Home

  • Umuhimu Wa Kuishi Maisha Yako.

    Rafiki yangu mpendwa watu wengi wamekuwa wakifanya mambo kwa ajili ya kujijengea sifa baada ya kuondoka hapa duniani.

    Wanafanya kwa lengo la kuendelea kukumbukwa vizazi kwa vizazi kwa majina yao kuandikwa maeneo muhimu au kuchengewa masanamu.

    Lakini kama ilivyo kwenye mambo mengine ya maisha, unapolazimisha kitu, huwa hakitokei.

    Unapofanya mambo ili ukumbukwe, hakuna anayekukumbuka, kwa sababu unakuwa siyo halisi.

    Achana na msukumo wa kufanya kitu ili kukumbukwa au kuacha alama. Badala yake chagua kuishi maisha halisi kwako, simamia kile kweli unachoamini na utakuwa na maisha bora huku pia ukiwa na nafasi kubwa ya kuendelea kukumbukwa.

    Watu hawatakukumbuka kwa sababu unataka wakukumbuke, bali watakukumbuka kwa aina ya maisha unayoishi. Hivyo wajibu wako mkubwa ni kuyaishi maisha yako kwa uhalisia na ukamilifu.

    Furahia pale mambo yanapokwenda vizuri na kuwa na shukran yanapokwenda vibaya.

    Waelewe wale wanaokuzunguka na wasamehe wale wanaokuumiza. Ichukulie kazi au biashara yako kwa heshima kubwa na toa thamani kubwa kwa wengine.

    Chagua kuwa wewe na kusimamia kile kilicho sahihi hata kama wengine wote wanapingana na wewe.

    Kuwa mnyenyekevu kadiri unavyofanikiwa na endelea kuifanya dunia kuwa bora zaidi.

    Jifunze kutokuweka uzito kwenye mambo madogo madogo na jua mengi unayohofia hata haitatokea.

    Chukua hatua; rafiki chagua kuyaishi maisha yako halisi wakati huu ukiwa hai na usijisumbue na nini kitatokea baada ya kuwa umekufa.

    Utakuwa chakula cha mchwa na mbolea ya ardhi. Namna ulivyoishi maisha yako ndiyo itaacha alama hapa duniani.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Matatizo 2 Makubwa Ya Fedha.

    Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini pale fedha inapotawala, matatizo mawili hujitokeza.

    Tatizo la kwanza ni kuyeyusha misingi muhimu. Pale fedha inapokuwa kitu kikuu, watu hawaoni tena umuhimu wa kujenga misingi muhimu, badala yake wanaangalia kile kinachoingiza fedha kwa sasa.

    Matokeo yake ni jamii inakosa taasisi muhimu zinazoweza kudumu kwa muda mrefu.

    Chukua mfano kwenye biashara, pale ambapo lengo la biashara ni kuingiza faida kubwa kwa muda, hauwezi kufanya uwekezaji wa muda mrefu.

    Matokeo yake ni biashara kushindwa kudumu kwa muda mrefu.

    Tatizo la pili ni kuondoa utofauti na upekee. Pale fedha inapokuwa ndiyo lengo kuu, kila biashara inakazana inapunguza gharama ili kuongeza faida zaidi. Kinachotokea ni bidhaa na huduma kuwa na ubora wa hali ya chini na zinazofanana kote.

    Hakuna aliye tayari kuingia gharama kuuza bidhaa au huduma ya kipekee, kwa sababu iyo hauwezi leta faida kubwa.

    Hii imepelekea biashara nyingi ndogo kushindwa kushindana na biashara kubwa, kwa sababu biashara kubwa zina nguvu kubwa ya mtaji.

    Biashara hizo ndogo zinaposhindwa na kufa, ule upekee unapotea kabisa. Na kinachobaki ni bidhaa na huduma zinazofanana kwa kila namna.

    Haya yanachangia sana watu kushindwa kujitoa kwenye kitu kimoja kwa muda mrefu.

    Fedha unapokuwa muhimu kuliko kingine chochote, ndiyo inayopewa kipaumbele kikubwa.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Jinsi Tabia Mbaya Ndani Ya Mtu Inavyokua.

    Rafiki yangu mpendwa kila mtu huwa anakasirika na hasira huwa zinamsukuma mtu kufanya kitu anachojutia baadaye. Kadhalika kwa hisia nyingine kama wivu, hofu na chuki.

