Kwa Nini Aristotle Alilala chini.

Rafiki yangu mpendwa Robin anatueleza kwamba hakuna sumu ya mafanikio kama mafanikio. Wengi hupata anguko kubwa baada ya kupata mafanikio, kwa sababu hubadili maisha yao.

Kabla ya kufanikiwa wanaishi maisha ya kushambulia, wanajifunza, wanajaribu vitu vipya, wanaweka juhudi kubwa na hayo yanawapa matokeo makubwa.

Baada ya kufanikiwa wanaacha kushambulia na kuanza kulinda mafanikio waliyopata . Wanaacha kujifunza,wanaogopa kujaribu vitu vipya na hawajitumi tena kama awali. Kinachotokea ni kupoteza mafanikio waliyoyapata.

Robin anatushirikisha kwamba mwanafalsafa Aristotle alikuwa na tabia ya kulala chini mara kwa mara licha ya kuwa na kitanda. Zoezi hilo lilimkumbusha alikotoka na kumfanya asijisahahu na kuanguka.

Rafiki yangu tunapaswa pia kuwa na zoezi la kutukumbusha tulikotoka na tubaki kwenye misingi yetu hata baada ya kupata mafanikio makubwa.

Kuwa na msingi utakayoishi kila siku hata kama umefanikiwa kiasi gani. Endelea kuwa upande wa ushambuliaji, kwa kujifunza, kujaribu mambo mapya na kujituma kila wakati, kitu kitakachokusukuma ufanikiwe zaidi na zaidi.

Hata siku moja usijisifu kwamba umeshafika kwenye kilele cha mafanikio. Hata siku moja usijiambie umeshajua kila kitu.

Kuwa mnyenyekevu, ichukulie kila siku kama siku ya kwanza kwako na utapata mafanikio yanayozidi kukua siku baada ya siku.

Mwandishi wako,

Maureen Kemei.

kemeimaureen7@gmail.com.