeo licha ya hali zako, utakua na nguvu na kuwa bora.

    Mimi wako akujaliaye.

    Maureen Kemei.

  • Umuhimu wa kuwa na subira.

    Mambo mazuri huwa hayataki haraka, hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mafanikio kama unataka mafanikio makubwa, lazima uwe na subira.

    Wengi wetu tunashindwa kwenye hii safari kwa sababu tuna haraka ya kupata mafanikio, hasa vijana wa kisasa wengi wetu tunataka kumaliza shule leo, kuajiriwa na kupata bosi mzuri leo, kazi kusiwe na changamoto yoyote, tujenge nyumba nzuri leo na tuolewe au kuoa na ndoa kusiwe na changamoto yoyote.

    Matarajio haya hayawezekani, lazima changamoto, maumivu na magumu katika maisha ya mwanadamu yatokee. Lazima tujifunze namna ya kuwa na subira kwa kile tunachofanya au tunachopitia.

    Mtu yeyote anayejua kile anachotaka, na ambaye yuko tayari kuweka kazi kukipata, ni swala la muda tu, akiwa na subira, ung”ang”anizi na uvumilivu,lazima atapata anachotaka.

    Kitu muhimu tunachopaswa kujua ni kwamba, mambo huwa yanatokea kwa wakati wake yenyewe, siyo kwa wakati tunaopanga wenyewe. Chochote tunachotaka tutakipata kwa wakati wake, lakini haitakuwa wakati tunaopanga sisi.

    Hivyo tusione tunachelewa kupata tunachotaka na kukata tamaa, kuwa na subira, tuendelee kukaa kwenye mchakato na wakati sahihi utakapofika, tutapata tunachotaka.

    Ili tuweze kuwa na subira, tunapaswa kuacha kuhesabu na kufanya sehemu yetu. Tuweke mkazo kwenye mchakato na siyo matokeo au muda ambao tumeweka juhudi. Kadiri mchakato na muda unavyokwenda, ndivyo tunavyojiweka kwenye nafasi nzuri ya kupata kile tunachotaka.

    Kila mtu anataka kupata utajiri wa haraka na kwa njia za mkato, lakini dunia huwa ina namna yake sahihi ya kukamilisha mambo, huwezi kuilazimisha bila ya kuleta madhara. Ni lazima uweke juhudi na muda ndiyo dunia ifike hatua ya kukupa kile unachotaka.

    Na kama ambavyo tumeshaona, lazima tuwe na ujuzi maalumu na tujijengee jina na sifa nzuri. Lazima tuwe bora kabisa kwenye kile tunachokifanya, tuweke juhudi na kujipa muda na mwisho tutapata matokeo makubwa.

    Hatua ya kuchukua, penda unachofanya na ukifanye kwa sababu unakipenda. Hilo litakufanya uwe na subira na uendelea kufanya, bila kuangalia muda au matokeo.

    Wako akujaliaye sana.

    Maureen Kemei.

  • Silaha kuu ya washindi.

    Kila mmoja huwa ana nyakati za furaha na huzuni. Kila mtu huwa ana matatizo mbalimbali, yanaweza kuwa ya fedha, kazi, biashara, familia, mahusiano na mengine mengi.

    Watu wengi hutumia matatizo wanayokutana nayo kwenye maisha kama sehemu ya kulaumu, kulalamika na kutafuta huruma kutoka kwa wengine. Huwa tayari kuwaambia wengine matatizo yao kwa kuona kama ndiyo matatizo makubwa kuliko ya wengine wote.

    Kufanya hivyo siyo sahihi kwa sababu kubwa mbili. Moja ni kila mtu ana matatizo yake na ya wengine yanaweza kuwa makubwa kuliko ya kwako. Na mbili ni matatizo yako ni yako, hayawahusu wengine, hakuna anayejali sana kuhusu matatizo yako.

    Joe Girard anatushirikisha kwenye kitabu chake cha “Girard’s 13 essential rules of selling,” kwamba kitu pekee kitakachoweza kukuvusha kwenye nyakati unazopitia magumu na matatizo mbalimbali ni kuwa na mtazamo chanya.

    Ni wakati huo wa magumu ndiyo unapaswa kuwa imara sana kwani ndiyo wakati rahisi kwa mtu kuyumba na kuanguka. Wakati mambo ni mazuri kila mtu anaweza kufanya vizuri, ni nyakati ngumu ndizo wengi wanashindwa.