    Kwenye mitandao ya kijamii kuna watu ambao kazi yao ni kuibua hisia kali kwa wengine ili kuibua mabishano na kushambuliana mtandaoni trolling.

    Hilo kumekuwa na manufaa kwa mtandao wa kijamii, maana watu wanapokuwa na hasira ni rahisi kuwabadili na kuwashawishi kufanya chochote.

    Ukijiangalia wewe mwenyewe, kuna mitandao ukiitumia au watu ukijadiliana nao mitandaoni unajikuta unakuwa mtu ambaye hukutegemea. Unajikuta umetoka maneno machafu na makali, umedharau na kudhalilisha wengine kwa sababu ya hisia kali ambazo umekuwa nazo.

    Ukishagundua mitandao hii inaibua hisia kali kwako na zinazokugeuza uwe mtu wa hovyo, sawa ni kuachana nayo.

    Maana mitandao hiyo itaendelea kuchochea hali hiyo ya kuibua hisia ili inufaike, huku wewe ukizidi kuwa hovyo na hata kuharibu sifa yako.

    Kuna watu wamefukuzwa au kukosa kazi kwa sababu ya mambo waliyoweka kwenye mitandao ya kijamii, ambayo hata hayakuwapa faida yoyote ile. Wengi huishia kujutia, usisubiri mpaka ujutie, chukua hatua ya kuachana na mitandao hiyo mara moja.

    Chukua hatua; rafiki usikubali mitandao ya kijamii ikubadilishe kuwa mtu ambaye siyo, unapaswa kuwa mtu halisi, na siyo kuwa mtu wa hovyo asshole au kuigiza ni mtu mwema.

    Mitandao haikupi nafasi ya kuwa mtu halisi, itakulazimisha uwe asshole au uigize ni mtu mwema sana, yoyote kati ya hizo itakuchosha zaidi.

    Kwa kuwa mitandao ya kijamii inapenda watu wawe na hisia kali muda wote, wawe wenye tabia za hovyo ndiyo wanaopewa nafasi zaidi, kitu kinachowafanya watu kuzidi kuwa na tabia mbaya zaidi.

    Chukua mfano wa kile kinachoitwa kiki, kwa kuwa wanajua habari za umbeya zinafuatiliwa zaidi, wamekuwa wanatengeneza umbeya ili tu kuzungumziwa mitandaoni.

    Wapi ambao wamekuwa wanaigiza kuachana na wenza wao huku wengine wameenda mbali zaidi na kudanganya wamekufa.

    Hapo bado wale wanaoshambulia watu maarufu, au siyo ya kweli kwa mambo yasiyo na kweli, ili tu kujizolea umaarufu.

    Bado hujaweka viongozi wanaotumia mitandao kusambaza uongo na chuki. Ukiangalia yote hayo, unaona jinsi mitandao hii ilivyo hatari katika kuwafanya watu wawe na tabia za hovyo asshole na hata kuleta mifarakano kwenye jamii.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Uraibu Unavyozalisha Tabia Mbaya.

    Rafiki yangu mpendwa uraibu wa aina yoyote ile, huwa unabadili tabia ya mtu kabisa. Mtu akishakuwa na uraibu hawezi tena kufikiria, anakuwa kama msukule.

    Yuko tayari kufanya chochote bila kujali madhara yake, hili tu kukamilisha hitaji la uraibu wake.

    Mfano mzuri ni wateja wa madawa ya kulevya wanapotaka kupata madawa, wapo tayari kufanya chochote ili kukamilisha hilo.

    Hivyo pia ndivyo mitandao ya kijamii inavyobadili watu, inawafanya wawe na uraibu wa mtandao hiyo kisha kuwasukuma kupata kile wanachotaka bila kujalia madhara yake.

    Kuna baadhi ya tabia ambazo zimekuwa zinaoneshwa na waraibu wa mitandao ya kijamii ambazo zina madhara kwao na kwa wengine, lakini hawajali. Tabia hizo ndizo zinainufaisha zaidi mitandao hiyo.

