Maisha yenye furaha ni maisha yenye maandalizi wakati wote, tunajifunza kupitia kwa wanajeshi wakati kuna amani na utulivu huwa wanafanya maandalizi ya vita.
Vivyo hivyo na sisi tunapaswa kufanya maandalizi ya hali ngumu wakati ambapo tuna hali nzuri. Mwanafalsafa Seneca anasema kuwa, licha ya kuwa na mali na kuweza kupata chochote unachotaka, mara mara tuishi kama watu tusioweza kupata vile tunavyotaka.
Licha ya kuwa na kitanda kizuri, mara kwa mara tunaweza kuchagua kulala chini. Hili likanikumbusha kisa cha Mwanafalsafa Aristotle ambaye alikuwa na tabia ya kulala chini mara kwa mara licha ya kuwa na kitanda.
Zoezi hili lilimkumbusha alikotoka na kumfanya asijisahu na kuanguka. Na sisi pia tunapaswa tuwe na zoezi tunalofanya kuwa sehemu ya maisha yetu, litatukumbusha tulikotoka na kutusaidia katika kubaki kwenye msingi sahihi hata baada ya kupata mafanikio.
Licha ya kuwa na gari binafsi, mara kwa mara unaweza kuchagua kutumia usafiri wa uma. Kwa kufanya mazoezi ya aina hii siyo tu utakuweka imara pale unapopoteza unachomiliki, bali pia itakufanya uthamini zaidi kile unachomiliki.
Unaweza kuwa umezoea sana kitanda chako, lakini siku moja ukilala chini, siku nyingine unapolala kwenye kitanda chako utashukuru mno.
Hatua ya kuchukua, amua kujiwekea misingi yako unayofuata kila siku, hata kama umefanikiwa kiasi gani. Hili litakusaidia ikiwa siku moja utapoteza kila kitu unachomiliki.
Akujaliaye sana.
Mshauri na Mwandishi.
Maureen Kemei.
Blog, kufikirichanya.wordpress.com
Email, kemeimaureen7@gmail.com