Umuhimu wa kuwaelewa wengine.

Rafiki yangu mpendwa tabia inayowafanya watu kuwa na ufanisi mkubwa ni kuwa msikilizaji mzuri kutoka kwenye kitabu cha habits of highly effective people.

Mwandishi anatueleza kuwa mawasiliano ni muhimu sana katika kila eneo la maisha, kuanzia kazi, biashara, ndoa, familia na hata urafiki.

Mawasiliano yamekuwa changamoto kwa wengi kwa sababu tunafundishwa kuongea, ila kuna kimoja muhimu sana huwa hatufundishwi nacho ni KUSIKILIZA.

Kusikiliza ni changamoto kubwa sana kwa wengi, kwanza wengi huwa hatusikilizi tunafikiria tutawajibuje wakishamaliza.

Watu wenye ufanisi mkubwa ni wasikilizaji wazuri sana, na hawasikilizi tu kwa masikio, lakini pia wanatumia macho yao na uelewa wao.

Wanajua sehemu kubwa ya mazungumzo haipo kwenye maneno yanayoongelewa, bali pia kwenye sauti na kwenye matendo ya mtu wakati anaongea lugha ya mwili.

Watu wenye ufanisi mkubwa wanatumia muda wao mwingi kuwasikiliza wengine, na wanasikiliza kwa lengo la kuwaelewa. Kwa njia hii wanajua ni nini hasa watu wanataka na hivyo kuweza kuwapatia au kuiboresha mahusiano zaidi.

Watu wenye ufanisi mkubwa, kabla hawajatoa maoni yao, kabla hawajatoa ushauri wao huwa wanasikiliza kwanza na kujua ni nini hasa kinawasilishwa pale. Wasiokuwa na ufanisi husikiliza juu juu na kukimbilia kuhukumu au kutoa ushauri, kitu ambacho kinaharibu kabisa mawasiliano yaliyopo.

Watu wasio na ufanisi mkubwa, husikiliza kwa kutumia uelewa wao wenyewe na huwa wanatumia njia hizi nne kuwajibu wale wanaowasiliana nao;

  1. Moja ni wanatathmini kile ambacho mtu anaongea, hivyo wanaamua kukubali au kukataa.
  2. Pili wanachimba zaidi kwa kuuliza maswali ya kuhoji, kutokana na uelewa wao wenyewe.
  3. Tatu wanashauri kulingana na uelewa wao na uzoefu wao wenyewe.
  4. Nne wanatafsiri, kujaribu kufikiria watu wana ni nini kingine wanataka au kinawasukuma.

Hatua ya kuchukua; Rafiki yangu boresha mawasiliano yako na wengine kwa kujifunza kuwa msikilizaji. Awe mtu yeyote yule, mteja,bosi wako, mfanyakazi wako, mwenza wako, mtoto wako.

Usikimbilie kutoa hukumu au kushauri, usimsikilize ukiwa tayari una upande wako, badala yake sikiliza kuelewa badala kuhitimu na hukumu.

Akupendaye sana,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.

By Maureen Kemei

Author, psychologist.

Leave a comment