    Baadhi ya tabia hizo ni:

    1. Ubinafsi wa mtu kujiangalia mwenyewe bila kujalia wengine.
    2. Hofu na wasiwasi uliopitiliza kwa kitu kisichoonekana na wengine.
    3. Kiburi na dharau kwa wengine. Watu wakishakuwa na uraibu wa mitandao wa kijamii na kuwa na wafuasi wengi hupata kiburi na kujiona wako juu kuliko wengine.
    4. Kuamini vitu visivyosahihi au uhalisia. Imani za nadharia za uongo conspiracy theories zimekuwa zinasambazwa kwa kazi kupitia mitandao ya kijamii.
    5. Kwa kuwa mtu anateseka na uraibu wake, anahakikisha anawatesa wengine pia. Watu wamekuwa wanatumia mitandao ya kijamii kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wengine hasa wanapokuwa wanajua udhaifu wao.

    Mwandishi wa kitabu cha ten arguments for deleting your social media accounts right now, anatupa mfano wa aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump ambaye alikuwa anatumia sana mtandao wa Twitter, ambapo kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda ndivyo alivyokuwa ana uraibu na mtandao huo na kuwa na tabia za hovyo.

    Hiyo ilipelekea Twitter na mitandao ya kijamii kumfungia kabisa, lakini ni baada ya mitandao hiyo kuwa imenufaika na uwepo wake vya kutosha na kuona hawezi kuwa na manufaa kwao tena baada ya kushindwa kwenye uchaguzi.

    Kwa kuangalia sakata la Trump na mitandao ya kijamii, tangia uwepo wake mpaka kufungiwa kwake, ni sababu tosha kwa nini kila mwenye akili timamu anapaswa kuachana kabisa na mitandao hiyo.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

  • Gereza Ambalo Mtu Unatembea Nalo.

    Mabadiliko makubwa ya teknolojia yaliyotokea miaka zaidi ya kumi iliyopita ni ujio wa simu janja smartphones, kifaa chenye uwezo mkubwa kama kompyuta na mtu unatembea nacho kila mahali.

    Kifaa hicho ni gereza mbalo mtu unatembea nalo kwa sababu kumekuwa kinatumika kukubadilisha tabia ili uendane na matakwa ya watu wachache wanaotaka kujinufaisha na kufaidika kupitia wewe.

    Kifaa hicho kinakuletea mapendekezo madogo madogo ambayo yanabadili kabisa maisha yako huku wewe ukiwa hujui kinachofanyika.

    Mwandishi wa kitabu cha ten arguments for deleting your social media accounts right now, anasema kifaa hiki kimetugeuza watu kuwa kama wanyama wanaofanyiwa majaribio kwenye maabara.

    Mitandao ya kijamii ina mfumo wa kukusanya taarifa Algorithms ambayo inakusanya taarifa nyingi za kila aina ambacho kila mtu anafanya akiwa kwenye mitandao hiyo.

    Umewahi kuangalia video moja mtandaoni kisha ukaletewa video nyingine nyingi zinazofanana na hiyo? Hapo jua mfumo huo unafanya kazi.

    Algorithms ni mfumo mkubwa unofanya kazi kila wakati na kukusanya taarifa zako zote za matumizi ya mitandao hiyo. Ukifungua kiungo cha aina fulani, mfumo unachukua taarifa, kama unaendelea kuangalia picha au video za aina fulani taarifa zako zinachukuliwa.

    Mfumo hiyo ina uwezo mpaka wa kujua ni wakati gani una furaha, wakati gani una huzuni na taarifa nyingine nyingi.

    Sasa pata picha mfumo huo inakusanya taarifa za mabilioni ya watumiaji ya mitandao hiyo, kisha kuzichakata kulingana na umri wa mtu, jinsia, alipo na taarifa zake nyingine nyeti anazokuwa ameweka kwenye mitandao hiyo.

    Kuwa na taarifa nyingi za mtu kunaipa mifumo hiyo nguvu ya kukushawishi bila ya wewe kujua. Kwa sababu inakuwa inakujua kuliko unavyojijua wewe mwenyewe.

    Lakini kumbuka mfumo huo haujaja kwako kukulazimisha uupe taarifa, ni wewe mwenyewe unaupa taarifa kwa kila unachofanya kwenye mitandao hiyo.

    Na ukishaupa mfumo taarifa za kutosha, unakuwa umeupa nguvu ya kukushawishi, unajikuta unafanya vitu ukifikiri umeamua mwenyewe, kumbe umeshawishiwa.

