Rafiki yangu mpendwa sina uhakika kama itakufaa, lakini sis binadamu ni kama viumbe wa kihisia ila kuna wakati hutokea tunakuwa hatujiskii vizuri.
Katika nyakati hizo tunakuwa chini sana na tunakosa msukumo wa kufanya chochote. Derek kwenye kitabu chake cha Hell yeah or no, anatushirikisha maswali matano ya kujiuliza na kujibu ili kuweza kuondokana kwenye hali hizo.
Jiulize ni kitu gani hakipo sawa kwako kwa wakati huo. Je unaumwa au una maumivu yoyote? Je kuna hatari yoyote inayokukabili? Mara nyingi hapa jibu linakuwa ni hapana, huna maumivu, ugonjwa au hatari yoyote inayokukabili. Kwa sehemu kubwa ni akili yako inatengeneza vitu ambavyo havipo.
Angalia sasa. Chukua hatua baadaye. Usikimbilie kufanya maamuzi au kuchukua hatua yoyote pale unapokuwa unajiskia vibaya. Iangalie hiyo hali jinsi inavyokwenda na jipe muda kabla hujaamua au kufanya chochote. Hii inakupa nafasi ya hisia zinazokukabili katika hali hiyo kupita.
Kuza viwango vyako. Jiwekee viwango vya juu na kataa chochote ambacho hakijafikia viwango hivyo. Pale unapokuwa hujiskii vizuri, usikubali chochote chini ya viwango vyako kukufanya uzidi kutokujiskia vizuri.
Sehemu kubwa ya kufanya hii ni kwa watu, unapokuwa chini, wakatae watu ambao wanazidi kukushusha au kukushikilia chini. Jihusishe na wale tu wanaokuinua juu zaidi.
Weka mkazo kwenye malengo yako. Kwa kuondoa vitu vilivyo chini ya viwango vyako, unapata nafasi ya kuweka nguvu zaidi kwa yale yaliyo muhimu zaidi kwenye maisha yako.
Jikumbushe malengo yako makubwa uliyonayo na jifunze na chukua hatua katika kuyafikia. Mara nyingi unajiskia vibaya pale unapoacha kuyaangalia malengo yako na kuhangaika na yasiyokuwa na tija kwako
Fanya vitu vyote vya msingi. Hata kama unajisikia vibaya au uko chini kiasi gani, hakikisha mambo yote ya msingi kwenye maisha yako umeyafanya.
Hatua ya kuchukua; amka mapema jifanyie usafi, pata milo kamili, fanya mazoezi jifunze na lala mapema.
Kwa kutokuvuruga utaratibu wako wa kila siku, itakusaidia kuvuka hali hiyo kwa haraka. Lakini ukikubali kuvunja utaratibu wako, utabaki kwenye hali hiyo kwa muda mrefu.
Unapokuwa umeyafanya yale yote ya msingi kabisa na ukajiuliza nini hakipo sawa, jibu utalipata kwamba kila kitu kipo sawa. Na hapo hutakuwa tena na sababu ya kuendelea kujiskia vibaya na kuwa chini.
Akupendaye sana,
Maureen Kemei.
kemeimaureen7@gmail.com.