    Kuwa na mtazamo chanya wakati unapitia magumu ni muhimu kwa sababu Kuna wakati utakuwa na wasiwasi na wewe mwenyewe. Kuna wakati utakuwa na mashaka na maamuzi uliyofanya, utaona kama unakosa. Hiyo ni hali ambayo ni lazima utaipitia kama binadamu. Kitu pekee kitakachokuwezesha kuendelea licha ya kukutana na hali hiyo ni mtazamo chanya unaokuwa nao.

    Mtazamo chanya ndiyo unaowatofautisha wale wanaofanikiwa na wanaoshindwa. Kufanikiwa kwenye maisha ni matokeo ya kuweza kukabiliana na nyakati ngumu na kuzivuka. Mtazamo chanya wa kifikra unakupa nguvu ya kuvuka chochote na kuendelea bila ya kukata tamaa. Hata kama hujapata matokeo unayoyataka, unapokuwa na mtazamo chanya unajua una wakati mwingine wa kufanya kwa ubora zaidi. Hukati tamaa kwa kuona ndiyo mwisho, bali unajua ni sehemu ya safari lazima iendelee.

    Hatua ya kuchukua, mara zote kuwa na mtazamo chanya na ya uwezekano. Fanya kila anayekutana na wewe ajue upo chanya, usiwe mtu wa kulaumu, kulalamika au kulia lia shida zako kwa wengine. Kwa kuonekana ukiwa chanya mara zote kunawafanya watu wakuamini na kushawishika na wewe.

    Yeyote unayemwona amefanikiwa, kuwa na uhakika kwamba safari yake halikuwa rahisi. Amepitia mengi magumu ambayo yalimkatisha tamaa. Kilichomwezesha yeye kufanikiwa ni kuwa na mtazamo chanya wa kiakili. Kama na wewe unataka kupata ushindi na mafanikio kwenye maisha yako, hakikisha unakuwa na mtazamo chanya wa kiakili mara zote.

    Kuwa na mtazamo chanya ni silaha ya wale wanaoshinda matatizo na magumu kama ambavyo tumejifunza. Uwe na simu njema.

    Mimi wako akujaliaye sana.

    Maureen Kemei.

  • Mambo yanayotengeneza furaha ya ndani.

    Rafiki, kutoka kwenye kitabu cha “the dedicated,” kilichoandikwa na Pete Davis, tunapata kujifunza mambo matatu yanayojenga furaha ya ndani, furaha ya kudumu.

    Cha kwanza kabisa ni uhuru binafsi au kwa kizungu inaitwa autonomy. Uhuru wa kuweza kujitawala sisi wenyewe na kuchagua namna tunayoishi maisha yetu.

    Cha pili ni ubobezi au competence kwa kizungu. Hii ni uwezo wa kufanya kitu chenye manufaa makubwa kwa wengine. Tunajiona wa thamani pale wengine wanapotutegemea kwenye kitu fulani tunachokifanya, pale tunapopewa sifa na hadhi kwa yale tunayofanya.

    Cha tatu ni kuwa sehemu ya jamii au community, ambayo inatujua, kutujali na kutusukuma kufanya makubwa zaidi. Ni jamii ndiyo inafanya maisha yetu yawe na maana kupitia yale tunayofanya na ushirikiano tunaokuwa nao.

    Muhimu, mambo hayo ndiyo yaliyotengeneza furaha ya ndani, furaha ambayo inadumu kwa muda mrefu. Yalikuwa yakijengwa na kuthaminiwa zaidi na jamii za asili.

    Lakini jamii za kisasa zimehama kutoka mambo ya ndani na kwenda kwenye mambo ya nje katika kutafuta furaha.

    Hatua ya kuchukua, ni muhimu tuzingatie haya mambo matatu muhimu katika kutafuta furaha ya ndani inayodumu, kuliko kukimbizana na mambo ya nje yanayoleta furaha ya muda mfupi.

    Akujaliaye sana.

    Maureen Kemei.

  • Kutokujilinganisha na wengine.

    Hakuna kitu kinachowaangusha wengi kama kujilinganisha na wengine. Kwa sababu haijalishi umepiga hatua kiasi gani, Kuna mtu mwingine ambaye amepiga hatua zaidi yako.

    Ukianza kujilinganisha na watu, utaingiwa na wivu kwa kuona wamekuzidi na hilo litaathiri mahusiano yako na watu hao.

    Sisi binadamu huwa hatuwezi kuficha hisia zetu, hivyo hisia zozote ulizonazo kwa wengine huwa zinajiweka wazi unapokuwa nao. Hivyo hata kama utaficha kiasi gani bado watu watajua hisia ulizonazo juu yao.