    Mfano, mfumo umejifunza kuwa ukiwa na huzuni unaangalia video za aina fulani, hivyo ukianza kuangalia video hizo, mfumo unakuletea tangazo ambalo litakushawishi zaidi kwa kuwa huzuni. Utajikuta unafanya maamuzi bila ya utashi wako.

    Hii ni hatari kubwa ambayo wengi hawaijui, lakini mambo mengi ambayo watu wanafanya wameshawishiwa na mitandao wa kijamii bila wao kujua. Ndiyo maana mwandishi anasisitiza sana, njia pekee ya kuepuka hili ni kuacha kabisa kutumia mitandao hiyo.

    Maana hata ukisema unatumia kwa kujidhibiti, bado mfumo unakusanya taarifa zako nyingi kila unapotumia na kuzitumia kukushawishi ufanye maamuzi yenye manufaa kwa wengine na siyo kwako.

    Mitandao ya kijamii huwa inakusanya taarifa za watumiaji wake na kisha kuziuza kwa wale wanaotaka kutangaza biashara zao kupitia mitandao hiyo.

    Matangazo yanakuwa na ushawishi mkubwa kwa sababu yanakuwa yanamlenga moja kwa moja mtu ambaye yuko kwenye hali ya kushawishika haraka, mtu ambaye utashi wake haupo huru tena.

    Unapotumia mitandao hii, huna tofauti na panya anayefanyiwa majaribio kwenye maabara. Wewe unafanyiwa majaribio ya kiutashi, kwa kufuatiliwa kwa muda mrefu, tabia zako kujulikana na kisha kuletewa matangazo yanayokuwa na ushawishi mkubwa kwako, bila ya kujua kama ni matangazo.

    Asante,

    Rafiki wako,

    Maureen Kemei .

    kemeimaureen7@gmail.com

  • Sheria Kuu 2 Za Mafanikio.

    Rafiki yangu mpendwa ili kupata na kudumu kwenye mafanikio makubwa, unapaswa kufuata sheria hizi mbili.

    Moja, kazana kuwa bora zaidi. Usiishi au kufanya chochote kwa mazoea. Hakikisha kila siku yako unajisukuma kuwa bora kuliko siku iliyopita. Siku zako mbili zisifanane.

    Kwa kila unachofanya, jiulize unawezaje kukiboresha zaidi na chukua hatua za kukiboresha.

    Kujifunza kwako kuwe endelevu, usifikie hatua na kuona kwamba umeshajua kila kitu.

    Usiridhike na popote ulipofika, kazana kuwa bora zaidi na kwenda juu zaidi.

    Mbili, wasaidie wengine. Kwa chochote unachofanya, kazana kutoa thamani kubwa kwa wengine kuliko unachopokea.

    wajali wengine kwa kuweka maslahi yao mbele, kuwasikiliza na kuwafanya wajione ni wa muhimu.

    Wape msaada wale wenye uhitaji mbalimbali kadiri unavyoweza kufanya hivyo.

    Kuwa mtu wa watu na utafanikiwa na kudumu kwenye mafanikio hayo.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Kanuni Ya Pareto 80/20.

    Rafiki yangu mpendwa kanuni hii huwa inasema asilimia 20 ya juhudi huwa inazalisha asilimia 80 ya matokeo.

    Yaani katika mambo kumi unayofanya, asilimia mbili tu ndiyo inazalisha asilimia 80 ya matokeo.

    Kama unafanya kazi kwa masaa kumi kwa siku,masaa mawili pekee ndiyo yanayozalisha asilimia 80 ya matokeo unayoyapata.

    Hiyo ina maana kwamba ukiyajua masaa mawili yenye manufaa makubwa na kuyazingatia hayo, kipato kitapungua kidogo, lakini utakuwa na muda mwingi zaidi, ambao unaweza kuutumia kufanya mengine muhimu na ukaingiza kipato kwa njia nyingine.

    Chukua hatua; rafiki kokotoa muda wako wa kazi na uone ni masaa mangapi unayafanya kazi ambayo yanakupa matokeo mazuri unayoyataka.

    Kisha masaa zingine ya ziada unaweza ukatumia kufanya kazi zingine muhimu na ukaingiza kipato kwa njia nyingine.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

  • Umuhimu Wa Kuzungukwa Na Watu Sahihi.

