Home

  • Sifa 4 Za Kufanya Kwa Makusudi.

    Rafiki yangu mpendwa ili uweze kufaulu kwa mambo yako unayofanya unapaswa ufanye kwa makusudi maalumu.

    Inasemekana kwamba inachukua mtu masaa elfu kumi ya kufanya kwa makusudi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa. Yaani angalau miaka kumi ili kufikia ‘ the world class ‘ kufanya bila kuacha.

    Jambo la kwanza ni kuweka malengo . Watu wengi wanafanya mambo bila kuweka malengo. Wanafanya kwa mazoea kabisa bila kuweka juhudi yoyote. Hata kama wanaweka juhudi fulani, juhudi hizo zinafanywa tu bila lengo.

    Mwisho mtu unatumia muda bila kupata chochote kwenye maisha. Unapaswa kuanza na lengo fulani likusukume kufikia mafanikio unayoyataka.

    Jambo la pili ni kuweka uzingatiaji au (focus). Kwa kuweka umakini wako kwenye yale unayofanya na kuacha mengine yote na kuweka umakini kwenye yale muhimu kwako.

    Sina uhakika kama itakufaa, lakini unaweza ukafanikiwa kwenye eneo lolote lile la maisha kama utaweka umakini na utulivu mkubwa kwa muda mrefu.

    Jambo la tatu ni kupata mrejesho. Watu wengi huwa hawapokei mrejesho unaofaa. Kwenye jamii zetu ni vigumu sana watu kuwaambia ukweli.

    Lakini ukiweza kupata mrejesho sahihi, itasaidia juhudi ulizoweka isipotee. Watu wengine wanaweza kuwa bora zaidi kupitia mrejesho unaotoa.

    Unapopata mrejesho unajiboresha kwa sababu utakaa chini na kujifanyia tathmini ili kuweza kurekebisha makosa .

    Jambo la nne ni kuendelea kukua. Je umekuwa ukifanya mambo yako na haukui? Labda unafanya kwa uchache zaidi, unapaswa kufanya na kwenda ngazi ya juu zaidi.

    Kinachokukwamiza wewe ni kuwa na malengo madogo sana. Unaanza kufanya mambo mengine yasiyofaa, inakutaka wewe uwache usumbufu na kusumbuka na mambo madogo madogo. Ukishafikia lengo fulani unapaswa kuongeza lengo hilo zaidi.

    Chukua hatua ; hupigi hatua kwa sababu hufanyi kwa makusudi. Kuna namna hufanyi kwa makusudi, Kuna mahali unadanganya, unapaswa kufanya kitu kwa makusudi na pia kutoka ndani yako.

    Naandika haya kwa ajili ya kujifunza na pia kujiimarisha na kuimarisha wengine. Na Mimi nimejifunza kitu, je wewe umetoka na nini ya kufanyia kazi?

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

    uamshobinafsi.com.

  • Fanya Mazoezi Ili Kuwa Mbunifu.

    Rafiki yangu mpendwa watu wengi wanaposikia na kufikiria kuhusu kufanya mazoezi, huwa wanajiangalia wao wenyewe.

    Huona wanafanya mazoezi ili kupunguza uzito au kuwa na afya bora.

    Lakini mazoezi ni zaidi ya wewe kupunguza uzito na kuwa na afya bora, na imara itakayokuwezesha kufanya kazi yako kwa muda mrefu zaidi bila kuchoka haraka.

    Unapofanya mazoezi akili yako inapata kemikali inayokufanya ujiskie vizuri, kitu ambacho kinakufanya uwe mbunifu zaidi na kuzalisha zaidi.

    Unapofanya mazoezi unakuwa na nidhamu na hivyo kuweza kuitumia nidhamu hiyo kufanya kazi bora.

    Unapofanya mazoezi unakuwa na utulivu na uvumilivu makubwa, vitu vinavyokuwezesha kufanya maamuzi bora.

    Kwa kifupi, kadiri unavyofanya mazoezi ya mwili, ndivyo unavyoongeza ubunifu wako, ufanisi wako na thamani unayotoa kwa wengine, kitu kinachofanya uingize kipato zaidi.

