-
Kundi 2 ya watu unayopaswa kuwaepuka.
Rafiki yangu mpendwa pamoja na vikwazo na changamoto ambazo unakutana nazo kwenye safari ya mafanikio, ipo pia changamoto kubwa ya watu wanaotuzuia tusifanikiwe.
Kundi la kwanza ni wale wanazoweka wazi kabisa kuwa wanatupinga na kufanya lolote lile hili tu kutuzuia tusifanikiwe. Hawa wanatukatisha tamaa, kutuhujumu au kujaribu kutuzuia tusichukue hatua. Watu hawa ni rahisi kuwaona na kuwajua na hivyo tunaweza kuwakwepa.
Kundi la pili ni wale ambao hawaonekani wazi kama wanatuzuia. Hawa ni watu ambao wanaofanya mambo yao, wala hata hawatupingi au kutuzuia tusifanye yetu. Ni wale watu wa karibu sana kwetu tunayofanya nao kazi na biashara zetu na hata tunaokuwa nao karibu muda mwingi. Watu hawa hawafanyi chochote kuonesha kwamba wanatupinga, ila uwepo wao kwenye maisha yetu ndiyo unakuwa na madhara kwetu.
Watu hawa wa karibu yako hawatumii nguvu kubwa kukuzuia, bali wao wanaishi maisha yao, na wewe unajikuta unashawishika kuishi maisha ya ngazi zile zile. Na hapo utapata matokeo sawa na wao wanavyopata . Kama unabisha hili, jaribu kuwaangalia wale watu wa karibu sana kwako, na uone kama mna tofautiana sana.
Hivyo rafiki, jukumu lako kubwa ni kuangalia watu gani wanaokuzunguka, watu gani ambao unatumia nao muda mwingi. Angalia wanaenda wapi, maana huko ndiyo na wewe utaenda. Pia angalia wanafanyaje, maana ndivyo na wewe utafanya.
Rafiki yangu tunapaswa kuwa macho sana na watu hawa ambao ni kikwazo kikubwa lakini hawaonekani. Chunga sana ule mduara wako wa ndani, yaani wale watu wa karibu sana kwako, wana athari kubwa kwenye maisha yako.
Kuchukua hatua; rafiki yangu chagua watu sahihi na kama huwapati basi tengeneza watu sahihi.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Namna ya kujijengea ujasiri mkubwa.
Rafiki yangu mpendwa kutoka kwenye kitabu cha ‘the everyday manifesto,’ Robin anatushirikisha hadithi ya Niki Lauda, mshiriki wa mbio za magari ambaye alipata ajali mbaya kwenye mashindano na kuungua kichwa na uso.
Alipelekwa hospitali akiwa taabani na kila mtu alijua hawezi kupona.
Lakini siku 40 baadaye alirudi kwenye mbio za magari, kabla hata hajapona vizuri.
Alipoulizwa alieleza kilichomwezesha kupona ni alikataza akili yake kupumzika, kwani alikuwa kwa hali aliyokuwa nayo, angeruhusu akili ipumzuke kingekuwa kifo.
Na pia alieleza baada ya kuona amepata nafuu, alichagua kurudi kwenye mbio za magari kwa sababu ndiyo kitu muhimu zaidi kwake.
Kupitia hadithi hii Robin anatupa mafunzo matatu mkubwa.
Kwanza ni kujenga ujasiri, hakuna anayezaliwa akiwa jasiri, bali ujasiri hutengenezwa kadiri mtu anavyokabiliana na magumu. Hivyo unapokutana na magumu usilalamike wala kuyakimbia, bali yakabili na yatumie kujenga ujasiri.
Mbili ni rudi kwenye mwendo mapema. Unapokutana na magumu ambayo yanakutoa kwenye mwendo, hakikisha unarudi kwenye mwendo mapema iwezekanavyo .
Magumu hayo yanaweza kukujengea hofu ambayo itaendelea kukua kadiri utakavyokuwa nje ya mwendo. Kwa kurudi kwenye mwendo mapema, utavunja hofu hiyo na kuimarisha ujasiri wako.
Tatu ni usistaafu. Hata baada ya Niki Lauda, kustaafu mbio za magari, aliendelea na ujasiriamali kwenye sekta ya usafiri. Licha ya kuwa alikuwa ameshafika kwenye kilele, hakuona huo ndiyo mwisho, bali aliendelea kujisukuma zaidi.
Kuchukua hatua; rafiki yangu hivyo ndivyo tunavyopaswa kuwa pia, kutokukubali kustaafu baada ya kufika kileleni, badala yake kuendelea kujisukuma na kufanya makubwa zaidi.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Njia 4 za kubadili mtazamo kuhusu fedha na utajiri.
Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini fedha na utajiri ni kitu ambacho kimekuwa kinawachanganya wengi.
Kila mtu anataka kupata fedha na utajiri na kuweka kila juhudi ili kupata. Lakini ni wachache pekee wanofanikiwa kupata fedha na utajiri.
Kinachowatofautisha wanaopata na wanaokosa siyo juhudi wanazoweka, bali mtazamo wanaokuwa nao.
Kuna mtazamo ya aina nne ambayo unapaswa kuibadili Ili kupata fedha na utajiri mkubwa kwenye maisha yako.
Moja ni uhaba. Wengi wanachukulia fedha kwa uhaba, kwa kuona njia pekee ya kuzipata ni kuzikumbatia na kuzificha. Mtazamo huo unaifanya asili ione mtu hayupo tayari kupata zaidi na hivyo kumfanya asione fursa za kupata zaidi.
Ondokana na mtazamo wa uhaba na jijengee mtazamo wa utele. Ona fedha ziko tele na unaweza kupata nyingi uwezavyo. Hivyo huna haja ya kuficha au kukumbatia fedha ulizonazo, badala yake unapaswa kuzizungusha ili zizalishe zaidi na zaidi.
Mbili ni kufa na kupona. Wengi huchukulia fedha kama kitu cha kufa na kupona, kwamba kama wakizikosa basi ndiyo maisha yamefika mwisho.
Hii inawafanya waishi kwa hofu kubwa na hofu hiyo inawazuia wasione fursa nzuri za kupata fedha zaidi.
Ondoa mtazamo huo wa kufa kupona na jenga mtazamo wa fedha kuwa kama mchezo. Kwamba kupoteza mchezo mmoja sio kama kushindwa, kuna michezo mingi mbeleni.
Kukosa au kupoteza fedha haimaanishi ndiyo mwisho wa maisha yako, bali ni sehemu ya maisha, unapokuwa na utulivu na kufanya yaliyo sahihi, utapata fedha zaidi.
Tatu ni ushindani. Wengi Wana mtazamo wa ushindani, kwamba ili wao wapate lazima wengine wakose. Wanaishi kwa ulimwengu wa pata potea au jumla sifuri.
Wanaamini ili wao wapate lazima wengine wakose. Huo ni mtazamo ambao unawazuia watu wasione fursa nzuri za kutoa thamani zaidi na kupata fedha zaidi.
Rafiki yangu ondokana na mtazamo huo na jenga mtazamo wa ushirikiano, jua unaweza kupata fedha kwa kuwawezesha wengine kupata fedha pia.
Kwa kuongeza thamani kwa wengine, matokeo yanakuwa ni jumla chanya, wewe unapata na wengine pia wanapata. Kwa mtazamo huu, utaziona na kuzitumia fursa zaidi za kuongoza kipato chako.
Nne ni kuchukua. Wengi wana mtazamo wa kuchukua au kupewa zaidi kuliko wanavyotoa . Kwa chochote wanachofanya, wanajiangalia kwanza wao wananufaikaje na hawajali wanawanufaishaje wengine. Ndiyo maana watu wanakuwa tayari kushiriki kwenye rushwa na ufisadi, kwa sababu wanataka kupata zaidi ya wengine.
Lakini mtazamo huu huwa kikwazo kwao kupata zaidi na zaidi. Badili mtazamo huo na jenga mtazamo wa kutoa, mtazamo wa kujali maslahi ya wengine badala ya kujali maslahi yako tu.
Hatua ya kuchukua; Kwa kuangalia unawanufaishaje wengine, unaweza kutoa manufaa makubwa zaidi tu ambacho kitafanya ulipwe zaidi.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Njia ya kuboresha mawasiliano.
Rafiki yangu mpendwa kwa chochote kile unachofanya, unahitaji kuwashawishi watu wakubaliane na wewe.
Watu hao waone na kukubali maono makubwa uliyonayo na wawe tayari kuambatana na wewe katika kufikia maono hayo.
Hilo linakufanya wewe kuwa kiongozi na kiongozi bora ni yule anayefanya watu wachague kumfuata na siyo kuwalazimisha.
Njia pekee ya kuwafanya watu wachague kukufuata ni kuwa na ushawishi na ushawishi unatengenezwa na mawasiliano unayokuwa nayo kwa watu unaowalenga.
Maneno huwa yana nguvu kubwa sana, yakitumika kwa usahihi yanaleta matokeo makubwa na yakitumika vibaya yanaleta majanga makubwa.