    Rafiki yangu mpendwa kufanya makubwa siyo kitu rahisi, kuna changamoto na vikwazo, kuna kushindwa na kukata tamaa.

    Hivyo basi, utaweza kuyavuka hayo kama utakuwa umezungukwa na watu sahihi.

    Tafuta watu ambao wanafanya makubwa, kisha zungukwa nao, kuwa na kikundi cha watu wanaofanya makubwa ambao mnapeana moyo wa kuendelea na mapambano.

    Usisubiri mpaka watu waje wakuite na kukuweka kwenye kikundi cha aina hiyo, tafuta kikundi ambacho tayari kipo, na kama hakuna anzisha kikundi cha aina hiyo.

    Wale wanaokuzunguka wana mchango mkubwa kwenye yale unayoyafanya.

    Kama unataka kufanya makubwa, lazima uzungukwe na wale wanaofanya makubwa pia.

    Chukua hatua; rafiki kama unataka kufanya makubwa na kuacha alama hapa duniani, lazima uzungukwe na watu sahihi, watu wanaoweza kukukosoa unapokosea na kukuelekeza kwenye njia sahihi.

    Mwandishi wako,

    Maureen Kemei,

    kemeimaureen7@gmail.com

    uamshobinafsi.com

  • Umuhimu Wa Kutoa Kafara.

    Rafiki, kila mtu kwenye maisha kuna kafara anayotoa, kitu muhimu anachoamua kukipoteza ili kupata kingine anachokihitaji zaidi.

    Wanaofanikiwa na kupata utajiri ni wale wanaotoa kafara ya muda. Hawa wanautumia muda mwingi kwenye kazi zao na kukosa muda wa starehe mbalimbali. Hawa huonekana kama hawana mlinganyo wa maisha, lakini huishia kuwa na maisha bora.

    Wasiofanikiwa na wanaobaki kwenye umaskini huwa wanatoa kafara ya ndoto zao. Hawa wanakubali kuzika ndoto kubwa walizonazo ili waendelee kuishi maisha ya kawaida. Wanafanya kazi zao kwa muda wa kawaida na baada ya hapo hupumzika na kustarehe. Kinachotokea ni wanakuwa na maisha ya kawaida na ya chini kabisa.

    Chukua hatua; rafiki yangu amua leo ni kafara ipi unatoa, kuweka muda wako kwenye kazi na kuachana na starehe na anasa au kuendekeza starehe na anasa na kuzika ndoto yako?

    Rafiki chagua kwa usahihi halafu usiwe na malalamiko tena.

    Rafiki yako,

    Maureen Kemei.

    kemeimaureen7@gmail.com.

    uamshobinafsi.com.

  • Mambo 4 Ya Kuzingatia Ili Kupata Utulivu Wa Akili.

    Katika zama tunazoishi sasa zama zenye kelele na usumbufu wa kila aina, kupata utulivu wa akili ni kitu kigumu sana.

    Rafiki sina uhakika kama itakufaa, lakini iyo ni kwa sababu kila mtu anawinda umakini wako na kutaka kuteka akili yako.

    Hivyo basi, kupata utulivu wa akili lazima uzuie kelele na usumbufu visiingie kabisa kwenye akili yako.

    Unaweza kufanya hivyo kwa kuzingatia haya:

    1. Usifuatilie habari kwenye tv,redio,magazeti au mitandaoni.
    2. Ondoka kwenye mitandao ya kijamii.
    3. Usibishane na mambo ya siasa,michezo, dini au mapenzi.
    4. Usihangaike kufuatilia maisha ya watu maarufu.

    Unaweza kujiuliza utajuaje yale yanayoendelea kama hufuatilii habari. Kwanza mengi yanayoendelea kwenye habari kila siku siyo muhimu. Na yale muhimu kabisa lazima yatakufikia kupitia watu wengine.

    Njia bora ya kutumia akili yako ni kujifunza kupitia usomaji wa vitabu na makala zenye maarifa yenye tija na unayoweza kutumia kupiga hatua.

    Chuka hatua; rafiki unapaswa kujua kwamba habari zinazoenezwa ni hasi na za kusisimua, achana nayo.

    Rafiki wako,

    Maureen Kemei .

    kemeimaureen7@gmail.com.