    Chukua hatua; hivyo kama unataka kuongeza kipato chako na kufanikiwa zaidi, anza kwa kufanya mazoezi zaidi ya mwili wako.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Kwa Nini Furaha Yako Isitegemee Vitu Vya Nje.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini ili uwe na maisha ya furaha kila mara kwenye maisha yako, furaha yako haifai kabisa itegemee vitu vya nje kama; magari,vyumba,pesa,na kadhalika. Bali inafaa itoke ndani yako hufurahie yale umejaaliwa kuwa nayo.

    Kama unataka kuwa huru kwenye haya maisha basi hakikisha furaha yako isitoke au kutegemea vitu vya nje.

    Mpaka ukiwa na fulani ndiyo maisha yako yanakuwa na furaha.

    Mpaka unywe kinywaji fulani ndiyo maisha yako yatakuwa na furaha. Usipopata kinywaji hicho basi huna furaha.

    Kifupi, furaha ya maisha yako ISITEGEMEE VITU VYA NJE.
    Unajua kwa nini?
    Kwa sababu, “Kama furaha na uhuru wako unategemea vitu vya nje, mara zote utakuwa mtumwa wa wale wanaoweza kukupa au kukunyima kile unachotegemea.

    Kama unataka kuwa mtumwa kwenye maisha yako, na watu wakupe au wakunyime furaha yako ni kujishikiza kwenye maisha yao.

    Yaani ukishasema maisha yako hayawezi kwenda bila yeye basi huo tayari ni utumwa.
    Unakuwa unampa mtu mwingine mamlaka kwenye furaha yako.
    Yaani watu wengine ndiyo wanaamua wakupe furaha au wasikupe furaha.

    Hatua ya kuchukua leo; usikubali furaha yako itegemee vitu vya nje.
    Furaha yako itoke ndani na siyo kwenye vitu.

    Ukisharuhusu tu furaha yako iwe kwenye vitu vya nje, tayari unakuwa umejiweka katika mbaya.
    Usikubali kuruhusu furaha yako kujishikiza kwenye vitu vya nje.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

    https://kessydeo.home.blog

  • Kuwa Chanya Asubuhi.

    Rafiki yangu mpendwa, unapoianza siku yako na kama unataka siku yako nzima iwe nzuri unapaswa kuianza asubuhi.

    Kuwa na mawazo chanya asubuhi, unakuwa ni wakati wa kuibadilisha kabisa siku yako.

    Kitendo tu cha kujitamkia maneno chanya, kinabadili kabisa siku yako nzima.

    Asubuhi unapoamka , jiambie maneno chanya kama vile. Mimi ni mshindi nimezaliwa kushinda.

    Leo ni siku bora na ya kipekee kwangu kwenda kufanya makubwa. Mimi ni mtu mwenye bahati sana na maisha yangu yamebarikiwa sana . Nina amini mambo mazuri yanakwenda kutokea leo katika maisha yangu.

    Kujitamkia maneno chanya ni sala ambayo unapaswa kusali kila siku asubuhi kabla hujaianza siku yako.

    Kuwa na kitu chanya asubuhi na itakwenda kuibadilisha kabisa maisha yako.

    Hakikisha unakuwa na sala yako maalumu ya kujinenea kila siku. Na ikiwezekana kabisa, uwe unajiambia kwa mdomo na kuandika. Na mara baada ya kuandika, unaweka na tarehe na sahihi kabisa.

    Hii inafanya kazi kubwa, na ifanye hivi kila wakati.

    Hatua ya kuchukua ; jitamkie maneno chanya kila siku asubuhi kabla hujaondoka nyumbani.

    Mara zote jitamkie maneno chanya.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Jiamini Na Amini Kwenye Ndoto Yako Kubwa.

    “Believe in yourself and you will be unstoppable.” Emily Guay.

    Utakapojaribu kufanya kitu chochote kikubwa kwenye maisha yako, ndiyo utaujua uhalisia wa dunia, kila kitu kutaibuka kukupinga na kukuzuia .