    Kuepuka hilo, acha kujilinganisha na yeyote, mpende na kumheshimu kila mtu ukijua kila mtu yuko kwenye njia yake ya maisha.

    Muhimu zaidi usiwachukie wale waliofanikiwa kuliko wewe. Kwenye jamii nyingi matajiri wamekuwa wakipewa majina mabaya na kuonekana ni watu wabaya, hakikisha huingii kwenye mkumbo huo.

    Ukiwachukia matajiri kamwe huwezi kuwa tajiri, hivyo wapende wale waliofanikiwa kuliko wewe, wapende kweli kutoka ndani yako na hilo litakufanya uwe tayari kujifunza kutoka kwao na wewe uweze kufanikiwa pia.

    Hatua ya kuchukua ;ondokokana kabisa na fikra na hisia zozote hasi, hizo ni kikwazo kwako kufanikiwa. Mara zote kuwa na hisia na fikra chanya ambazo zitakusukuma kufanikiwa zaidi.

    Akujaliaye sana.

    Maureen Kemei.

  • Mchujaji bora wa mawazo.

    Rafiki, ni rahisi kuona waliofanikiwa kwenye kazi zao kama wana njia ya kupata mawazo bora kuliko wengine.

    Unaweza kuona kama wao wana namna ya tofauti ya kupata mawazo ambayo wakiyafanyia kazi yanafanikiwa sana.

    Ukweli ni kwamba watu wote huwa tunapata mawazo yanayofanana, mawazo mengi yako kwenye yale tunayofanya.

    Kinachowatofautisha waliofanikiwa ni uwezo wao wa kuyachuja mawazo wanayopata na kujua yapi yana uwezo wa kuleta matokeo makubwa.

    Wakati wasiofanikiwa wakihangaika na kila wazo wanalopata, wakijaribu mengi na wasipige hatua.

    Wanaofanikiwa wanachuja mawazo hayo, wanaachana na mengi yasiyo sahihi na kufanyia kazi machache sahihi.

    Hatua ya kuchukua ; rafiki, na wewe pia unaweza kujifunza na kuwa mchujaji bora wa mawazo unayopata ili kufanyia kazi yale yaliyo sahihi.

    Unachohitaji rafiki yangu, ni kujua vizuri kile unachofanya na kuyasikiliza machale yako pia.

    Akujaliaye sana.

    Maureen Kemei

    Blog:kufikirichanya.wordpress.com

  • Sababu nzuri ya kusema hapana.

    Ili uweze kusema hapana kwenye mambo yasiyo sahihi, lazima uwe na mambo sahihi unayosema ndiyo.

    Lazima ndiyo yako iwe kubwa na muhimu kuliko hapana. Sema ndiyo kwenye mchakato unofanyia kazi na sema hapana kwa mengine yote ambayo hayasaidii mchakato huo.

    Ndiyo hapana zako zitawaumiza watu kwa muda mfupi, lakini zitawasaidia kwa muda mrefu kupitia kile unachofanya, ambapo kwa kusema hapana kwenye mengine utakifanya kwa ubora sana.

    Lazima pia kuwe na kiasi kwenye hapana zako, maana iwapo utasema hapana kwa kila kitu, itakuwa ni njia nyingine ya kujificha au unaweza kuwapoteza wale muhimu unaowahitaji sana kwenye kile unachofanya.

    Ukisema ndiyo kwenye mambo mengi nalo unakosa muda wa umakini wa kutosha kwenye kile muhimu unachofanya.

    Hatua ya kuchukua ; weka vipaumbele vyako kwa usahihi, Sema ndiyo kwa yanayohusiana na vipaumbele vyako na hapana kwa yasiyohusiana.

    Usiogope kuwaumiza watu kwa muda mfupi kwa hapana zako, kwani baadaye watanufaika na matokeo utakayozalisha.

    Akujaliaye sana.

    Maureen Kemei.

  • Vipi kama?

    Pale unapotaka kupata kitu lakini unakutana na magumu, pale ambapo watu wanakukatalia na kukuambia haiwezekani, tena wakiwa na ushahidi, pale unapochukua hatua na kushindwa, ni wakati rahisi sana kwako kukata tamaa na kuamua kuacha.

    Lakini huu ni wakati mzuri kwako kujiuliza swali hili muhimu sana ;vipi kama?

    Vipi kama kila unachotaka kinawezekana ila tu hujajua njia bora ya kufanya? Hapa utapata msukumo wa kujifunza zaidi.