Hapa kuna njia ya kuboresha mawasiliano yako, Ili uweze kuwa na ushawishi mkubwa na kutengeneza wafuasi wanaokuamini kwenye maono uliyonayo.
Moja ni kuwa msikilizaji mzuri. Kama wewe unaongea tu, huwezi kujifunza na huwezi kujua wengine wanataka nini. Unapaswa kuwa msikilizaji mzuri na makini.
Wengine wanapoongea, weka umakini wako wote katika kuwasikiliza ili kuelewa kile wanachosema, lakini pia kuelewa kile ambacho hawasemi kwa maneno bali kwa vitendo.
Kwa zama tunazoishi sasa ambapo hakuna mtu mwenye muda wa kumsikiliza mwingine, ukiwa msikilizaji siyo tu utajifunza mengi, bali utawavutia wengi kuja kwako.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@kemeimaureen
-
Umuhimu wa kusikiliza kwa umakini.
Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini tunapaswa kuwa msikilizaji makini.
Tunahitajika kusikiliza kwa makini sana pale mtu mwingine anapoongea.
Tunapaswa kuweka umakini wetu kwenye kusikiliza ambacho yule anayeongea anaona tunamjali kuhusu kile anachokielezea. Kwa yeye kuona unajali anafunguka kuelezea zaidi na zaidi
Atakuwa tayari kukuelezea hata mambo ambayo amekuwa anayaficha kwa sababu tu umeonyesha umakini.
Nguvu nyingine ya kusikiliza kwa umakini ni kuweza kumwelewa mtu kwa undani na kujua yale yaliyo muhimu zaidi kwake, ambayo utaweza kuyatumia kumshawishi.
Kwa kusikiliza kwa umakini na kuelewa, utaweza kumuuliza mtu maswali ambayo yatamfanya atoe ufafanuzi zaidi, kitu ambacho kitatupa fursa ya kumwelewa kwa undani zaidi.
Kusikiliza kwa umakini ni kumpa mtu nafasi ya kuchanua yale yaliyo ndani yake . Watu wengi wanatembea na mambo mengi yaliyojaa ndani yao ambayo yanawapa msongo mkubwa.
Kuchukua hatua; kwa kuwasikiliza kwa umakini, watu wanajikuta wakitoa yale yaliyowajaa ndani yao, kitu kinachowafanya wajiskie vizuri baada ya kuwa wameongea na wewe.
Katika hali hiyo ya kujiskia ndiyo wanakuwa rahisi kuwashawishi.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com
-
Kwa Nini Uhitaji Kufanya Kila Kitu.
Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini mtego mkubwa wa ufanisi ni pale mtu unapodhani unapaswa kufanya kila kinachokuja mbele yako, au kila ambacho watu wanataka ufanye.
Pata picha unaweza kuanza na nia nzuri kwamba umalize haraka majukumu madogo madogo yaliyo mbele yako ili upate muda kwa majukumu makubwa.
Lakini unapokuja kushtuka unagundua majukumu madogo madogo yanazidi kuongezeka, huku majukumu makubwa yakiwa yanazidi kuahirishwa.
Hivi ndivyo watu wengi wanavyoyapoteza maisha yao, kwa kujikuta muda umeenda sana lakini hakuna mkubwa waliyofanya.
Wanahangaika na mambo madogo madogo yanayokuja mbele yao, wakiamini watayamaliza, lakini hayaishi.
Chukua mfano wa mwandishi ambaye jukumu lake kuu ni kuandika. Lakini kwanza anaanza kwa kujibu barua pepe ambazo ametumiwa, akiamini anazimaliza ndiyo aanze kuandika.
Wakati anamaliza kujibu barua pepe, zile alizoanza kujibu zinakuwa zinajibiwa tena hivyo inabidi azijibu tena. Kinachotokea ni siku inakuwa imeisha, amechoka lakini jukumu kuu la uandishi halijafanyika.
Kabla hujafanya maamuzi, ni lazima ujue kwamba hata uwe na mbinu bora kiasi gani ya ufanisi, unapochagua kufanya kitu kimoja maana yake umechagua kutokufanya kitu kingine.
Rafiki yangu muda unaotenga kufanya kitu hiki ni muda ambao huwezi kuutumia kufanya kitu kile.
Kuchukua hatua; rafiki yangu bila ya kukubali hili na kupangilia vizuri yale ambayo mtu unafanya, ufanisi utazidi kukupoteza badala ya kukusaidia. Maana utafanya mengi sana, lakini yasiyo na tija.