    Vitaibuka vikwazo ambavyo hata hukuwahi kuvifikiria. Hata ndugu na jamaa wa karibu watakuwa kikwazo kikubwa kwako.

    Nguvu ya kukupinga itakuwa kubwa kiasi kwamba huwezi kabisa kupiga hatua. Unaweza kuwa unajua hili vizuri kama umeajiriwa na ukawahi kuwaambia watu wa karibu yako kwamba unataka kuacha kazi ujiajiri.

    Sasa kipo kitu kimoja ambacho kinaweza kukufanya usizuilike, pamoja na vikwazo na mapingamizi ya wengine, ukaweza kuchukua hatua na ukafanikiwa zaidi baadaye.

    Kitu hicho ni; kujiamini na kuamini kwenye ndoto yako kubwa na kile unachofanya.

    Chukua hatua; anza kujiamini na amini kwenye ndoto yako kubwa na utaweza kufanya makubwa kwenye maisha yako.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Salaam Za Kheri Ya Mwaka Mpya 2024 Kutoka Kwa Maureen Kemei.

    Rafiki yangu mpendwa, salaam alaikum. Napenda nichukue nafasi hii kukutakia kheri ya mwaka mpya 2024.

    Sina uhakika kama itakufaa, lakini ule mwaka uliokuwa umesubiri sana kwa hamu ndio huu hapa umefika.

    Bila shaka umeanza kufanyia kazi mambo yote uliyokuwa umesema kwamba utayafanya ndani ya huu mwaka, sasa ndiyo muda nzuri sana wa kufanya na kukamilisha kwa ushindi kubwa.

    Kabla hujafanya maamuzi kwenye lengo lako kuu la mwaka, ni bora kuweka mipango na malengo ya jinsi gani utajituma kila siku kuhakiksha lengo linatimia kabla huu mwaka uishe.

    Rafiki kwa kuweka malengo na jinsi utakavyofanyia kazi ni njia moja ya kujipa uhakika kwamba mwaka huu utakuwa wa baraka kwako.

    Kuchukua hatua, rafiki yangu siku ya leo pitia malengo yako kama ulikuwa umeweka na kama bado hujaweka, weka sasa na ufanyie kazi kila siku.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Ni Kitu Gani Unathamini Sana Kwenye Maisha Yako?

    Karibu kwenye makala hii ambayo itajadili kuhusu kitu muhimu ambayo watu wanaithamini sana kwenye maisha. Kila mtu kuna kitu anachokithamini zaidi kwenye maisha na hiyo ndiyo kinamsukuma kufanya maamuzi yote ya maisha yake.

    Wanaofanikiwa ni wale wanaojua kile wanachothamini zaidi na kuishi maisha yao kwa namna ambayo wanakifanyia kazi.

    Sina uhakika kama itakufaa, lakini huwezi kufanikiwa bila kujitambua wewe mwenyewe, bila kujua nini hasa unataka nini unathamini zaidi na hata uimara yako.

    Kujua kile unachothamini zaidi, jiulize maswali haya manne.

    1. Ni wakati gani ulikuwa na furaha sana kwenye maisha yako? Angalia ulichokuwa unafanya wakati huo na namna gani ulikuwa unafanya na utaona ni kile unachothamini zaidi.
    2. Ni wakati gani ulikuwa umevurugwa sana na kwenye maisha yako, ukiangalia utaona hukuwa unafanya kile unachothamini.
    3. Ni wakati gani ulikuwa umekata tamaa kabisa na maisha yako, ukiangalia utagundua hukuwa na matumaini ya kuweza kuishi kile unachothamini.
    4. Ni kitu gani unakipenda sana kwa jinsi unavyofanya mambo yako kiasi kwamba wengine wanakuona ni mtu wa ajabu? Hicho kinaathiria unachothamini zaidi.
    5. Jua unachothamini kwenye maisha yako na kuishi, maana ukikipuuza, sehemu fulani ya ndani yako inakufa na unaishia kukata tamaa.
    6. Unaweza kuwa unathamini uhuru binafsi, mchango wako kwa wengine , maamuzi yako, mipango yako, kuanza na kukamilisha mambo makubwa na kadhalika.