    Vipi kama wale wanaokuambia ni kwa sababu hawajawahi kujaribu? Hapa utapata msukumo wa kujaribu.

    Vipi kama njia unayotumia siyo sahihi? Hapa utachukua njia ya tofauti.

    Hatua ya kuchukua, jiulize swali vipiĀ  kama ili uweze kujaribu vitu vipya na utaweza kufanikiwa.

    Akujaliaye sana.

    Maureen Kemei.

  • Vitu ambavyo huwezi kuharakisha.

    Hitaji letu la kuharakisha kila kitu limekuwa kikwazo kwenye mambo mengi kwa sababu hatukubali ukomo tulionao.

    Tunaamini kwa sababu teknolojia inaharakisha viti vingi, basi kila kitu kinaweza kuharakishwa.

    Lakini kuna vitu vingi kwenye maisha ambavyo hakuna namna unaweza kuviharakisha, hata ufanyeje.

    Kutoka kwenye kitabu cha four thousand weeks na Oliver Burkeman. Anatushirikisha vitu ambavyo hatuwezi kuharakisha kwenye maisha.

    Moja ya vitu hivyo :ni usomaji wa vitabu. Watu wamekuwa wanalalamika kwamba hawana muda wa kusoma vitabu. Lakini watu hao wanatumia muda mwingi kwenye mitandao na mambo mengine.

    Ambacho hawataki kukubali watu hao ni kwamba hakuna namna unaweza kuharakisha usomaji. Unaweza kuharakisha kuperuzi mitandao ya kijamii, kwa kupita haraka haraka kwa kasi kubwa.

    Lakini huwezi kuharakisha usomaji wa kitabu na ukatoka ukiwa umeelewa vizuri ulichosoma. Unahitajika kutenga muda wa kutosha na wa kusimama na kusoma kwa umakini na utulivu mkubwa. Kitu ambacho ni adimu sana kwenye zama hizi za kasi ya teknolojia na kukosa subira.

    Kusoma kitu kwa namna ambayo utakielewa na kunufaika nacho kunahitaji muda wa kutosha na hakuna namna ya kuharakisha hilo.

    Watu wamekuwa wakijaribu usomaji wa kasi, lakini uelewa umekuwa ni ndogo. Pia watu wamekuwa wakijaribu kusikiliza vitabu vilivyosomwa, nako pia uelewa unakuwa mdogo.

    Katika kuendeleza ukosefu wa subira na kutaka kuharakisha vitu, watu wamekuwa wanasikiliza vitabu vilivyosomwa kwa kasi mara mbili ya kawaida. Hapo wanaona wanajifunza mengi kwa muda mchache,lakini ni kujidanganya tu, kwani uelewa kwao unakuwa ni mdogo sana kwenye kasi ya aina hiyo.

    Hatua ya kuchukua, kwa kukubali kwamba tumenaswa kwenye uraibu wa kufanya mambo kwa kasi, ambayo haileti utija kwenye maisha yetu, yatatusaidia tuchukue hatua ya kutenga muda wa kutosha na wenye utulivu wakati wa kusoma au kufanya jambo muhimu.

    Akujaliaye sana.

    Maureen Kemei

  • Tawala mazingira yako.

    Akili yako ni kitu cha kushangaza sana. Akili kama ikiwa inafanya kazi kwenye njia moja utapata mafanikio makubwa, lakini kama ikiwa inafanya kazi kwenye njia tofauti tofauti itakusababishia kushindwa katika maisha.

    Akili ni sawa na kitu kinachoweza kuharibika kwa urahisi sana na ni kama kifaa chenye utambuzi wa haraka sana.

    Akili yako inatambulisha au kuwakilisha aina ya chakula kinachokula, na mwili wako vile vile kinatambulisha aina ya chakula kinachokula kutoka kwako.

    Kwa hivyo wewe ni zao la mazingira yako unayoishi au uliyokulia. Mazingira yanatutengeneza yanatuelekeza nini cha kufanya.

    Kitu muhimu ni kwamba kiwango cha uelewa wako, mipango yako, akili yako na utu wako vimetengenezwa na mazingira unayoishi.

    Tunapojihusisha na watu wenye mtazamo hasi na sisi tunakuwa hasi pia, na tunapojihusisha na watu wenye mtazamo chanya na sisi tunakuwa chanya vilevile.

    Hatua ya kuchukua:Jitengenezee mwenyewe mazingira ya kuweza kufanikiwa. Boresha mazingira mazuri ya kiakili na kiafya.

    Kutoka kwa mimi ninayekujali sana.

    Maureen Kemei.