Hakikisha kila siku unafanya kile chenye tija pekee na kuachana na kile kinachokuchosha na kukupotezea muda wako.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Njia 2 za kuyakabili magumu.
Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini wastoa wanatushirikisha njia kuu mbili tunazoweza kuzitumia kuyakabili magumu ili yasivuruge maisha yetu.
Njia ya kwanza ni kutambua wema pekee ndiyo kitu bora. Hapa ustoa unatukumbusha kurudi kwenye asili yetu binadamu ambayo ni viumbe wa kufikiri. Hivyo tunapaswa kuziweka fikra zetu vizuri na tusitawaliwe na hisia zozote mbaya.
Kwani kinachofanya mambo yaharibike wakati tunapitia magumu ni tunaporuhusu kutawaliwa na hasira.
Njia ya pili ni kutambua baadhi ya mambo yapo nje ya uwezo wetu kabisa. Kwamba tunaweza kufanya kila tunachopaswa kufanya lakini bado tukakutana na magumu kwa sababu kuna yaliyo nje ya uwezo wetu yanayokuwa yameingilia.
Ni muhimu kujua mambo yapi yako ndani ya uwezo wetu na kuyafanyia kazi, huku yale yaliyo nje ya uwezo wetu kuyapokea kama yalivyo.
Kuchukua hatua; rafiki yangu kwa kutumia njia hizi mbili kwa pamoja, hakuna gumu lolote linaloweza kututikisa, kwani tunafikiri kwa usahihi na kujua yaliyo nje ya uwezo wetu hatuna namna ya kuyaathiri.
Hata pale magumu yanapotokea hatupati taharuki au kuumia sana kwa sababu siyo kitu kinachokuja kwetu kwa mshangao.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Jinsi usomaji wa vitabu unavyopunguza msongo wa mawazo.
Rafiki yangu mpendwa msongo wa mawazo umekuwa ni sehemu ya maisha yetu, na kutafuta njia za kupunguza ni muhimu sana kwa afya zetu.
Kama ilivyo njia nyingi za kuondoa msongo wa mawazo kama vile; kufanya tahajudi, yoga na mazoezi, kusoma ni njia nzuri zaidi ya kupunguza msongo na kupumzisha mwili.
Usomaji wa vitabu unasaidia kutoa akili kwenye mafadhaiko nyingi ya siku kama vile kupunguza hofu na kutoa njia ya kutokezea.
Njia zifuatazo zinaelezea umuhimu wa usomaji wa vitabu na jinsi unavyopunguza msongo.
Usomaji unaondoa msongo wa mawazo. Usomaji umethibitishwa kuwa inaongeza kupumzisha mwili kama kupunguza mpigo wa moyo, kusaidia mvuto wa misuli,na shinikizo la damu.
Kusoma inapunguza msongo unaoletwa na shughuli za kazi za kila siku.Vitabu tofauti zinaelezea njia tofauti za kukabiliana na msongo. Kuna vitabu kama fiction genres ambazo zinasaidia kwenye hisia na utulivu wa mwili. Na vitabu kama self-help na non- fiction zinatoa ushauri wa kutatua changamoto au kupata uwezo wa kiakili ya jinsi ya kukabiliana na msongo.
Njia ya tatu ni kuweka malengo ya kusoma kulingana na hitaji na upendeleo wako. Kuweka lengo la kusoma itakusaidia kukaa kwenye mchakato wa usomaji na kuona umuhimu wa kusoma vitabu.
Ni muhimu kuchagua vitabu vinavyoendana na upendeleo na hitaji wako ndivyo usomaji uwe njia ya kupata msukumo na motisha.
Kutafuta saa na mahali nzuri ya kusoma kabla ya kulala inasaidia kupumzika na kujitayarisha kulala vizuri. Kutafuta mahali palipo tulia na nzuri inatengeneza mazingira chanya na kuepuka usumbufu mwingi.
Kuchukua hatua; rafiki ni jukumu letu sasa kuhakikisha tunasoma vitabu mbalimbali ambazo zitatusaidia kupunguza msongo wa mawazo na kupata utulivu wa kiakili.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Madhara makubwa ya hasira.
Rafiki yangu mpendwa hasira ina madhara siyo tu kwa mtu anayepata hasira, bali kwa familia, jamii na hata taifa kwa ujumla. Familia nyingi zimevunjika kwa sababu ya hasira.
Jamii zimekuwa na uhasama na watu wameuana kwa sababu ya hasira. Mataifa yameingia kwenye vita na damu nyingi kumwagwa kwa sababu ya hasira.