    Kuchukua hatua; jijue wewe mwenyewe na yale unayothamini na kwa kuyafanya unakuwa na nguvu isiyozuilika.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Jinsi Ya Kuepuka Migogoro Isiyofaa.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini kuna wakati watu wanatukwaza na kufanya mambo yanayoenda kinyume na yale tunayosimamia.

    Katika nyakati hizo huwa tupo tayari kupambana nao ili kusimamia maadili au maamuzi yetu. Hili ni sahihi, kwa sababu kama huna unachosimamia, kila kitu kitakuangusha.

    lakini siyo kila vita unapaswa kupigania, siyo kila mgogoro unapaswa kujihusisha nao. Chagua migogoro utakayojihusisha nayo na ambayo utaiepuka.

    Kama mgogoro unaathiri ubunifu wako, ufanisi, furaha kwenye maisha, achana nao.

    Hata kama wewe ndiye mwenye haki na una uhakika wa kushinda, ushindi utakaoupata hauwezi kufidia kile utakachokuwa umepoteza.

    Ebuka migogoro ambayo ina madhara makubwa kwako kuliko faida. Hata kama utakuwa umewapa wengine ushindi wako, ushindi mkuu wa kuwa na maisha bora na tulivu utabaki kwako.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Mambo 6 Ya Kujifunza Kutoka Kwa Leonardo Da Vinci.

    Rafiki yangu mpendwa Robina anatushirikisha aliyojifunza baada ya kutembelea jumba la makumbusho ya kazi za Leonardo da Vinci ambaye anachukuliwa kuwa mtu mbunifu zaidi kuwahi kuishi hapa duniani.

    Wengi waliamini uwezo wake haukuwa wa kibinadamu, bali kulikuwa na uungu ndani yake. Kwani katika kipindi chake alifanya makubwa kwenye sekta mbalimbali kama usanifu, uinjinia, sayansi ya anga na muundo wa viumbe hai.

    Robin anatushirikisha tabia sita za Leonardo alizojifunza kutoka kwenye vitabu vyake na ambazo zilimwezesha kuwa mbunifu wa kipekee.

    Tabia ya kwanza ni kuandika. Leonardo alikuwa na tabia ya kuandika kila alichofikiria na alichopanga kufanya. Kuandika kulimwezesha kupangilia mawazo yake vizuri na hivyo kuweza kufanya makubwa.

    Tabia ya pili ni kutumia udadisi uliokuwa ndani yake. Wote tulipokuwa watoto tulikuwa wadadisi, lakini baada ya kukua tukaacha udadisi huo. Leonardo hakuwahi kuacha udadisi wake, aliendeleza kila alichofanya akiwa na udadisi kama wa mtoto mdogo. Hivyo alikuwa tayari kuuliza maswali na kutafuta majibu, badala ya kujiambia tayari najua.

    Tabia ya tatu ni kuwa na subira. Leonardo hakuwa anaharakisha kufanya kazi zake, alijipa muda wa kutosha katika kufanya kazi zake na hilo lilimwezesha kuzalisha matokeo makubwa.

    Wakati anachora moja ya picha zake maarufu sana ya chakula cha mwisho cha Yesu, alikuwa anaweza kuangalia picha kwa siku nzima bila kufanya chochote, kisha akafanya marekebisho machache na kuondoka. Lilimchukua muda mrefu kukamilisha picha hiyo, lakini ni picha maarufu kuliko zote duniani.

    Tabia ya tano alitenga muda wa kupumzika. Leonardo hakuweka muda wake wote kwenye kazi, badala yake alijipa muda wa kupumzika na kutembea maeneo mbalimbali. Hilo liliipa akili yake mapumziko ambayo yalichochea zaidi ubunifu. Na pia katika matembezi yake, ndipo alipata mawazo mapya ya kufanyia kazi.

    Ubunifu unahitaji mtu ayaishi maisha kwa ukamilifu wake na siyo kufanya kazi muda wote na kuichosha akili mpaka inashindwa kuja na ubunifu mzuri.

    Tabia ya sita ni kupenda uzuri wa asili. Leonardo alitumia muda wake mwingi kutembea kwenye asili, sehemu ambayo alipata mawazo mazuri na ya kibunifu. Kwa kuona uzuri wa asili na utulivu mkubwa wanaokuwa nao, mawazo ya kibunifu yanakuja kwao kwa urahisi.

    Chukua hatua, hata wewe rafiki yangu unaweza kujijengea ubunifu kama Leonardo, unachohitaji ni kujijengea tabia hizo sita.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Siri 4 Za Kujenga Mtazamo Wa Uwezekano.

    Rafiki yangu mpendwa tunaishi kwenye kipindi ambacho mambo hasi yanapewa nguvu kubwa na ni rahisi sana kukata tamaa. Lakini pia njia za mkato ambazo siyo sahihi zimekuwa nyingi na kuwapoteza wengi. Tunapaswa kuwa na njia ya kujilinda ili kutokukata tamaa na kufanya yaliyo sahihi.

    Ili kutokukata tamaa, tunapaswa kujaza akili zetu fikra sahihi za ndoto kubwa ambazo tunazo na kufanya hizo zitutawale muda wote. Kwani akili zetu ni ni kama kisima, kikiwa kitupu, kitajaa uchafu. Kama hakuna fikra sahihi zinazojaa akili yako, fikra za hovyo zitapata nafasi na kukukatisha tamaa.

    Kuepuka kufanya yasiyo sahihi jiwekee sheria ya mara zote kufanya kilicho sahihi na siyo kilicho rahisi. Kwa kila unachofanya mbele yako kutakuwa na njia mbili, iliyo sahihi na iliyo rahisi. Na karibu mara zote, kilicho rahisi kufanya huwa siyo sahihi. Hivyo fanya maamuzi yako kwa kuangalia usahihi na siyo kuangalia urahisi.

    Siri ya kwanza ya kujenga mtazamo wa uwezekano ni kuwa na kadi ndogo ambayo umeandika kauli au nukuu chanya na inayokupa msukumo mkubwa. Kwenye siku yako, kadiri unavyopata muda soma kadi hiyo na utendelea kubaki chanya na kuwa na msukumo mkubwa.

    Mbili pata muda wa kuwa peke yako kuwa na utulivu. Kelele na usumbufu unaotuzunguka kila mahali na kila wakati imekuwa chanzo cha wengi kuvurugwa. Ili kuondokana na hilo, tenga muda utakaokuwa peke yako na kwenye utulivu mkubwa.

    Tumia muda huo kufanya tahajudi na kutafakari mambo mbalimbali kwenye maisha yao. Huu ni wakati wa kuwa na wewe mwenyewe, ambao ni muhimu kwa mafanikio yako.

    Tatu ni shukuru kwa mnyororo mzima wa thamani. Haijalishi unapitia nini, kuna mambo mengi mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako. Shukuru kwa mambo hayo na hilo litakufanya uwe kwenye mtazamo mzuri.

    Na usiishie tu kushukuru kile kilicho mbele yako, bali shukuru mnyororo mzima wa thamani. Mfano kama umesafiri salama, shukuru dereve wa gari, waliojenga barabara na wengine wanaohusika kuhakikisha safari inakuwa salama. Kadhalika unaponunua kitu, shukuru mnyororo mzima wa thamani unaowezesha wewe kupata kitu hicho.

    Nne ona suluhisho kwenye kila tatizo. Hakuna tatizo ambalo halina suluhisho ndani yake. Hivyo wewe usiwe mtu wa kuangalia tu tatizo, bali angalia ni suluhisho lipi lililo ndani ya tatizo hilo. Kwa kutafuta suluhisho utaliona na kuweza kutatua matatizo mbalimbali yanayokukabili.

    Chukua hatua, rafiki yangu usikubali chochote kile kikukatishe tamaa, kuwa na mtazamo wa uwezekano mara zote na utaweza kufanya makubwa.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei .

    kemeimaureen7@gmail.com