Mwanafalsafa Seneca anaeleza nguvu ya uharibifu wa hasira ni kubwa kwa sababu hasira ikishamtawala mtu haiwezi tena kudhibitiwa. Mtu anakuwa kama amepatwa na kichaa na anayoyafanya hayawezi hata kueleweka.
Hivyo salama yetu ipo kwenye kujua hatua za mwanzo za hasira na kuidhibiti kabla haijatutawala.
Seneca anaeleza hatua ya kwanza kabisa ya hasira ni tafsiri ambayo mtu anakuwa nayo kuhusu kitu au jambo. Pale mtu anapoamini kwamba ameumizwa au kutendewa isivyo sawa ndiyo hasira huanza kuwaka.
Hasira inashika kasi pale mtu anapoamua alipe kisasi kwenye kile ambacho anaona siyo sawa. Hapo ndipo hisia za hasira zinapata nguvu na mtu kujihalalishia kwamba kulipa kisasi ni sahihi.
Ni pale mtu anapoingia kwenye kulipa kisasi ndiyo hasira zinakuwa zimemtawala na hawezi tena kuzidhibiti. Hapo ndipo anafanya mambo ambayo baadaye huja kuyajutia.
Kuchukua hatua; kama ambavyo tumeona madhara ya hasira tunapaswa kuidhibiti hasira pale tunapozidiwa. Na pia hamna haja ya kulipiza kisasi ya hasira.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.
-
Jinsi ya kuondokana na hali ya kujiskia vibaya.
Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini sis binadamu ni kama viumbe wa kihisia ila kuna wakati hutokea tunakuwa hatujiskii vizuri.
Katika nyakati hizo tunakuwa chini sana na tunakosa msukumo wa kufanya chochote. Derek kwenye kitabu chake cha Hell yeah or no, anatushirikisha maswali matano ya kujiuliza na kujibu ili kuweza kuondokana kwenye hali hizo.
Jiulize ni kitu gani hakipo sawa kwako kwa wakati huo. Je unaumwa au una maumivu yoyote? Je kuna hatari yoyote inayokukabili? Mara nyingi hapa jibu linakuwa ni hapana, huna maumivu, ugonjwa au hatari yoyote inayokukabili. Kwa sehemu kubwa ni akili yako inatengeneza vitu ambavyo havipo.
Angalia sasa. Chukua hatua baadaye. Usikimbilie kufanya maamuzi au kuchukua hatua yoyote pale unapokuwa unajiskia vibaya. Iangalie hiyo hali jinsi inavyokwenda na jipe muda kabla hujaamua au kufanya chochote. Hii inakupa nafasi ya hisia zinazokukabili katika hali hiyo kupita.
Kuza viwango vyako. Jiwekee viwango vya juu na kataa chochote ambacho hakijafikia viwango hivyo. Pale unapokuwa hujiskii vizuri, usikubali chochote chini ya viwango vyako kukufanya uzidi kutokujiskia vizuri.
Sehemu kubwa ya kufanya hii ni kwa watu, unapokuwa chini, wakatae watu ambao wanazidi kukushusha au kukushikilia chini. Jihusishe na wale tu wanaokuinua juu zaidi.
Weka mkazo kwenye malengo yako. Kwa kuondoa vitu vilivyo chini ya viwango vyako, unapata nafasi ya kuweka nguvu zaidi kwa yale yaliyo muhimu zaidi kwenye maisha yako.
Jikumbushe malengo yako makubwa uliyonayo na jifunze na chukua hatua katika kuyafikia. Mara nyingi unajiskia vibaya pale unapoacha kuyaangalia malengo yako na kuhangaika na yasiyokuwa na tija kwako
Fanya vitu vyote vya msingi. Hata kama unajisikia vibaya au uko chini kiasi gani, hakikisha mambo yote ya msingi kwenye maisha yako umeyafanya.
Hatua ya kuchukua; amka mapema jifanyie usafi, pata milo kamili, fanya mazoezi jifunze na lala mapema.
Kwa kutokuvuruga utaratibu wako wa kila siku, itakusaidia kuvuka hali hiyo kwa haraka. Lakini ukikubali kuvunja utaratibu wako, utabaki kwenye hali hiyo kwa muda mrefu.
Unapokuwa umeyafanya yale yote ya msingi kabisa na ukajiuliza nini hakipo sawa, jibu utalipata kwamba kila kitu kipo sawa. Na hapo hutakuwa tena na sababu ya kuendelea kujiskia vibaya na kuwa chini.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.